Ezekieli 8

Ezekieli 8

Matapisho ya kutambikia vinyago Patakatifu pa Bwana.

1Ikawa katika mwaka wa sita siku ya tano ya mwezi wa sita nilipokuwa nimekaa nyumbani mwangu pamoja na wazee wa Yuda waliokaa mbele yangu, ndipo, mkono wa Bwana Mungu uliponiangukia.[#Ez. 14:1.]

2Nilipotazama nikaona, kama ni sura ya mtu; toka hapo palipokuwa kama kiuno mpaka chini ni moto, tena toka penye kiuno mpaka juu kulionekana kuwa kama kumetuka kulikokuwa kama kwa shaba iliyong'aa sana.

3Kisha akakunjua kilichofanana na mkono, akanishika kishungi cha kichwani, upepo ukanichukua kuwa katikati ya nchi na ya mbingu, ukanipeleka Yerusalemu katika maono ya Kimungu pa kuliingilia lango la ndani lilioelekea kaskazini; ndipo, palipokuwa pamewekwa kinyago cha wivu kilichotia wivu.[#Ez. 3:12.]

4Nikauona hapo utukufu wa Mungu wa Isiraeli, kama nilivyouona katika ile mbuga ya bondeni.[#Ez. 1:4-28.]

5Akaniambia: Mwana wa mtu yaelekeze macho yako upande wa kaskazini! Nilipoyaelekeza macho yangu upande wa kaskazini, nikakiona hicho kinyago cha wivu kaskazini langoni pa kuingia penye meza ya kutambikia.

6Akaniambia: Mwana wa mtu, unayaona, hao wanayoyafanya? Ni machukizo makubwa, watu wa mlango wa Isiraeli wanayoyafanya hapa, niondoke Patakatifu pangu mwenda mbali. Tena utaona mengine yaliyo machukizo makubwa zaidi.

7Kisha akanipeleka langoni penye ua; nilipotazama nikaona tundu moja ukutani.

8Akaniambia: Mwana wa mtu, penya humu ukutani! Nikapenya mle ukutani, nikaona mlango mmoja.

9Akaniambia: Ingia, uyaone hayo machukizo mabaya, hao wanayoyafanya hapo!

10Basi, nikaingia; nilipotazama nikaona kila mfano wa wadudu na wa nyama watapishao, nayo magogo yote, wao wa mlango wa Isiraeli wanayoyatambikia, yalikuwa yamechorwa ukutani kupazunguka po pote.[#Rom. 1:23.]

11Mbele yao walikuwa wamesimama wazee 70 wa mlango wa Isiraeli, naye Yazania, mwana wa Safani, alisimama katikati yao; kila mtu alishika chetezo mkononi mwake, mvuke wa moshi wa uvumba ukapanda juu.

12Akaniambia: Umeyaona, mwana wa mtu, wazee wa mlango wa Isiraeli wanayoyafanya gizani kila mmoja katika vyumba vyake vya vinyago? Kwani husema: Hakuna Bwana anayetuona, Bwana ameondoka katika nchi hii.[#Ez. 9:9; Sh. 94:7.]

13Akaniambia: Utaona tena mengine yaliyo machukizo makubwa zaidi, hao wanayoyafanya.

14Akanipeleka penye lango la kuingia Nyumbani mwa Bwana lililoko upande wa kaskazini, nikaona humo wanawake waliokaa wakimlilia Tamuzi.

15Akaniambia: Umeyaona, mwana wa mtu? Utaona tena mengine yaliyo machukizo mabaya kuliko haya.

16Akanipeleka katika ua wa ndani wa Nyumba ya Bwana, nikaona hapo pa kuliingilia Jumba la Bwana katikati ya ukumbi na meza ya kutambikia waume kama 25, walikuwa wameligeuzia Jumba la Bwana migongo yao, lakini nyuso zilielekea upande wa maawioni kwa jua, wakiliangukia jua na kuyaelekea maawio yake.[#2 Mambo 29:6.]

17Akaniambia: Umeyaona, mwana wa mtu? Je? Kuyafanya haya machukizo, wanayoyafanya hapa, hakukuutoshea mlango wa Isiraeli? Imekuwaje, wakiieneza nchi makorofi ya kunikasirisha mara kwa mara? Watazame, jinsi wanavyoyashika yale machipuko ya miti mbele ya pua zao.

18Mimi nami nitawatolea makali yangu yenye moto; jicho langu halitawaonea uchungu, wala mimi sitawahurumia; ingawa wanililie masikioni kwa sauti kuu, sitawasikia kabisa.[#Yes. 1:15.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania