Waebureo 11

Waebureo 11

Kumtegemea Mungu kulivyo.

1Kumtegemea Mungu ni kuyatumaini, tunayoyangojea, pasipo kuyaonea mashaka yasiyonekana bado.[#2 Kor. 5:7.]

2Kwani wakale walishuhudiwa kuwa wenye kumtegemea hivyo.[#Ebr. 11:4-5,39.]

Jinsi Abeli na Henoki na Noa walivyomtegemea Mungu.

3Kwa kumtegemea Mungu twajua, ya kuwa ulimwengu ulitengenezwa kwa Neno lake Mungu, mtu asiseme: Tunavyoviona kwa macho, vilipata kuwapo kwa nguvu yao vile vinavyoonekana.[#1 Mose 1.]

4Kwa kumtegemea Mungu Abeli alimtolea Mungu kipaji cha tambiko kilichokuwa kikubwa kuliko chake Kaini, akashuhudiwa nacho kuwa mwongofu, kwani Mungu alipendezwa na vipaji vyake. Naye angawa amekufa, kwa hiyo anasema bado.[#1 Mose 4:4; Mat. 23:35.]

5Kwa kumtegemea Mungu Henoki alichukuliwa, asione kufa. Naye hakuonekana tena, kwa kuwa Mungu alikuwa amemchukua. Naye alipokuwa hajachukuliwa bado, alikuwa ameshuhudiwa, ya kuwa alimpendeza Mungu.[#1 Mose 5:24.]

6Lakini pasipo kumtegemea haiwezekani kumpendeza Mungu. sharti. Kwani atakayemjia Mungu, amtegemee kwamba: Yupo, nao watakaomtafuta huwalipa.

7Kwa kumtegemea Mungu Noa alionyeshwa mambo yaliyokuwa hayajaonekana bado, naye kwa hivyo, alivyomcha Mungu, akakitengeneza chombo, awaokoe waliokuwamo nyumbani mwake. Ndivyo, alivyouumba ulimwengu, lakini yeye akaurithi wongofu unaopatikana kwa kumtegemea Mungu.[#1 Mose 6:8-9,13-22; Rom. 3:22,24; 4:20.]

Jinsi Aburahamu na Sara walivyomtegemea Mungu.

8Kwa kumtegemea Mungu Aburahamu alitii alipoitwa, ahame, aende mahali, atakapopewa kuwa urithi wake. Akahama, asijue, aendako.[#1 Mose 12:1,4.]

9Kwa kumtegemea Mungu akawa mgeni katika nchi, aliyoagiwa, kama siyo yake, akakaa katika mahema pamoja na Isaka na Yakobo waliokuwa wenziwe wenye urithi wa kiagio kilekile.[#1 Mose 26:3; 35:12.]

10Kwani alikuwa akiutazamia mji wenye misingi iliyotengenezwa na kujengwa na Mungu.

11Kwa kumtegemea Mungu naye Sara alipewa nguvu ya kupata mimba hapo, alipokwisha kuwa mzee; kwani alimwazia yule aliyemwagia hivyo kuwa mwelekevu.[#1 Mose 21:2.]

12Kwa hiyo wale waliozaliwa na yeye mume mmoja aliyekuwa mwenye mwili uliokwisha kufa walikuwa wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa ufukoni penye bahari usiohesabika.[#1 Mose 22:17; Rom. 4:19.]

13Hao wote walikufa na kumtegemea Mungu: kwa kuwa hawakuyapata, waliyoagiwa, ila waliyaona, yako mbali bado, wakaenda kuyakutia kule, wakaungama: Nchini tu wageni wanaopita tu.[#1 Mose 23:4; 47:9.]

14Kwani wenye kusema hivyo wanaonekana kuwa wenye kutafuta nchi ya kutua.

15Nao kama wangaliikumbuka nchi ile, waliyotoka, wangaliweza kurudi.

16Lakini sasa wanaitaka nchi iliyo nzuri kuliko ile, nayo iko mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni soni ya kuitwa Mungu wao, kwani aliwatengenezea mji.[#2 Mose 3:6.]

Jinsi wakale tangu Aburahamu walivyomtegemea Mungu.

17Kwa kumtegemea Mungu Aburahamu alipojaribiwa alimtoa Isaka, awe ng'ombe ya tambiko, yeye aliyekuwa mwana wake wa pekee.[#1 Mose 22.]

18Naye alikuwa amevipokea viagio, alivyowekewa kwamba: Wa Isaka ndio watakaoitwa uzao wako.[#1 Mose 21:12.]

19Alidhani, ya kuwa Mungu anaweza kuamsha mtu hata kwenye wafu. Kwa hiyo alimpata tena papo hapo, alipokwisha kumtoa.[#Rom. 4:17.]

20Kwa kumtegemea Mungu Isaka alimbariki Yakobo na Esau kwa ajili ya mambo, watakayoyaona.[#1 Mose 27:28-29,39,40.]

21Kwa kumtegemea Mungu Yakobo alipokuwa mwenye kufa aliwaombea mema kila mmoja wao wana wa Yosefu, akawaombea na kuinama, akiiegemea ncha ya mkongojo wake.[#1 Mose 47:31; 48:15-16.]

22Kwa kumtegemea Mungu Yosefu alipofikisha kufa alikumbuka, ya kuwa wana wa Isiraeli wataitoka ile nchi, akawaagizia mifupa yake.[#1 Mose 50:24.]

23Kwa hiyo, wazazi wake walivyomtegemea Mungu, Mose alipozaliwa alifichwa nao miezi mitatu; kwa sababu walimwona mtoto kuwa mzuri, hawakuliogopa agizo la mfalme.[#2 Mose 2:2.]

24Kwa kumtegemea Mungu Mose alipokuwa mtu mzima alikataa kuitwa mwana wa binti Farao,[#2 Mose 2:11-12.]

25akapendezwa kufanyiziwa maovu pamoja na watu wa Mungu, akayakataa mazuri yaliyopatikana kwa kukosa, maana huishia upesi.

26Kwani alifikiri hivyo: kubezwa kwa kuwa wake Kristo ni kilimbiko kikuacho kuliko mali zote za Misri, maana aliyatazamia malipo ya mwisho.[#Ebr. 10:34-35; 13:13.]

27Kwa kumtegemea Mungu akatoka Misri, asiyaogope makali ya mfalme, kwani yeye asiyeonekana alishikamana naye, kama anamwona.[#2 Mose 2:15; 12:51.]

28Kwa kumtegemea Mungu akaifanya Pasaka na kupaka damu, mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse.[#2 Mose 12:12-13.]

29Kwa kumtegemea Mungu wakapita katika Bahari Nyekundu, kama ni nchi kavu, lakini Wamisri walipovijaribu wakatoswa.[#2 Mose 14:22,27.]

30Kwa hivyo, Waisiraeli walivyomtegemea Mungu, maboma ya Yeriko yakaanguka yalipozungukwa siku saba.[#Yos. 6:20.]

31Kwa kumtegemea Mungu Rahabu, angawa alikuwa mwanamke mgoni, hakuangamia pamoja na wale wasiotii, maana wale wapelelezi aliwapokea na kuwatuliza mioyo.[#Yos. 2:11,12; 6:17,23; Yak. 2:25.]

Nguvu ya kumtegemea Mungu huoneka katika mateso.

32Nisemeje tena? Kwani saa hazingenitosha, kama ningeyasimulia mambo ya Gideoni na ya Baraka na ya Samusoni na ya Yefuta na ya Dawidi na ya Samweli na ya wafumbuaji.[#Amu. 4:6; 6:11; 12:7; 15:20; 1 Sam. 3.]

33Hao kwa kumtegemea Mungu walipigana na wafalme, wakawashinda, wakaamua kwa wongofu, wakaona, viagio vilivyotimia, wakavifunga vinywa vya simba,[#Amu. 14:6; 1 Sam. 17:34-35; Dan. 6:22.]

34wakazima mioto yenye nguvu, wakapona ukali wa panga. Walipokuwa wanyonge walipewa nguvu tena, wakawa wakali vitani, wakakimbiza vikosi vizima vya wageni.[#Dan. 3:23-25.]

35Kwa kufufuka kwao, ambao walifiwa nao, wanawake waliwapata tena wao hao, waliofiwa nao. Lakini wengine walipoteswa walitaka kuuawa, wakakataa kukombolewa, wapate ufufuko ulio mzuri uliko huo.[#1 Fal. 17:23; 2 Fal. 4:36.]

36Wengine walijaribiwa na kufyozwa pamoja na kupigwa, wengine wakafungwa minyororo, wakatiwa vifungoni.[#Yer. 20; 37; 38.]

37Waliuawa kwa kupigwa mawe, walipondwa, walipasuliwa, walikufa kwa kuchomwa majisu, walifukuzwa po pote, wajiendee wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi tu, wakiwa na njaa, wakiumia kwa maovu, waliyofanyiziwa.[#2 Mambo 24:21.]

38Kweli haikuupasa ulimwengu huu kuwa nao, wakatangatanga maporini na milimani na mapangoni na mashimoni ndani ya nchi.

39Hao wote walipoteseka, ndipo, walipotimiza kumtegemea Mungu, lakini hawakuona, kiagio kilivyotimia.

40Kwani Mungu alikuwa ametupatia kale kitu kilicho kizuri sana, maana wale wasipate kutimilika pasipo sisi.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania