Waebureo 8

Waebureo 8

Agano Jipya.

1Neno lililo kuu katika hayo, tuliyoyasema, ni hili: Tunaye mtambikaji mkuu aliyeketi mbinguni kuumeni kwa kiti cha kifalme chenye ukuu.[#Ebr. 4:14.]

2Naye ni mtunzaji wa Patakatifu na wa Hema lile la kweli, Bwana alilolisimamisha, siye mtu aliyelisimamisha.

3Kwani kila mtambikaji huwekwa kupeleka matoleo na vipaji vya tambiko. Kwa hiyo hata huyu amepaswa kuwa na kitu cha kumpelekea Mungu.[#Ebr. 5:1.]

4Kama angekuwa ulimwenguni, asingekuwa mtambikaji, maana wako wanaompelekea Mungu vipaji, kama walivyoagizwa.

5Nao huvitumikia vile vilivyo mfano na kivuli cha vile vilivyoko mbinguni. Ndivyo, Mose naye alivyoagizwa alipotaka kulitengeneza lile hema, kwamba:

Angalia, uyafanye yote kwa mfano, ulioonyeshwa mlimani!

6Lakini sasa huyu amepata utumikizi ulioupita, kwani agano, alilotuletea, ni zuri kuliko lile, tena limeunganishwa na maagizo na viagio vilivyo vizuri navyo kuliko vile.[#Ebr. 7:22; 12:24; 2 Kor. 3:6.]

7Kwani lile la kwanza kama lingalikuwa pasipo masazo, pasingalitafutwa mahali pa kuwekea la pili.

8Kwani anawakanya na kuwaambia: Bwana anasema:

Mtaona, siku zikija, ndivyo asemavyo Bwana;

ndipo, nitakapowatimilizia wao wa mlango wa Isiraeli

nao wa mlango wa Yuda Agano Jipya!

9Halitakuwa, kama Agano lile lilivyokuwa,

nililolifanya na baba zao siku ile,

nilipowashika mikono, niwatoe katika nchi ya Misri;

kwani wao wenyewe hawakulishika Agano langu,

nami nikawakataa; ndivyo, asemavyo Bwana.

10Kwani Bwana asema:

Agano, nitakalolifanya nao wa mlango wa Isiraeli,

siku hizi zitakapokuwa zimepita,

ni hili, asema Bwana:

Nitawapa Maonyo yangu, yakae katika mawazo yao,

tena nitayaandika mioyoni mwao;

nami nitakuwa Mungu wao,

nao watakuwa watu wangu.

11Hawatafundishana tena mtu na mwenziwe

wala mtu na ndugu yake kwamba: Mtambue Bwana!

Kwani wote watanijua, hivyo walivyo wadogo,

mpaka wakiwa wakubwa.

12Kwani nitawahurumia kwa ajili ya mapotovu yao,

nisiyakumbuke tena makosa yao.

13Agano anapoliita Jipya, lile la kwanza amekwisha kulifanya kukuu. Lakini lililo kukuu na chakavu limefikia kutoweka.[#Rom. 10:4.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania