Ezekieli 28

Ezekieli 28

Yatakayompata mfalme wa Tiro.

1Neno la Bwana likanijia la kwamba:[#Dan. 5:20; Tume. 12:23.]

2Mwana wa mtu, mwambie mfalme wa Tiro: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Moyo wako umejikuza kwamba: Mungu ni mimi, tena ninakaa pake Mungu baharini katikati! Kumbe nawe u mtu, hu Mungu, nawe moyo wako ukajiwazia kuwa kama moyo wa Mungu!

3Je? Wewe u mwerevu wa kweli kuliko Danieli, lisifichike jambo lo lote, usipolipambazua?[#Ez. 14:14; Dan. 4:9.]

4Kwa werevu wako wa kweli na kwa utambuzi wako ulijipatia mali, ukalimbika dhahabu na fedha katika maweko yako.

5Kwa kuwa mwenye werevu mwingi ulio wa kweli ukaziongeza sana mali zako kwa biashara zako, ulizozifanya; kwa hizo mali zako moyo wako ukajikuza.

6Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Kwa kuwa moyo wako unajiwazia kuwa kama moyo wa Mungu,

7kwa sababu hiyo utaniona, nikikupelekea wageni, ndio mataifa yenye ukali kupita wengine. Nao watazichomoa panga zao kupigana na uzuri wa werevu wako wa kweli, wauchafue uangafu wako.

8Watakusukuma, ushuke shimoni, nawe utakufa baharini katikati, kama waliopigwa na panga wanavyokufa.[#Ez. 26:20.]

9Je? Usoni pa mwuaji utasema tena: Mungu ni mimi? Nawe u mtu, hu Mungu, tena utakuwa mkononi mwake akupigaye kwa upanga.[#Ez. 28:2.]

10Utakufa mikononi mwa wageni, kama wanavyokufa wasiotahiriwa, kwani mimi nimeyasema; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.

11Neno la Bwana likanijia la kwamba:

12Mwana wa mtu, mtungie mfalme wa Tiro ombolezo! Mwambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Wewe ulikuwa kielelezo cha ulinganifu, tena mwenye werevu wa kweli mwingi na mwenye kuutimiza uzuri.[#Ez. 27:2.]

13Ukawa Edeni katika bustani ya Mungu, ukalipamba vazi lako kwa vito vya kila namna: sardio na topazio na yaspi na krisolito na oniki na berilo na safiro na ametisto na sumarato na dhahabu; siku hiyo ulipoumbwa, kazi za patu zako na filimbi zako zilikuwa zimetengenezwa, zikuwie tayari.

14Ukawa kama Kerubi aliyepakwa mafuta kuwa mlinzi, nikakuweka juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, ukawako ukitembea katika mawe yenye moto katikati.[#Yes. 14:14.]

15Ukawa pasipo kosa lo lote katika njia zako tangu siku ile, ulipoumbwa, mpaka upotovu ulipooneka kwako.

16Lakini kwa uchuuzi wako mwingi ukajaa makorofi ndani yako, ukakosa, nami nikakukimbiza kwenye mlima wa Mungu, kwa kuwa ulijipatia uchafu, nikakutowesha uliyekuwa kama Kerubi alindaye, uondoke katika yale mawe yenye moto.

17Moyo wako ulijikuza kwa ajili ya uzuri wako, ukauharibu werevu wako wa kweli kwa ajili ya uangafu wako; ndipo, nilipokubwaga chini, nikakutoa machoni pao wafalme, wakutumbulie macho.

18Kwa manza zako nyingi ulizozikora, tena kwa kupotoa uchuuzi wako, ulipatia Patakatifu pako uchafu; kwa hiyo nikatoa moto mwako katikati, ukakuteketeza, nikakutoa kuwa mavumbi ya nchi machoni pao wote waliokutazama.

19Wote waliokujua katika makabila ya watu hukustukia, kwa kuwa umegunduliwa na maangamizo, nawe hutakuwapo tena kale na kale.[#Ez. 27:36.]

Ufunuo wa maangamizo ya Sidoni.

20Neno la Bwana likanijia la kwamba:

21Mwana wa mtu, uuelekezee Sidoni uso wako na kuufumbulia yatakayokuwa![#Yes. 23:2,12.]

22Sema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikikujia, Sidoni, nijitokeze katikati yako kuwa mtukufu. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitakapouhukumu, nijulike mwake, ya kuwa ni mtakatifu.[#2 Mose 14:18.]

23Nitatuma kwake magonjwa mabaya na damu barabarani mwake, waangushwe mwake chini po pote waliopigwa kwa panga; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.

24Mlango wa Isiraeli hautaona tena miiba ya kuwachoma wala machomo ya kuwaumiza kwao wote wanaokaa na kuwazunguka waliowabeza; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu.

Wokovu wa Isiraeli.

25Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Nitakapowakusanya walio ukoo wa Isiraeli na kuwatoa kwenye makabila yote, walikotawanyikia, ndipo, nitakapoutokeza kwao utakatifu wangu, wao wa mataifa wauone; nao watakaa katika nchi yao, niliyompa mtumishi wangu Yakobo.

26Nao watakaa huko kwa kutulia, wajenge nyumba, wapande mizabibu; watakaa kwa kutulia, kwa kuwa nitawakatia mashauri kwao wote wanaokaa na kuwazunguka waliowabeza. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu wao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania