Ezekieli 3

Ezekieli 3

Ezekieli analishwa kitabu kilichozingwa.

1Akaniambia: Mwana wa mtu, utakachokiona, kile! Ukile kitabu hiki kilichozingwa! Kisha nenda kusema na mlango wa Isiraeli![#Ez. 2:9.]

2Nikakifunua kinywa changu, akanilisha hicho kitabu cha kuzingwa.

3Akaniambia: Mwana wa mtu, lilishe tumbo lako, uyajaze matumbo yake hiki kitabu cha kuzingwa, mimi ninachokupa! Basi, nikakila, kikawa kitamu kinywani mwangu kama asali.

4Akaniambia: Mwana wa mtu, nenda, ufike kwao wa mlango wa Isiraeli, uwaambie niliyokuambia!

5Kwani wewe hutumwi kwa kabila lenye msemo mgumu na ndimi nzito, ila kwa mlango wa Isiraeli.

6Hutumwi kwa makabila mengi yenye misemo migeni na ndimi nzito, usizozisikia; kama ningekutuma kwao hao wangekusikia.

7Lakini hawa wa mlango wa Isiraeli watakataa kukusikia, kwani hawataki kunisika mimi, kwani mlango wote wa Isiraeli ndio wenye mapaji mashupavu na wenye mioyo migumu.

8Tazama: Nao uso wako nitaushupaza kuwa sawasawa kama zao, nalo paji lako nitalishupaza kuwa sawasawa kama yao.[#Yer. 1:18.]

9Kama almasi inavyoshupaa kuliko mwamba, ndivyo, nilivyolipa paji lako kuwa. Usiwaogope, wala usizistuke nyuso zao! Kwani ndio mlango mkatavu.

10Akaniambia: Mwana wa mtu, maneno yangu yote, nitakayokuambia, yaweke moyoni mwako ukiyasikia kwa masikio yako!

11Kisha nenda ufike kwao waliotekwa na kuhamishwa, walio wana wa ukoo wako, useme nao na kuwaambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema. Ikiwa wanasikia, au ikiwa wanaacha kusikia, basi.[#Ez. 2:5,7.]

Ezekieli anawekwa kuwa mlinzi wa Waisiraeli.

12Upepo ukanichukua, nikasikia nyuma yangu sauti ya uvumi mkubwa wa kwamba: Utukufu wa Bwana na utukuzwe hapo, alipo![#Ez. 8:3; Tume. 8:39.]

13Kukasikilika nako kuvuma kwa mabawa ya wale nyama, wakigusana na kuvuma, na kuvuma kwa yale magurudumu yaliyokuwako kwao, zikawa sauti za uvumi mkubwa.

14Upepo ukanichukua, ukanipeleka; nami nikaenda kwa uchungu wa kukasirika rohoni mwangu, nao mkono wa Bwana ulikuwa ukinishika kwa nguvu.

15Hivyo ndivyo, nilivyokuja Teli-Abibu kwao waliotekwa na kuhamishwa, waliokaa kwenye mto wa Kebari; huko walikokaa hao, ndiko, nilikokaa nami siku saba nikiwa kimya katikati yao kwa kushangaa.

16Hizo siku saba zilipopita, neno la Bwana likanijia la kwamba:

17Mwana wa mtu, nimekuweka kuwa mlinzi wa mlango wa Isiraeli. Hapo, utakaposikia neno kinywani mwangu, sharti uwaonye, wanisikie.[#Ez. 33:7-9; Yes. 52:8; Ebr. 13:17.]

18Ninapomwambia mtu asiyenicha: Utakufa, nawe usipomwonya, usiposema naye yeye asiyenicha, kwamba umwonye, aiache njia yake, umpatie kuwapo uzimani, basi, yeye asiyenicha atakufa kwa manza zake, alizozikora, lakini damu yake nitakulipisha, kwani itakuwa imeishika mikono yako.

19Lakini wewe unapomwonya asiyenicha, naye asipoyaacha mapotovu yake, asiporudi katika njia yake ipotokayo, basi, yeye atakufa kwa manza zake, alizozikora, nawe wewe utakuwa umeiokoa roho yako.

20Tena mwongofu anapouacha wongofu wake, afanye mapotovu, nitaweka mbele yake pa kujikwalia, naye atakufa. Ikiwa hukumwonya, atakufa kwa makosa yake, nayo maongofu yake, aliyoyafanya, hayatakumbukwa, lakini damu yake nitakulipisha, kwani itakuwa imeishika mikono yako.[#Ez. 18:24.]

21Lakini wewe unapomwonya mwongofu, asikose kwa kuwa mwongofu, naye akaacha kukosa, basi, atakaa uzimani, kwani ameonyeka, nawe utakuwa umeiokoa roho yako.

Ezekieli anauona tena utukufu wa Bwana.

22Ndipo, mkono wa Bwana ulipokuja kuwa juu yangu, akaniambia: Ondoka kwenda kwenye mbuga iliyoko bondeni! Ndiko, nitakakosema na wewe.[#Ez. 1:4.]

23Nikaondoka kwenda kwenye mbuga iliyoko bondeni, mara nikauona utukufu wa Bwana, ukisimama hapo, ulikuwa kama ule utukufu, niliouona kwenye mto wa Kebari, nikaanguka kifudifudi.

24Kisha roho ikanijia, ikanipa kusimama kwa miguu yangu. Akasema na mimi, akaniambia: Ingia nyumbani mwako, ufungiwe humo![#Ez. 2:2.]

25Nawe mwana wa mtu, utaona, wakikutia kamba, wakufunge nazo, usiweze kutoka katikati yao.

26Nao ulimi wako nitaugandamanisha na ufizi wako, uwe bubu, usiweze tena kuwaonya, kwani ndio mlango mkatavu.[#Ez. 2:5,7.]

27Lakini hapo, nitakaposema na wewe, nitakifumbua kinywa chako, uwaambie: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema. Mwenye kusikia atasikia; lakini mwenye kukataa atakataa vilevile, kwani ndio mlango mkatavu.[#Ez. 3:11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania