The chat will start when you send the first message.
1Neno la Bwana likanijia la kwamba:
2Mwana wa mtu, uelekeze uso wako kumtazama Gogi katika nchi ya Magogi aliye mkuu wa Rosi na wa Meseki na wa Tubali, umfumbulie yatakayomjia,[#Ez. 32:26; 39:1; Ufu. 20:8.]
3ukisema: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Utaniona, nikikujia wewe Gogi uliye mkuu wa Rosi na wa Meseki na wa Tubali.
4Nitakugeuza nikikutia hatamu katika taya zako, nikutoe katika nchi yako pamoja na vikosi vyako vyote, farasi nao wawapandao, wao wote watakuwa wamevaa nguo za urembo, nao watakuwa mkutano mkubwa wenye ngao kubwa na ndogo, nao wote watashika panga.[#Ez. 29:4.]
5Kwako unao Wapersia na Wanubi na Waputi, wao wote ni wenye ngao na kofia za vita.
6Wagomeri na vikosi vyao nao wa mlango wa Togarma wakaao kaskazini mbali sana na vikosi vyao, kweli ni makabila mengi, uliyo nayo.
7Jipangeni na kujiweka tayari, wewe na mikutano yako yote iliyokusanyika kwako, nawe uwe mlinzi wao!
8Siku zitakapopita nyingi, utakaguliwa; miaka iliyowekwa itakapokwisha, utakwenda katika nchi iliyopata nguvu tena kwa kupona madonda ya panga, ufike kwao waliokusanywa na kutolewa kwa makabila mengi, wakae tena katika milima ya Isiraeli, iliyokuwa siku zote mapori matupu. Wao ndio waliotolewa kwenye makabila mengine, wakae salama wote pamoja.
9Ndiko, utakakopanda, uwajie kama upepo wa chamchela, utaifunika hiyo nchi kama wingu, wewe na vikosi vyako vyote vya yale makabila mengi, uliyo nayo.
10Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Siku ile yatakuingia moyoni mambo yatakayokuwazisha mawazo mabaya.
11Ndipo, utakaposema: Nitapanda kwenda katika nchi iliyo wazi, nitaingia kwenye watu wanaotulia, wanaokaa salama; wote wanakaa pasipo boma, hawajui makomeo wala milango.[#Zak. 2:4.]
12Huko utataka kuteka mateka na kunyang'anya mali za watu, uinulie mkono wako mahame yanayokaa watu tena, uteke watu waliokusanywa na kutolewa kwenye mataifa, waliojipatia tena ng'ombe na mali nyingine, wanaokaa katikati ya dunia.[#Ez. 5:5.]
13Wasaba na Wadedani na wachuuzi wa Tarsisi na masimba yao wenye nguvu watakuuliza: Je? Umekuja kuteka mateka na kunyang'anya mali za watu? Umeikusanya mikutano yako kuchukua fedha na dhahabu, kujipatia ng'ombe na mali nyingine za watu, kuteka mateka mengi?
14Kwa hiyo, mwana wa mtu, mfumbulie Gogi yatakayompata ukimwambia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Siku hiyo, walio ukoo wangu wa Isiraeli watakapokaa salama, hutaijua?
15Ndipo, utakapoondoka mahali pako huko mbali kaskazini wewe na makabila mengi pamoja na wewe, wote ndio wapanda farasi, ni mkutano mkubwa na vikosi vingi.
16Utapanda kuwajia walio ukoo wangu wa Isiraeli, utaifunika nchi hiyo kama wingu. Siku zilizowekwa zitakapokwisha, nitakupeleka katika nchi yangu, kusudi wamizimu wapate kunijua mimi, nitakapojitokeza kuwa mtakatifu, nikikupatiliza, wewe Gogi, machoni pao.
17Hivi ndivyo, Bwana Mungu anavyosema: Kumbe si wewe, niliyemsema siku za kale kwa vinywa vya watumishi wangu, wale wafumbuaji wa Isiraeli, waliofumbua siku zile miaka kwa miaka, ya kuwa nitakupeleka wewe, uwajie?[#Yes. 24:21; 63:6; Yoe. 3:2,12; Sef. 3:8.]
18Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu: Siku ile, Gogi atakapoiingia nchi ya Isiraeli, ndipo, makali yangu yenye moto yatakaponipanda kuingia puani mwangu.
19Kwa wivu wangu na kwa moto wa machafuko yangu nasema: Siku hiyo itakuwa na tetemeko kubwa katika nchi ya Isiraeli.
20Kwa kuniona watatetemeka samaki wa baharini na ndege wa angani na nyama wa porini na vidudu vyote vitambaavyo katika nchi nao watu wote wanaokaa katika nchi; ndipo, milima itakapoporomoka, nayo magenge yataanguka, nayo maboma yote yataanguka chini.
21Kisha nitaziita panga katika milima yangu yote, zije kumpiga; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu; ndipo, upanga wa kila mtu utakapompiga ndugu yake.
22Nami nitampatiliza kwa magonjwa mabaya na kwa kumwaga damu zao, tena nitanyesha mvua ifurikayo maji na mvua ya mawe na ya moto uchanganyikao na mawe ya viberitiberiti; hizo mvua nitamnyeshea yeye na vikosi vyake na yale makabila mengi, aliyo nayo.[#Ufu. 20:9.]
23Hivyo nitajitokeza kuwa mkubwa na mtakatifu, nijulikane machoni pa wamizimu wengi, nilivyo; ndipo, watakapojua, ya kuwa mimi ni Bwana.[#Ez. 29:6.]