Waebureo 10

Waebureo 10

Kufa kwake Kristo ni ng'ombe ya tambiko inayotimiliza.

1Maonyo hufanana, kama ni kivuli tu cha yale mema yatakayotokea, wala siyo sura yao yenyewe, ni kufanana tu nayo. Navyo vipaji vya tambiko, walivyovipeleka kila mwaka, ni vivyo hivyo kale na kale, navyo haviwezi kuwapa utimilifu wenye kuvitoa.[#Ebr. 7:19; 8:5; Kol. 2:16-17.]

2Je? Hao wenye kutambika wakiisha kutakaswa mara moja, kama wasingejua mioyoni kwamba: Makosa yako, hawangeacha kupeleka vipaji vya tambiko?

3Lakini hivyo vipaji vya tambiko ndivyo vinavyowakumbusha makosa yao mwaka kwa mwaka,[#3 Mose 16:21,34.]

4kwani damu za ng'ombe na za mbuzi haziwezi kuondoa makosa.

5Kwa hiyo anasema anapoingia ulimwenguni:

Ng'ombe na vyakula vya tambiko hukuvitaka;

lakini umenitengenezea mwili.

6Ng'ombe za tambiko zinazoteketezwa nzima

navyo vipaji vya kulipa makosa hukupendezwa navyo.

7Ndipo, niliposema: Tazama, ninakuja!

Mambo yangu yameandikwa katika kitabu cha kale,

niyafanye, uyatakayo wewe, Mungu.

8Kwanza anasema: Ng'ombe na vyakula vya tambiko, nazo ng'ombe za tambiko zinazoteketezwa nzima, navyo vipaji vya kulipa makosa hukuvitaka, wala hukupendezwa navyo, tena hutolewa, kama vilivyoagizwa.

9Kisha alisema: Tazama, ninakuja, nifanye uyatakayo wewe. Hivyo analitangua lile la kwanza, apate kulisimamisha lile la pili.

10Kwa hayo, aliyoyataka, tumetakaswa, kwani mwili wake Yesu Kristo ulitolewa mara moja.[#Ebr. 9:12,28; Ebr. 10:1; 2 Mose 29:38.]

11Kila mtambikaji husimama siku kwa siku akitambika, navyo vipaji vya tambiko, anavyovitoa mara nyingi, ni vivyo hivyo visivyoweza kabisa kuondoa makosa.

12Lakini huyu alitoa kipaji kimoja tu cha tambiko kwa ajili ya makosa ya watu, nacho ni cha kale na kale, kisha aliketi kuumeni kwa Mungu.[#Ebr. 10:10,14.]

13Sasa anangoja tu, adui zake wawekwe chini miguuni pake.[#Sh. 110:1.]

14Kwani kwa kukitoa kile kipaji chake kimoja cha tambiko amewapa wenye kutakaswa utimilifu ulio wa kale na kale.[#Ebr. 10:12.]

15Naye Roho Mtakatifu anatushuhudia hivyo. Kwani kwanza anasema:

16Bwana anasema:

Agano, nitakalolifanya nao,

siku hizi zitakapokuwa zimepita, ni hili:

Nitawapa maonyo yangu, yakae mioyoni mwao;

tena nitayaandika katika mawazo yao.

17Sitayakumbuka tena makosa yao na mapotovu yao.[#Ebr. 8:12; Yer. 31:34.]

18Basi, hayo yanapoondolewa, hapo hapana tena kutoa kipaji cha tambiko kwa ajili ya ukosaji.

Kwa hiyo tumkaribie Mungu pasipo woga!

19*Ndugu, changamko letu la sasa ni hili la kwamba: Tunayo njia inayotuingiza Patakatifu, ni damu ya Yesu;[#Mat. 27:51; Rom. 5:2.]

20njia hii ni ya siku hizi, tena inatupa uzima; yeye ameifungua hapo, alipopaingia Patakatifu Penyewe, ni hapo, alipoutoa mwili wake.[#Ebr. 9:8.]

21Kwa hiyo tunaye mtambikaji mkuu wa Nyumba ya Mungu.

22Basi, na tumwendee kwa mioyo yenye kweli, inayojikaza kumtegemea! Kwa hivyo, tulivyonyunyizwa mioyo, isijue tena ubaya, tena kwa hivyo, miili yetu ilivyooshwa kwa maji yatakatayo,[#Ebr. 4:16; Ef. 5:26; 1 Petr. 3:21.]

23na tufulize kukiungama kingojeo chetu, tusichoke! Kwani yeye aliyetupa kiagio chake ni mwelekevu.[#Ebr. 4:14.]

24Tena tuangaliane, tupate kuhimizana, tupendane kwa kufanya matendo mazuri![#Ebr. 13:1.]

25Kisha tusiache makutano yetu, kama wengine walivyojizoeza, ila tuonyane! Tena tukaze kuonyana kwa hivyo, tunavyoona: Siku ile inakaribia!*[#Ebr. 3:13; 10:37; Rom. 13:11-12.]

Mtu asiubeze upole!

26Kwani sisi tuliokwisha kuyatambua yaliyo ya kweli tukikosa tena kwa kuyapenda makosa, hakuna kipaji cha tambiko tena kilichotusalia cha kuondoa makosa,[#Ebr. 6:4-8.]

27ila kinachotusalia ni woga wa kuingoja hukumu na ukali wa moto utakaowala wabishi.

28Mtu ayatanguaye Maonyo ya Mose huuawa pasipo kuonewa uchungu, akisutwa na mashahidi wawili au watatu.[#4 Mose 15:30; 5 Mose 17:6.]

29Tena je? Silo lipizi baya kuliko hilo limpasalo mtu, aliyemponda Mwana wa Mungu na kuiwazia damu ya Agano, aliyotakaswa nayo, kwamba: Haifai kitu? Huko siko kumkorofisha Roho aliyemgawia mema?[#Ebr. 2:3.]

30Kwani twamjua aliyesema:

Lipizi ni langu mimi, ni mimi nitakayelipisha.

Na tena:

Bwana atawaamulia walio ukoo wake.

31Kunatia woga sana kutumbukia mikononi mwa Mungu aliye Mwenye uzima.

Kilimbiko chetu.

32*Lakini mzikumbuke siku za kwanza, mlipoangazwa! Hapo mlivumilia mapigano mengi mkiteseka.[#Ebr. 6:4.]

33Siku nyingine mkatolewa wenyewe kutazamwa na watu, mkitukanwa pamoja na kuumizwa, siku nyingine mliwatazama wenzenu, wakifanyiziwa hivyo.[#1 Kor. 4:9.]

34Kwani wale waliofungwa mliteseka pamoja nao; nanyi mliponyang'anywa, mliyokuwa nayo, mliitikia na kufurahi, kwani mlitambua, ya kuwa mnacho kilimbiko kiyapitacho yale kuwa kizuri, maana hakichakai.[#Mat. 6:20; 19:21,29.]

Mwongofu ataishi kwa kumtegemea Mungu.

35Basi, msikitupe kingojeo chenu! Kwani kitawapatia malipo makubwa.

36Lakini mnapaswa na uvumilivu, myafanye, Mungu ayatakayo, myapokee yale, mliyoagiwa.[#Luk. 21:19.]

37Kwani

pamesalia padogo penyewe,

patokee mwenye kuja, hatakawia.

38Naye mwongofu wangu atapata uzima kwa kunitegemea.

Lakini atakayerudi nyuma hataipendeza roho yangu.

39Lakini sisi hatu wenye kurudi nyuma, tuangamie, ila wenye kumtegemea, tuziokoe roho zetu.*

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania