Ezera 4

Ezera 4

Wayuda wanazuiliwa kuendelea kuijenga Nyumba ya Mungu.

1Wapingani wao Wayuda na Wabenyamini waliposikia, ya kuwa waliorudi kwenye kutekwa wanamjengea Bwana Mungu wa Isiraeli Jumba,

2ndipo, walipomkaribia Zerubabeli nao waliokuwa vichwa vya milango, wakawaambia: Na tujenge pamoja nanyi! Kwani nasi tunamtumikia Mungu wenu kama ninyi, tunamtambikia tangu hapo, Esari-Hadoni, mfalme wa Asuri, alipotuleta huku, tukae.[#2 Fal. 17:24,33; 19:37.]

3Lakini Zerubabeli na Yesua nao wenzao wengine waliokuwa vichwa vya milango ya Isiraeli wakawaambia: Haipasi, ninyi na sisi tumjengee Mungu wetu Nyumba pamoja, ila sisi tunataka kumjengea Bwana Mungu wa Isiraeli Nyumba peke yetu, kama mfalme Kiro, mfalme wa Wapersia, alivyotuagiza.[#Ezr. 1:3.]

4Ndipo, wenyeji wa hiyo nchi walipoilegeza mikono ya Wayuda na kuwatia woga, wasiendelee kujenga.

5Wakawapenyezea viongozi fedha, walivunje hilo hauri lao, siku zote Kiro alipokuwa mfalme wa Wapersia, mpaka Dario alipoupata ufalme kuwa mfalme wa Wapersia.[#Ezr. 4:24.]

6Ahaswerosi alipoupata ufalme, katika siku za mwanzo wa ufalme wake wakaandika barua ya kuwashtaki waliokaa Yuda na Yerusalemu.

7Siku za Artasasta Bisilamu na Mitiridati na Tabeli na wenziwe wengine wakaandika barua kwa Artasasta, mfalme wa Wapersia; nayo maandiko ya barua hii yalikuwa yameandikwa Kishami, nayo maneno yake yalikuwa yamegeuzwa kuwa ya Kishami vilevile:

8Mwenye amri Rehumu na mwandishi Simusai waliandika barua moja kwa mfalme Artasasta kwa ajili ya Yerusalemu ya kwamba:

9Kale mwenye amri Rehumu na mwandishi Simusai na wenzao wengine waliandika barua, wao pamoja na Wadinai na Waafarsatiki, tena Watarpeli, Waafarsi, Waarkewi, Wababeli, Wasusaniki, Wadehai, Waelamu

10na makabila mengine, Osinapari aliyekuwa mwenye ukuu na utukufu aliowateka na kuwahamisha akiwakalisha katika miji ya Samaria na katika miji mingine iliyoko ng'ambo hii ya jito kubwa na penginepengine;[#Ezr. 4:2.]

11basi, huu ndio mwandiko wa pili wa barua yao, waliyoituma kwake:

Kwa mfalme Artasasta watumwa wako tunaokaa ng'ambo ya huku ya jito kubwa na penginepengine:

12Na ijulike kwa mfalme, ya kuwa Wayuda waliotoka kwako wapande kufika kwetu Yerusalemu, wanaujenga mji huu mbaya wenye ukatavu, boma lake wamelimaliza, nayo misingi yake wameitengeneza.

13Tena na ijulike kwa mfalme, ya kuwa mji huu ukijengwa, boma lake likimalizwa, watu wake hawatatoa kodi wala ushuru wa forodhani wala wa njiani, mwisho wafalme watapungukiwa fedha zao.

14Kwa kuwa tunakula chumvi ya jumba la mfalme, haitupasi kutazama tu, mfalme akiharibiwa mali zake, kwa hiyo tumetuma kumjulisha mfalme mambo haya.

15Sasa na wachunguze katika kitabu cha makumbusho ya baba zako. Ndipo, utakapoyaona humo kitabuni mwenye makumbusho, utajua, ya kuwa mji huu ni mji wenye ukatavu uliowaharibia wafalme nchi hata mali zao, hata mafujo wameyafanya kwao tangu siku za kale. Kwa sababu hii mji huo ukabomolewa.

16Sisi tunamjulisha mfalme, ya kwamba: Mji huu ukijengwa, nalo boma lake likimalizwa, basi, kwa hiyo hutakaa nalo hilo fungu la nchi lililoko ng'ambo ya huku ya jito kubwa.

17Ndipo, mfalme alipotuma jibu kwa mwenye amri Rehumu na kwa mwandishi Simusai na kwa wenzao wengine waliokaa Samaria na penginepo ng'ambo ya huko ya jito kubwa kwamba: Salamu na mengine yafuatayo!

18Barua, mliyoituma kwetu, imesomwa masikioni pangu neno kwa neno.

19Nami nikatoa amri, wayachunguze hayo; ndipo, walipoona, ya kuwa mji huo uliwainukia wafalme tangu siku za kale, hata mivurugo na mafujo yalifanyika humo.

20Nao Wafalme wenye nguvu walikuwamo Yerusalemu, wakazitawala nchi zote zilizoko ng'ambo ya huko ya jito kubwa, wakapewa kodi na ushuru wa forodhani na wa njiani.

21Kwa hiyo toeni amri ya kuwakataza watu hao, mji huo usijengwe, hata amri itakapotolewa na mimi.

22Nanyi mwangalie, msipoteze njia ya kulitengeneza jambo hili, wafalme wasipatwe na hasara kubwa wakipunguziwa mali zao!

23Papo hapo mwandiko wa pili wa barua ya mfalme Artasasta uliposomwa masikioni pao Rehumu na mwandishi Simusai na wenzao, ndipo, walipopiga mbio kwenda Yerusalemu kwa wayuda, wakawakataza majengo kwa ukorofi na nguvu.

24Hapo ndipo, zilipokoma kazi za Nyumba ya Bwana mle Yerusalemu, zikawa zimekoma mpaka mwaka wa pili wa ufalme wa Dario, mfalme wa Wapersia.[#Ezr. 4:5; 6:15.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania