1 Mose 21

1 Mose 21

Kuzaliwa kwake Isaka.

1Bwana akamkagua Sara, kama alivyosema; naye Bwana akamfanyizia Sara, kama alivyomwagia.[#1 Mose 18:10; Ebr. 11:11.]

2Kwa hiyo Sara akapata mimba, akamzalia Aburahamu mtoto mume katika uzee wake siku zizo hizo, Mungu alizomwagia.

3Mwanawe aliyezaliwa, Sara aliyemzaa, Aburahamu akamwita jina lake Isaka (Acheka).[#1 Mose 17:19.]

4Huyu mwanawe aburahamu akamtahiri, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwagiza.[#1 Mose 17:11-12.]

5Naye Aburahamu alikuwa mwenye miaka 100, mwanawe Isaka alipozaliwa.[#1 Mose 17:17; Rom. 4:19.]

6Naye Sara akasema: Mungu amenipatia kuchekwa, kwani kila atakayevisikia atanicheka.[#1 Mose 18:12.]

7Akasema tena: Yuko nani aliyemwambia Aburahamu: Sara atanyonyesha wana? Kwani nimezaa mwana katika uzee wake.

8Mtoto alipokua akakomeshwa kunyonya; siku hiyo, Isaka alipoacha kunyonya, Aburahamu akafanya karamu kubwa.

Kufukuzwa kwake Isimaeli.

9Sara alipomwona yule mwana wa Mmisri Hagari, aliyemzalia Aburahamu kuwa mfyozaji,

10Akamwambia Aburahamu: Mfukuze huyu kijakazi pamoja na mwanawe! Kwani mwana wa huyu kijakazi hatapata urithi pamoja na mwanangu Isaka.[#Gal. 4:30.]

11Neno hili likawa baya sana machoni pake Aburahamu kwa ajili ya mwanawe,

12lakini Mungu akamwambia Aburahamu: Neno hilo lisiwe baya machoni pako kwa ajili ya huyo kijana na huyo kijakazi wako! Yote, Sara atakayokuambia, mwitikie sauti yake! Kwani watakaoitwa uzao wako ni wa Isaka tu.[#Rom. 9:7-8; Ebr. 11:18.]

13Lakini mwana wa kijakazi naye nitamweka kuwa taifa zima, kwani naye ni uzao wako.[#1 Mose 17:20.]

14Kesho yake Aburahamu akaamka na mapema, akachukua mkate na kibuyu cha maji, akampagaza Hagari begani, kisha akampa na mwanawe; ndivyo, alivyompa ruhusa kwenda zake. Lakini alipokwenda akapotea katika nyika ya Beri-Seba.

15Maji yalipokwisha kibuyuni, akamwacha mwanawe chini ya kijiti,

16akaenda kukaa peke yake na kumwelekea mbali kidogo kama hapo, mtu anapotupa mshale kwa upindi, kwani alisema: Nisione, mwana anavyokufa! Alipokaa hivyo na kumwelekea akapaza sauti yake, akalia.

17Mungu alipokisikia kilio cha mtoto, malaika wa Mungu akamwita Hagari toka mbinguni, akamwambia: Una nini, Hagari? Usiogope! Kwani Mungu amekisikia kilio cha mtoto hapo, anapolala.

18Inuka, umwinue mtoto na kumshika kwa mkono wako! Kwani nitamfanya kuwa taifa kubwa.

19Kisha Mungu akamfumbua macho; ndipo, alipoona kisima cha maji, akaenda kukijaza kile kibuyu, akampa mtoto, anywe.

20Mungu akawa na huyu mtoto, akakua, akakaa nyikani, akawa mpiga upindi.

21Akakaa katika nyika ya Parani; naye mama yake akamwoza mwanamke wa nchi ya Misri.[#1 Mose 16:3.]

Maagano ya Aburahamu na Abimeleki.

22Ikawa wakati huo, ndipo, Abimeleki na Pikoli, mkuu wa vikosi vyake, walipomwambia Aburahamu kwamba: Mungu yuko pamoja na wewe katika mambo yote, unayoyafanya.[#1 Mose 26:26.]

23Sasa niapie na kumtaja Mungu kwamba: Hutanidanganya mimi wala wao wa uzao wangu wajao nyuma yangu, ila huo wema, niliokufanyia wewe, unifanyie mimi nayo nchi hii, unayoikaa ugeni![#1 Mose 20:15.]

24Aburahamu akasema: Basi, mimi nitaapa.

25Kisha Aburahamu akamwonya Abimeleki kwa ajili ya kisima cha maji, watumishi wake Abimeleki walichokinyang'anya.[#1 Mose 26:15,18.]

26Naye Abimeleki akasema: Simjui aliyelifanya jambo hilo, wewe nawe hujanipasha habari, mimi nami sijavisikia, ni leo hivi tu.

27Kisha Aburahamu akachukua mbuzi na kondoo na ng'ombe, akampa Abimeleki; hivyo ndivyo, wao wawili walivyofanya agano.

28Aburahamu akaweka wana kondoo saba peke yao,

29naye Abimeleki akamwuliza Aburahamu: Hawa wana kondoo saba ukiwaweka peke yao, ni wa nini?

30Akajibu: Hawa wana kondoo saba wa kike wachukue mkononi mwangu, upate kunishuhudia, ya kuwa nilikichimbua kisima hiki.

31Kwa sababu hii wakapaita mahali pale Beri-Seba (Kisima cha Kiapo), kwa kuwa waliapiana hapo wote wawili.[#1 Mose 26:33.]

32Walipokwisha kulifanya agano hilo hapo Beri-Seba, Abimeleki na Pikoli, mkuu wa vikosi vyake, wakaondoka, wakarudi katika nchi ya Wafilisti.

33Aburahamu akapanda mvinje hapo Beri-Seba, akalitambikia hapo Jina la Bwana aliye Mungu wa kale na kale.[#1 Mose 12:8; Yes. 40:28; Rom. 16:26.]

34Aburahamu akakaa ugenini katika nchi ya Wafilisti siku nyingi.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania