The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa 10 katika mwezi wa kumi siku yake ya kumi na mbili neno la Bwana likanijia la kwamba:
2Mwana wa mtu, mwelekezee Farao, mfalme wa Misri, uso wako na kumfumbulia yote yatakayomjia yeye nayo nchi yake yote nzima ya Misri![#Yes. 19; Yer. 46.]
3Sema ukimwambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikikujia, wewe Farao, mfalme wa Misri, uliye mamba mkubwa aoteaye katika majito yake katikati na kusema: Ni langu hili jito langu, nami nimelifanyizia kuwa langu![#Ez. 32:2.]
4Nitakutia ndoana kubwa katika taya zako, kisha nitawagandamanisha samaki wa majito yako magambani pako, nikupandishe na kukutoa ndani ya majito yako pamoja na samaki wote waliomo majitoni mwako, wakigandamana na magamba yako.[#Ez. 38:4; 2 Fal. 19:28.]
5Kisha nitakubwaga nyikani wewe pamoja na samaki wote waliokuwamo majitoni mwako, hutaokotwa wala hutakusanywa, ila nitakutoa, nyama wa porini na ndege wa angani wakule.
6Ndipo, wote wakaao Misri watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, kwa kuwa walikuwa kwao wa mlango wa Isiraeli kama mwanzi wa kujiegemezea.[#2 Fal. 18:21.]
7Lakini walipokushika mikononi mwao, ukakunjika, ukawapasua mabega yao yote; tena walipojiegemeza kwako, ukavunjika na kuvilemaza viuno vyao vyote.
8Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Utaniona, nikikupelekea panga, niangamize kwako watu na nyama.
9Ndipo, nchi ya Misri itakapokuwa peke yake kwa kuharibiwa, ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana, kwa kuwa alisema: Jito ni langu, mimi ndiye aliyelifanya.
10Kwa hiyo utaniona, nikikujia wewe, hata majito yako, niitoe nchi ya Misri, iharibiwe kabisa, mpaka iwe peke yake tu kuanzia Migidoli kufikisha Siwene hata mipaka ya Nubi.
11Hautapita kwake mguu wa mtu, wala mguu wa nyama hautapita kwake, wala hawatakaa watu miaka 40.
12Nitaitoa nchi ya Misri kuwa peke yake katikati ya nchi nyingine zilizo peke yao nazo, nayo miji yake itakuwa peke yao katikati ya miji mingine iliyo mabomoko tu, itakuwa hivyo miaka 40. Nao Wamisri nitawatawanya kwenye mataifa mengine na kuwatupatupa katika nchi zao.
13Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Miaka 40 itakapokwisha, nitawakusanya Wamisri na kuwatoa kwenye makabila ya watu, walikotawanyikia.
14Ndipo, nitakapoyafungua mafungo yao Wamisri, niwarudishe katika nchi ya Patirosi, ndiyo nchi, waliyozaliwa; ndiko, watakakokuwa ufalme ukaao chini tu.
15Katika nchi za kifalme nyingine itakaa chini tu, haitaweza kuyainukia mataifa tena, kwani nitawapunguza, wawe wachache tu, wasiyatawale mataifa.
16Wala hawatakuwa tena egemeo lao mlango wa Isiraeli la kunikumbusha manza, walizozikora walipowageukia kuwafuata. Ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana Mungu.
17Ikawa katika mwaka wa 27 siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, ndipo, neno la Bwana liliponijia la kwamba:
18Mwana wa mtu, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, amevitumikisha vikosi vyake utumishi mkubwa huko Tiro, mpaka vichwa vyote vikapata vipara, nayo mabega yote yakachubuka, lakini hakuna walichokipata huko Tiro, wala yeye wala vikosi vyake, kwa huo utumishi wao, waliomtumikia kule.
19Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Mtaniona, nikimpa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, nchi ya Misri, azichukue mali zao na kuyateka mateka yao na kuyapokonya mapokonyo yao; hayo yatakuwa mshahara wa vikosi vyake.
20Kwa kumlipa kazi zake, alizozitumikia huko, nitampa nchi ya Misri, kwa kuwa amenifanyizia kazi; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#Ez. 30:24; Yes. 10:5.]
21Siku ile nitakuza pembe kwao wa mlango wa Isiraeli, nami nitakupa kukifunua kinywa chako katikati yao; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.