Ezekieli 41

Ezekieli 41

Nyumba mpya ya Mungu.

(Taz. 1 Fal. 6.)

1Akanipeleka Patakatifu, akaipima miimo, upana ulikuwa mikono sita upande wa huku na mikono sita upande wa huko, ndio upana wa kuta za Nyumba.

2upana wa hapo pa kuingia ulikuwa mikono kumi napo hapo kando pa kuingia palikuwa mikono mitano upande wa huku na mikono mitano upande wa huko. Akaupima urefu wake, ulikuwa mikono arobaini, nao upana ulikuwa mikono ishirini.

3Akaingia chumba cha ndani, akaupima mwimo wa hapo pa kuingia ulikuwa mikono miwili, napo hapo pa kuingia palikuwa mikono sita, nao upana wa kando pa kuingia ulikuwa mikono saba.

4Kisha akaupima urefu wake, ulikuwa mikono ishirini, nao upana ulikuwa mikono ishirini, kama upande wa mbele wa Patakatifu ulivyokuwa. Akaniambia; Hapa ndipo Patakatifu Penyewe.[#Ez. 43:12.]

5Akaupima ukuta wa Nyumba, ulikuwa mikono sita; nao upana wa vyumba vya kando vilivyoizunguka Nyumba pande zote po pote ulikuwa mikono minne.

6Hivyo vyumba vya kando vilikuwa vitatu kwenda juu, kila kimoja juu ya kingine, tena vilikuwa kila mara thelathini kwenda mbele vikizunguka ukutani penye Nyumba kando, vipate kushikizwa humo, lakini havikushukizwa ndani ya ukuta wa Nyumba.

7Hivyo vyumba vya kando vilivyozunguka kila dari lao la juu viliongezwa kuwa vipana kuliko vya chini; kwa kuzunguka hivyo nayo Nyumba yenyewe, ulipoitazama nje, upande wake wa juu ulikwenda ukiongezwa pande zake zote. Mtu alipotaka kupandia vyumba vya juu alitoka penye vyumba vya chini, akapita penye vile vya kati, afike juu.

8Nilipoitazama Nyumba nikaona palipoinuka kuizunguka pande zote; ndipo, misingi ya vyumba vya kando ilipokuwa, urefu wao wa kwenda juu ulikuwa mwanzi mzima wa mikono sita mpaka juu ukingoni pake.

9Upana wa ukuta wa nje penye hivyo vyumba ulikuwa mikono mitano; napo katikati vile vyumba vya kando ya Nyumba vilipatiwa mahali pao.

10Napo mahali palipoizunguka Nyumba upana wake mpaka penye hivyo vyumba palikuwa po pote mikono ishirini.[#Ez. 42:1-3.]

11Milango ya kuviingilia vyumba vya kando uliwekwa mmoja upande wa kaskazini, tena mmoja upande wa kusini. Tena palikuwa mahali palipoachwa kujengwa kuizunguka Nyumba pande zote, upana wake ulikuwa mikono mitano.

12Nalo jengo lililokuwa hapo palipokatazwa watu, palipoelekea baharini upana wake ulikuwa mikono sabini, nao ukuta wa hilo jengo unene wake ulikuwa mikono mitano po pote kulizunguka, nao urefu wake mikono tisini.

13Akaipima Nyumba, urefu wake ulikuwa mikono mia, napo palipokatazwa watu na lile jengo na kuta zake pamoja urefu wao ulikuwa nao mikono mia.

14Nao upande wa mbele wa Nyumba napo palipokatazwa watu upande wa maawioni kwa jua upana wao nao ulikuwa mikono mia.

15Akaupima urefu wa lile jengo lililopaelekea hapo palipokatazwa watu, lililokuwa nyuma yake Nyumba, na baraza zake upande wa huku na upande wa huko, ulikuwa mikono mia.

Upande wa ndani wa hiyo Nyumba nazo kumbi za uani

16navyo vizingiti vyao na madirisha yao yenye vyuma na baraza zao zilizozunguka katika madari yale matatu na kukielekea hicho kizingiti zilikuwa zimefunikwa po pote kwa mbao nyembamba chini, tena kando mpaka penye madirisha, napo penye madirisha kando palikuwa pamefunikwa hivyo.

17Hapo juu penye mlango napo penye Nyumba upande wa ndani na wa nje katika kuta zote kuzunguka po pote ndani na nje palikuwa sawa.

18Tena palikuwa pamechorwa Makerubi na mitende hivyo: katikati mtende, tena hapa Kerubi na hapo Kerubi, kila mwenye nyuso mbili:

19uso wa mtu uliuelekea mtende upande wa huku, nao uso wa simba uliuelekea mtende upande wa huko; yalikuwa yamechorwa hivyo penye Nyumba yote kuizunguka pande zote.

20Toka chini mpaka juu ya mlango palikuwa pamechorwa Makerubi na mitende penye ukuta wa Nyumba.

21Hapo Patakatifu miimo ilikuwa yenye pembe nne, napo Patakatifu Penyewe, nilipopatazama, pakaoneka kuwa vivyo hivyo.

22Tena palikuwa na meza ya kutambikia iliyotengenezwa kwa mbao, urefu wa kwenda juu ulikuwa mikono mitatu, nao urefu wake wa kwenda mbele ulikuwa mikono miwili; pembe zake zilikuwa zimetokea nje, nao upande wa chini kwa urefu wake wote ulikuwa wa mbao, nazo kuta zake vilevile, akaniambia: Hii Meza ndiyo iliyoko mbele ya Bwana.[#2 Mose 30:1-10.]

23Palikuwa na milango miwili hapo Patakatifu, tena Patakatifu Penyewe.

24Hii milango miwili ilikuwa yenye mbao mbili zizungukazo, ambao mbili za mlango huu mmoja, tena mbao mbili za mlango ule mmoja.

25Napo penye milango hii ya Patakatifu palikuwa pamechorwa Makerubi na mitende, kama palivyochorwa kutani. Tena hapo upande wa mbele wa ukumbi wa nje palikuwa na baraza iliyotengenezwa kwa mbao za miti.

26Madirisha yenye vyumba na machoro ya mitende yalikuwa upande wa huku na upande wa huko penye kuta za ukumbi napo penye vyumba vya kando vya hiyo Nyumba napo penye zile baraza.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania