Ezera 7

Ezera 7

Mfalme Artasasta anamsaidia Ezera.

1Mambo hayo yalipokwisha, Artasasta, mfalme wa Wapersia, akapata ufalme. Siku zile alikuwako Ezera, mwana wa Seraya, mwana wa Azaria, mwana wa Hilkia,[#1 Mambo 6:14.]

2mwana wa Salumu, mwana wa Sadoki, mwana wa Ahitubu,

3mwana wa Amaria, mwana wa Azaria, mwana wa Merayoti,

4mwana wa Zeraya, mwana wa Uzi, mwana wa Buki,

5mwana wa Abisua, mwana wa Pinehasi, mwana wa Elazari, mwana wa mtambikaji mkuu Haroni.

6Huyu Ezera akatoka Babeli, akapanda kuja kwao. Alikuwa mwandishi aliye fundi wa Maonyo ya Mose, Bwana Mungu wa Isiraeli aliyoyatoa; kwa kuwa mkono wa Bwana Mungu wake ulikuwa naye, mfalme akampa yote, aliyoyataka.[#Ezr. 7:9,28; 8:18,22; Neh. 2:8.]

7Wakapanda naye wana wa Isiraeli na watambikaji na Walawi na waimbaji na walinda malango na watumishi wa Nyumbani mwa Mungu kwenda Yerusalemu katika mwaka wa saba wa mfalme Artasasta.[#Ezr. 2:43.]

8Akafika Yerusalemu katika mwezi wa tano wa huo mwaka wa saba wa mfalme.

9Kwani siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza walianza kutoka Babeli na kupanda kwenda zao, tena siku ya kwanza ya mwezi wa tano akafika Yerusalemu, kwa kuwa mkono wa Mungu wake ulikuwa naye, ukamsaidia vema.[#Ezr. 7:6.]

10Kwani Ezera alikuwa ameuelekeza moyo wake kuyatafuta Maonyo ya Bwana, ayafanye, tena awafundishe Waisiraeli maongozi na maamuzi yapasayo.

11Huu ndio mwandiko wa pili wa ile barua, mfalme Artasasta aliyompa mtambikaji na mwandishi Ezera aliyeyajua vema maneno ya maagizo na ya Maonyo, Bwana aliyowapa Waisiraeli.

12Artasasta, mfalme wa wafalme, kwa mtambikaji Ezera anayeyajua vema maagizo ya Mungu wa mbingu: Salamu zote na mengine yafuatayo![#Ez. 26:7.]

13Mimi nimetoa amri kwamba: katika ufalme wangu kila aliye wa ukoo wa Isiraeli na watambikaji na Walawi, akitaka mwenyewe kwenda Yerusalemu, na aende na wewe!

14Kwani unatumwa na mfalme na wakuu wake saba wanaokula njama naye, uje kuyachunguza mambo ya Yuda na ya Yerusalemu, kama yanapatana na Maonyo ya Mungu wako yaliyomo mkononi mwako.

15Tena uzipeleke fedha na dhahabu, mfalme na wakuu wake wanaokula njama naye wanazozitoa kwa kupenda wenyewe, wampe Mungu wa Isiraeli anayekaa Yerusalemu;

16uzipeleke nazo fedha na dhahabu zote, utakazopewa katika mji wote wa Babeli pamoja na vipaji, watu na watambikaji wenyewe watakavyoitolea Nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu.

17Kwa hiyo ziangalie vema hizo fedha, kisha zitoe kununua madume ya ndama na madume ya kondoo na wana kondoo navyo vilaji na vinywaji vya tambiko; kisha vyote umtolee Mungu penye meza ya kutambikia katika Nyumba ya Mungu wenu iliyomo Yerusalemu!

18Kisha fedha na dhahabu zitakazosalia zitumieni, kama wewe na ndugu zako mtakavyoona kuwa vema vya kumtumikia Mungu wenu, apendezwe.

19Tena vyombo, ulivyopewa vya kutumikia Nyumbani mwa Mungu wako, vyote uvipeleke Yerusalemu kuviweka mbele ya Mungu.

20Nayo mengine yote, Nyumba ya Mungu wako itakayopaswa nayo, nayo malipo yote yatakayokuangukia wewe, utayapata nyumbani mwenye vilimbiko vya mfalme.

21Tena mimi mfalme Artasasta ninawatolea amri watunza mali wote walioko ng'ambo ya huko ya jito kubwa kwamba: Yote, mtambikaji Ezera anayeyajua vema Maonyo ya Mungu wa mbingu atakayowaomba ninyi, yafanyike sawasawa,

22mpaka yapate vipande mia vya fedha, ndio milioni ya shilingi na frasila elfu za ngano na frasila mia za mvinyo na frasila mia za mafuta, tena chumvi pasipo kipimo cho chote.

23Yote, watakayoyataka kwa amri ya Mungu wa mbingu, sharti yafanyike vizuri, kwa kuwa ni ya Nyumba ya Mungu wa mbingu, ufalme wa mfalme na wanawe wasipatwe na makali yake.

24Nayo hii ijulike kwenu, ya kuwa hakuna ruhusa kabisa ya kuwatoza kodi, wala ushuru wa forodhani wala wa njiani, walio watambikaji na Walawi na waimbaji na walinda malango na watumishi wa Nyumbani nao wengine wanaoitumikia Nyumba hiyo ya Mungu.

25Kisha wewe Ezera kwa hivyo, unavyomjua Mungu wako kwa kweli, weka waamuzi na wenye kukata mashauri, wawakatie mashauri yao walio wa ukoo huu wote wanaokaa ng'ambo ya huko ya jito kubwa, wao wayajuao Maonyo ya Mungu wako, nao wasioyajua wawafundishe!

26Lakini kila mtu asiyeyafanya maagizo ya Mungu wako, nayo maagizo ya mfalme, sharti apatilizwe kwa ukali, kama ni kuuawa au kuhamishwa au kutozwa fedha au kufungwa.

27Bwana Mungu wa baba zetu na atukuzwe kwa kumpa mfalme moyoni mwake mawazo kama hayo, aipambe Nyumba ya Bwana iliyomo Yerusalemu!

28Mimi amenipatia upendeleo mbele ya mfalme na mbele ya wakuu wake wanaokula njama naye na mbele ya wakuu wote wa mfalme walio na nguvu; kwa hivyo, mkono wa Bwana Mungu wangu ulivyokuwa na mimi, nimejipa moyo wa kukusanya wakuu wa milango ya Waisiraeli, waje kupanda kwenda kwetu pamoja na mimi.[#Ezr. 7:6.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania