Habakuki 2

Habakuki 2

Wamtegemeao Mungu wanatulizwa mioyo.

1Na nije kusimama pangu pa kulindia,

ningoje zamu mnarani juu!

Na nichungulie, nione, atakayoniambia,

niyajue, nitakayoyajibu kwa ajili ya malalamiko yangu.

2Bwana akaniitikia, akaniambia: Liandike, uliloliona,

ulichore katika vibao, watu wapate kulisoma mumo humo upesi.

3Kwani hilo ono liko na siku zake, hazijatimia bado,

lakini linajihimiza kumalizika, haliongopi.

Ingawa likawie, lingojee! Kwani halina budi kuja, halitachelewa.

4Utaona, moyo wake umejitutumua wenyewe, haunyoki;

lakini mwongofu atapata uzima kwa kumtegemea Mungu.

Wenye majivuno wataangamia.

5Kweli mvinyo hudanganya:

mtu mwenye majivuno hawezi kutulia,

ingawa aupanue moyo wake kuwa kama kuzimu,

ingawa awe kama kifo, hawezi kushiba,

sharti akusanye kwake mataifa yote,

kweli sharti ayapeleke kwake makabila yote ya watu.

6Je? Hao wote hawatamtungia mafumbo

ya kumsimanga na kumfyoza kwamba:

Yatampata achukuaye mengi yasiyo yake!

Ataviweza mpaka lini?

Hata mizigo mizima ya mali, wengine walizompa, awawekee,

amejipa, ziwe zake.

7Je? Hawatainuka kwa mara moja, wakuumize?

Hawataamka, wakusumbue? Ndipo, utakapotekwa nao!

8Kwa kuwa wewe ulipokonya mali za mataifa mengi,

kwa hiyo wao wa masao ya makabila yote watazipokonya mali zako,

wazilipize damu ya watu, ulizozimwaga,

wakulipishe nayo makorofi,

ambayo uliitendea nchi na miji na wenyeji wao wote.

9Yatampata aupatiaye mlango wake mapato mabaya,

apate kujitengenezea kiota juu kwamba:

ajiepushe mikononi mwao wabaya.

10Mashauri yako yatautia mlango wako soni:

ulipoangamiza makabila mengi, umeikosesha roho yako.

11Kwani majiwe yaliyomo ukutani yatapiga kelele,

nayo miti ya kipaga itaitikia.

12Yatampata ajengaye miji kwa damu

na kuishupaza mitaa yake kwa mapotovu!

13Je? Hamjayaona yatokayo kwake Bwana Mwenye vikosi?

Namwone: Makabila ya watu waliyoyasumbukia, huliwa na moto,

nayo, mataifa waliyoyafanyia kazi na kujichokesha, huwa ya bure.

14Kwani nchi hii itajazwa nao waujuao utukufu wa Bwana,

kama maji yanavyofurikia baharini na kuyafunika yote

15Yatampata amnyweshaye mwenziwe kinywaji,

alichokichanganya na makali yake!

Kisha anamlewesha, kusudi auone uchi wake na kumfurahia!

16Umejishibisha yatiayo soni ukiyaacha yenye utukufu,

lakini wewe nawe sharti unywe,

ujulikane kuwa mtu asiyetahiriwa.

Kikombe kilichomo kuumeni mwa Bwana kinakufikia,

utukufu wako ufunikwe nayo yenye soni.

17Kwani makorofi, ambayo uliitendea Libanoni, yatakufunika,

nao nyama, uliowaua bure tu, watakutia woga,

kwa ajili ya damu za watu, ulizozimwaga

kwa kuikorofisha nchi na miji pamoja na wenyeji wao wote.

18Hapo kinyago kilichochongwa kitafaaje?

Maana ni kazi tu ya fundi aliyekichonga.

Au kinyago cha vyuma vilivyoyeyushwa

kifundishacho uwongo tu kitafaaje?

Maana ni egemeo lake fundi aliyekitengeneza,

apate miungu isiyosema.

19Yatampata akiambiaye kipande cha mti: Amka!

naye akiambiaye kipande cha jiwe lisilosema: Inuka!

Je? Hicho kitaweza kufumbua neno?

Kitazame! Kimefunikwa na dhahabu na fedha,

lakini ndani yake hamna pumzi yo yote.

20Lakini Bwana yumo Jumbani mwake mwenye utakatifu,

usoni pake kila mtu wa nchi hii anyamaze kimya!

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania