Waebureo 9

Waebureo 9

Hema la Agano la Kale.

1Nalo Agano la kwanza lilikuwa na maongozi ya kumtambikia Mungu, tena lilikuwa na Patakatifu palipopasa ulimwenguni.

2Kwani palikuwa pamesimamishwa hema la kuingilia; mwake mlikuwamo taa na meza na mikate aliyowekewa Bwana. Ndipo palipoitwa Patakatifu.[#2 Mose 25:23,30,31.]

3Lakini mle ndani mbele ya pazia lililoko katikati mlikuwamo hema lililoitwa Patakatifu Penyewe.[#2 Mose 26:33-34.]

4Humo mlikuwa na kivukizio cha uvumba cha dhahabu tupu na Sanduku la Agano lililofunikizwa po pote na mabati ya dhahabu; ndani yake mlikuwa na kitungi cha dhahabu chenye Mana na fimbo yake Haroni iliyochipuka na vibao vya Agano.[#2 Mose 16:33; 25:16,21; 4 Mose 17:10.]

5Lakini juu ilikuwa imefunikwa na Makerubi yenye utukufu waliokipatia hicho Kiti cha Upozi kivuli. Hayo yote hatuwezi kuyasema sasa moja moja.[#2 Mose 25:18; 26:34; Rom. 3:25.]

6Hivi vilipokwisha kutengenezwa hivyo, watambikaji huingia kila siku katika hema la kwanza wakifanya kazi za tambiko.[#4 Mose 18:3-4.]

7Lakini katika hema la pili humwingia mtambikaji mkuu peke yake kila mwaka mara moja tu, naye hamwingii pasipo damu, anayoipeleka, iwe kole yake yeye na ya makosa ya watu wanaojikosea tu.[#3 Mose 16:2,14-15.]

8Hivyo Roho Mtakatifu hueleza kwamba: Njia ya kupaingilia Patakatifu Penyewe haijafunguka siku, hema la kwanza litakapokuwa likingali limesimama bado.[#Ebr. 10:19.]

9Nalo lilikuwa mfano wa kuonyesha, siku hizi za sasa zilivyo: kwani mle watu humpelekea Mungu matoleo na vipaji vya tambiko visivyoweza kumpa mwenye kuvitoa moyo uliotulia wote.[#Ebr. 10:1-2.]

10Kwani miiko ya kula na ya kunywa nayo maosho mengi ni maongozi ya miili tu, yatufikishe hapo, siku za kuinyosha njia zitakapokutia.[#3 Mose 11:2; 15:18; 4 Mose 19:13; Mar. 7:8.]

Nguvu ya ukombozi, Kristo aliotupatia.

11*Lakini Kristo alikuja kuwa mtambikaji mkuu wa yale mema yatakayotokea, akapita katika hema lililo kubwa na timilifu kulipita lile lililotengenezwa na mikono ya watu, maana halikufanywa na viumbe vilivyopo nchini.[#Ebr. 6:20; 10:1.]

12Naye hakupeleka damu za mbuzi na za ndama, ila damu yake mwenyewe, akapaingia nayo Patakatifu Penyewe ile mara moja, akatupatia ukombozi usio na mwisho.

13Kwani kale damu za mbuzi na za ng'ombe na majivu ya mori aliyechomwa yalinyunyiziwa wenye uchafu, yawatakase, uchafu wa miili uwaondoke;[#3 Mose 16:14-15; 4 Mose 19:9.]

14lakini sasa kwa hivyo, Kristo alivyojitoa kwa nguvu ya Roho aliye wa kale na kale kumwia Mungu ng'ombe ya tambiko isiyo na kilema, damu yake itazidi kuing'aza sana mioyo yetu yote, tuyaache matendo yenye kutuua, tupate kumtumikia Mungu aliye mwenye uzima.[#1 Petr. 1:18-19; 1 Yoh. 1:7; Ufu. 1:5.]

15Kwa sababu hii alikuwa mpatanishi aliyetuletea Agano Jipya kwamba: Walioitwa na waupate urithi wao ulio wa kale na kale, kama walivyoagiwa, kwani kufa kumeoneka kunakokomboa katika makosa yaliyofanyika siku za Agano la kwanza.*[#Ebr. 12:24; 1 Tim. 2:5.]

16Kwani hapo palipo na agano, sharti kwanza mwenye kuliweka afe.

17Kwani agano hutimizwa na kufa, lakini halina maana kabisa, mwenye kuliweka angali yu hai.

18Kwa hiyo hata lile la kwanza halikueuliwa pasipo damu.

19Kwani Mose alipokwisha kuwaambia watu wote kila agizo la maonyo, akachukua damu za ndama na za mbuzi, kisha akachukua na maji na pamba nyekundu na kivumbasi, akakinyunyizia Kitabu chenyewe, kisha nao watu wote,

20akisema: Hizi ni damu za Agano, Mungu alilowaagizia.[#2 Mose 24:6-8.]

21Hata hema na vyombo vyote vya kutambikia akavinyunyizia damu vilevile.[#3 Mose 8:15,19.]

22Nayo Maonyo yaliagiza, vyombo vyote vitakaswe na damudamu, maana pasipo kumwagika damu hakuna ondoleo.[#3 Mose 17:11; Ef. 1:7.]

Amejitoa mara moja tu.

23Basi, mifano ya vile vilivyoko mbinguni ilipasa kutakaswa hivyo. Lakini vile vya mbinguni vyenyewe vilipaswa na vipaji vya tambiko vilivyo vyenye nguvu kuliko vile.[#Ebr. 8:5.]

24Kwani Kristo hakupaingia Patakatifu palipofanywa na mikono, palipo mfano wa Patakatifu pa kweli, ila aliingia mbinguni kwenyewe, atokee sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu sisi.[#Ebr. 9:11-12; 1 Yoh. 2:1.]

25Lakini hakuingia, ajitoe mara nyingi, kama mtambikaji mkuu anavyopaingia Patakatifu kila mwaka na kupeleka damu isiyo yake.

26Yeye angalipaswa na kuteswa mara nyingi, kuanzia hapo, ulimwengu ulipoumbwa. Lakini sasa ameonekana mara moja tu, siku zilipotimia, azitangue nguvu za ukosaji na kujitoa kuwa kipaji cha tambiko.[#Ebr. 9:12; 1 Kor. 10:11; Gal. 4:4.]

27Kama inavyowapasa watu, wafe mara moja, kisha wahukumiwe,[#1 Mose 3:19.]

28vivyo naye Kristo ametolewa mara moja, awe kipaji cha tambiko cha kuyaondoa makosa ya watu wengi. Lakini mara ya pili atawatokea pasipo kosa wale wanaomngojea, awaokoe.[#Ebr. 10:10,12,14.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania