The chat will start when you send the first message.
1Ikawa katika mwaka wa 11 siku ya kwanza ya mwezi wa tatu, ndipo neno la Bwana liliponijia la kwamba:
2Mwana wa mtu, mwambie Farao, mfalme wa Misri, nao watu wake walio wengi: kwa ukuu wako unafanana na nani?
3Tazama, Mwasuri alikuwa mwangati wa Libanoni ulio mzuri kwa matawi yake yaliyo yenye majani mengi yenye kivuli, tena ni mrefu kwa kimo chake, kilele chake huyapita majani mengine ya miti iliyoko.[#Dan. 4:10-14.]
4Maji ndiyo yaliyoukuza hivyo, vilindi vya chini ndivyo vilivyouendesha juu, mito yao ikapitia po pote ulipopandwa, kisha vikavipeleka vijitojito vyao penye miti yote ya shambani.
5Kwa hiyo ulikua kuwa mrefu kwa kimo chake kuliko miti yote ya kondeni, matawi yake yakawa mengi, nayo machipuko yake yakawa marefu, ukiweza kuyachipuza vema kwa hayo maji mengi.
6Ndege wote wa angani walijenga matundu yao katika matawi yake, hapo chini ya machipuko yake wakazaa nyama wo wote wa porini, napo kivulini pake wakakaa mataifa mengi na mengi.
7Hivyo ulikuwa mzuri kwa ukubwa wake na kwa urefu wa matawi yake, kwani mizizi yake iko kwenye maji mengi.
8Katika bustani ya Mungu haukuwako mwangati ulioupita, wala mivinje haikufanana nao kwa matawi yao, wala migude haikuwa yenye machipuko kama huo; miti yote iliyoko bustanini kwake Mungu haikufanana nao kwa uzuri wake.
9Niliutengeneza kuwa mzuri kwa wingi wa matawi yake, kwa hiyo miti iliyoko Edeni bustanini kwake Mungu iliuonea wivu.
10Kwa hiyo Bwana Mungu anasema hivi: Kwa kuwa ulikuwa mrefu kwa kimo chake, kilele chake kikayapita majani ya miti iliyoko, ukajiwazia moyoni mwake kuwa mkuu kwa urefu wake.[#Ez. 28:2-10.]
11Lakini nitamtia mikononi mwake aliye peke yake mkuu wa mataifa, aufanyizie ayatakayo; kwa uovu wake nimekwisha kuutupa.
12Ndipo, wageni walio wakali kuliko mataifa mengine walipoukata, wakaubwaga, matawi yake yaanguke milimani na mabondeni po pote, nayo machipuko yake yakavunjika, yakawa katika makorongo yote ya nchi, nayo makabila yote ya nchi yakaondoka kivulini pake, wakauacha tu.
13Juu ya gogo lake lililoanguka watakaa ndege wote wa angani, nako kwenye machipuko yake watakuwako nyama wote wa porini.
14Itakuwa hivyo, kusudi miti yote iliyoko kwenye maji isijikuze, wala isipeleke vilele vyao juu kabisa kupita miti mingine yenye majani mengi, wala ile yenye nguvu isisimame kwa urefu wao na kuishinda yote mingine inyweshwayo, kwani yote imewekewa kufa, ifike mahali palipo chini ya nchi kwenye watu walioshuka shimoni.
15Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Siku ile, uliposhuka kuzimuni, naliviombolezesha vilindi vya maji vilivyoko ndani ya nchi nikivifunika kwa ajili yake huo, tena nikiizuia mito yao, yale maji mengi yakomeshwe, nayo milima ya Libanoni naliivika mavazi ya matanga, nayo miti yote ya kondeni ikazimia.
16Kwa uvumi wa kuanguka kwake nikayatetemesha mataifa, nilipoushusha kuzimuni pamoja nao washukao shimoni; ndipo, miti yote ya Edeni ilipotulizana pale mahali palipo chini ya nchi, ni ile miti ya Libanoni iliyochaguliwa kwa uzuri, ile yote iliyonyweshwa maji.[#Ez. 31:14.]
17Hii nayo ilishuka pamoja nao kuzimuni kwao waliouawa kwa panga, ndio waliokuwa mkono wake walipokaa kivulini pake katikati ya mataifa.
18Kwa hiyo umefanana na nani kwa utukufu na kwa ukuu kwenye miti ya Edeni? Pamoja na miti hii ya Edeni nawe utashushwa pale mahali palipo chini ya nchi, ulale kwao wasiotahiriwa pamoja nao waliouawa kwa panga. Huo ndio Farao na watu wake wote walio wengi. Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.