Wagalatia 6

Wagalatia 6

1Ndugu, mtu akipatikana ameanguka, ninyi mlio wa Kiroho, mwonyeni Kiroho kwa upole, ashupae tena! Jiangalie mwenyewe, usijaribiwe nawe![#Mat. 18:15; Yak. 5:19.]

2Mchukuliane mizigo! Hivyo mtayatimiza Maonyo yake Kristo.[#2 Kor. 11:29.]

3Kwani mtu akijiwazia kuwa mwenye nguvu, tena siye, hujidanganya mwenyewe.

4Lakini kila mtu azitazame kazi zake mwenyewe, ziwe nzuri! Ndipo, atakapojivuma moyoni tu, asitolee wengine majivuno yake.[#2 Kor. 13:5.]

5Kwani kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe.[#Rom. 14:12.]

Tutavuna, tuliyoyapanda.

6Lakini mwenye kufundishwa lile Neno na amgawie mfunzi mema yote, aliyo nayo![#1 Kor. 9:14.]

7Msidanganyike, Mungu habezwi! Kwani mtu aliyoyapanda, ndiyo, atakayoyavuna.

8Maana mwenye kupanda mwilini mwake atavuna humo mwilini kuoza. Lakini mwenye kupanda Rohoni atavuna humo Rohoni uzima wa kale na kale.[#Rom. 8:13.]

9Tusichoke kuyafanya yaliyo mazuri, kwani siku zake zitakapotimia, tutavuna pasipo kukoma.[#2 Kor. 4:1; 2 Tes. 3:13.]

10Basi, kwa sababu tuko nchini bado, wote na tuwatendee mema, lakini kuliko wengine wenzetu wa kumtegemea Bwana!*[#2 Petr. 1:7.]

Tukuzo la msalaba wake Yesu Kristo.

11Yatazameni haya maandiko yote, niliyowaandikia kwa mkono wangu mimi!

12Wote wanaotaka kupendeleza miili, hao huwashurutisha kutahiriwa; tena hapana neno jingine, ni kwamba tu: Wasifukuzwe kwa ajili ya msalaba wake Kristo.[#Gal. 5:11; Fil. 3:18.]

13Kwani nao wenyewe waliotahiriwa hawayashiki Maonyo, ila hutaka, ninyi mtahiriwe, wapate kujivunia miili yenu.

14Lakini mimi sitaki kujivuna, isipokuwa kwa ajili ya msalaba wake Bwana wetu Kristo, maana mlemle mimi nimefiwa na ulimwengu, nao ulimwengu umefiwa na mimi mlemle.[#1 Kor. 1:31; 2:2.]

15Kwani ukiwa naye Kristo Yesu, kutahiriwa siko, wala kutotahiriwa siko, ila kuwa kiumbe kipya ndiko.[#Gal. 5:6; 1 Kor. 7:19.]

16Nao wote wanaoendelea na kujipingia hivyo na watengemane, upole uwakalie pamoja nao Waisiraeli wa Mungu![#Sh. 125:5.]

17Basi, tangu sasa asionekane atakayenisumbua tena! Kwani mwilini mwangu mimi ninayo makovu ya Yesu.[#2 Kor. 4:10.]

18Upole wa Bwana wetu Yesu Kristo uzikalie roho zenu, ndugu! Amin.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania