Ezekieli 4

Ezekieli 4

Mfano wa maumivu na wa makosefu yatakayoupata Yerusalemu.

1Wewe mwana wa mtu jipatie tofali, uliweke mbele yako! Kisha chora humo mji wa Yerusalemu!

2Kisha uuzungushie boma! Hilo boma ulijengee minara, ulizungushie hata ukingo wa mchanga! Tena uupigie po pote makambi ya askari, uweke nayo magogo ya kuvunjia boma!

3Kisha jipatie bati la chuma, kalisimamishe kuwa ukuta wa chuma wa kukutenga wewe nao mji! Kisha uuelekezee uso wako, kwamba uwe ukisongwa, nawe uwe mwenye kuusonga! Hiki ndicho kielekezo, mlango wa Isiraeli utakachokipata.

4Tena wewe ulalie ubavu wako wa kushoto, ukiisha ziweke manza za mlango wa Isiraeli juu yake; siku, utakazoulalia, zitahesabiwa kuwa siku za kuzichukua manza zao.

5Nami nitakupa miaka ya manza zao kuwa hesabu ya hizo siku, zitakuwa 390; ndizo, utakazozichukua manza za mlango wa Isiraeli.

6Utakapozimaliza hizo siku, uulalie ubavu wako wa kuume mara ya pili, uzichukue manza za mlango wa Yuda siku 40; kwa kila mwaka mmoja nimekupa siku moja.

7Tena uso wako utauelekezea Yerualemu uliosongwa, hata mkono wako, ukiisha kuuondoa nguo. Kisha sharti uufumbulie huo mji yatakayokuwa.

8Tena utaniona nikikufunga kwa kamba, usiweze kugeuka na kuulalia ubavu wa pili, mpaka uzimalize siku za kusongwa kwako.

9Tena jipatie ngano na mawele na maharagwe na choroko na mtama mweupe na mwekundu, uzitie zote katika chombo kimoja! Ndizo ujitengenezee mikate, kama hesabu ilivyo ya siku, utakazoulalia ubavu wako; siku 390 utaila hio mikate.[#Ez. 4:5.]

10Hicho chakula chako, utakachokila, utapimiwa kwa mizani kila siku ratli moja kaso robo muda kwa muda.

11Maji nayo utakunywa kwa kupimiwa, nusu kibaba kila siku moja, nayo utayanywa muda kwa muda.

12Hiyo mikate utaila, ikitengenezwa kama mikate ya mofa ya mawele, nawe sharti uichome kwa mavi ya choo cha mtu machoni pao.

13Bwana akasema: Kwenye mataifa, nitakakowatupa, wana wa Isiraeli, watavila vyakula vyao, vikiwa vichafu vivyo hivyo.

14Nikasema: E Bwana Mungu, tazama, roho yangu haijatiwa uchafu; tangu hapo, nilipokuwa mtoto, mpaka sasa sijala kibudu wala makombo ya nyama wa porini, wala yenye uvundo hayajaingia kinywani mwangu.[#Tume. 10:14.]

15Akaniambia: Tazama, nimekupa mavi ya ng'ombe penye mavi ya mtu, ndiyo utumie ya kuchomea mikate yako.

16Akaniambia: Mwana wa mtu, utaniona, nikilivunja shikizo la chakula mle Yerusalemu, wale vyakula vyao kwa kupimiwa na mizani na kwa kuvihangaikia; nayo maji watakunywa kwa kupimiwa na kwa kupigwa na bumbuazi,[#Ez. 5:16.]

17kwani watakosa vyakula na maji, wapigwe na bumbuazi wote pamoja, wakitoweshwa kwa ajili ya manza zao walizozikora.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania