Hosea 5

Hosea 5

Waisiraeli na Wayuda wanatishwa.

1Yasikieni haya, ninyi watambikaji!

Yasikilizeni, nanyi mlio mlango wa Isiraeli!

Nanyi wa mlango wa mfalme, yategeni masikio!

Kwani liko shauri linalowataka,

kwa maana mmekuwa tanzi la kuwanasa Wamisipa

na wavu uliotegwa Tabori juu.

2Wakachimba mwina mrefu Setimu, lakini mimi nitawachapa wote.

3Mimi ninamjua Efuraimu, naye Isiraeli hafichiki, nisimwone,

kwani hata sasa, wewe Efuraimu, unaufuata ugoni,

naye Isiraeli amejipatia uchafu.

4Matendo yao yanawazuia kurudi kwa Mungu wao,

kwani roho ya ugoni imo mioyoni mwao, lakini Bwana

hawamjui.

5Majivuno ya Isiraeli huwaumbua usoni pake;

Isiraeli na Efuraimu watajikwaa kwa ajili ya manza,

walizozikora,

naye Yuda atajikwaa pamoja nao.

6Huchukua kondoo na ng'ombe kwenda kumtafuta Bwana,

lakini hawamwoni, amekwisha kutengana nao.

7Bwana wamemwacha kwa udanganyifu, wakazaa wana wasio wake.

Sasa mwezi utakaoandama utawala pamoja na fungu lao.

8Pigeni mabaragumu huko Gibea! Pigeni matarumbeta huko Rama!

Pigeni yowe Beti-Aweni: Ni nyuma yako, Benyamini!

9Siku, Efuraimu atakapochapwa,

atageuzwa kuwa mapori yaliyo peke yao;

niliyoyajulisha mashina ya Isiraeli yatatimia kweli.

10Wakuu wa Yuda wanafanana nao wanaosogeza mawe ya mipakani;

wao hao nitawamwagia machafuko yangu kama maji.

11Efuraimu anakorofishwa, amepondwa na hukumu,

kwani alikuwa amependezwa kufuata maagizo ya watu.

12Mimi kwake Efuraimu ni kama mende,

nako kwao walio mlango wa Yuda kama ugonjwa wa ubovu.

13Efuraimu alipouona ugonjwa wake,

Yuda naye alipouona usaha wa madonda yake,

ndipo, Efuraimu alipokwenda Asuri,

naye akatuma kwa mfalme Yarevu (Mgombeaji),

lakini hataweza kuwaponya, wala hataukausha usaha wenu.

14Kwani mimi kwake Efuraimu ni kama simba,

nako kwao walio mlango wa Yuda kama mwana wa simba,

mimi, kweli mimi mwenyewe nitanyafua, kisha nitakwenda

zangu;

nitakapochukua, hapatakuwapo atakayeopoa.

15Nitakwenda kurudi mahali pangu,

mpaka watakapojutia, wautafute uso wangu;

kwa kusongeka kwao watanichungulia usiku kucha.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania