The chat will start when you send the first message.
1Haya ndiyo maono ya Yesaya, mwana wa Amosi, aliyoyaona kwa ajili ya Yuda na kwa ajili ya Yerusalemu siku za Uzia na za Yotamu na za Ahazi na za Hizikia, waliokuwa wafalme wa Yuda.
2Sikilizeni, ninyi mbingu! Angalieni, ninyi nchi!
Kwani Bwana anasema:
Nilikuza wana, nikawapa utukufu; lakini wao wamenitengua.
3Ng'ombe humjua bwana wake.
naye punda hupajua,
mabwana wake wanapomwekea chakula;
lakini Isiraeli hanijui,
walio ukoo wangu hawanitambui.
4Utaona, wewe kabila lenye makosa,
nanyi mnaolemewa na manza, mlizozikora,
wewe kizazi cha wabaya, nanyi wana wapotovu!
Wamemwacha Bwana na kumbeza Mtakatifu wa Isiraeli,
wakarudi nyuma.
5Mnapigiwa nini, kwa kuwa mnafuliza bado kurudi nyuma?
Kila kichwa kiko na vidonda, kila moyo umeugua.
6Toka wayo wa mguu mpaka kichwani hapana palipo pazima,
ni madonda na machubuko na mapigo matupu;
hayaoshwi, wala hayakufungwa,
wala hayakulegezwa na mafuta.
7Nchi yenu ni mapori tu, miji yenu imeteketezwa na moto,
mashamba yenu yanaliwa na wageni machoni penu;
kweli ni mapori tu,
kama nchi zilivyo zikiharibiwa na wageni.
8Paliposalia ni penye binti Sioni,
ni kama kilindo mizabibuni,
ni kama dungu shambani kwa miboga,
kweli ni kama mji uliozungukwa na adui.
9Bwana Mwenye vikosi kama asingalitusazia hao wachache waliookoka,
tungalikuwa kama Sodomu, tungalifanana na Gomora.
10Lisikilizeni neno lake Bwana, ninyi waamuzi wa Sodomu!
Yaangalieni maonyo yake Mungu wetu, ninyi watu wa Gomora!
Bwana anasema: Ni vya nini
11vipaji vyenu vingi, mnavyonitolea vya tambiko?
Nimeshiba kondoo, mlionichomea,
hata mafuta ya ndama wanonao,
damu zao ng'ombe na wana kondoo na mbuzi hazinipendezi.
12Mnapokuja kuoneka machoni pangu,
ni nani aliyevitaka hivyo mikononi mwenu,
mkija kuzikanyaga nyua zangu?
13Acheni kuleta tena vilaji vya tambiko visivyofaa!
Uvumba nao hunitapisha, hata sikukuu za miandamo ya mwezi
nazo za mapumziko na za makusanyiko;
sivumilii, upotovu ukiwa hapohapo, mnaponikusanyikia.
14Roho yangu huzichukia sikukuu zenu za miandamo ya mwezi
nazo sikukuu zenu nyingine,
zimeniwia mzigo mzito, nimechoka kuuchukua tena.
15Mkininyoshea mikono yenu, nitayafumba macho yangu, yasiione,
hata mkikaza kuniomba, sisikii;
maana mikono yenu imejaa damu.
16Iosheni na kuitakasa!
Uondoeni ubaya wa matendo yenu, macho yangu yasiuone tena!
Msiendelee na kufanya mabaya!
17Jifundisheni kufanya mema!
Tafuteni njia ya kunyosha maamuzi mkiwapingia wakorofi!
Waamulieni wafiwao na wazazi! Wagombeeni wajane!
18Njoni, tuumbuane! Ndivyo, asemavyo Bwana.
Makosa yenu ijapo yawe mekundu kama damu,
yatakuwa meupe kama chokaa juani;
ijapo yawe mekundu kama nguo za kifalme,
yatakuwa kama pamba.
19Ikiwapendeza, mnisikie, basi, mtakula mema ya nchi.[#3 Mose 25:18-19.]
20lakini mkikataa, mkaacha kutii, mtaliwa na panga.
Kwani kinywa chake Bwana kimesema.
21Kumbe mji uliokuwa wenye welekevu umegeuka kuwa wenye ugoni!
Ulikuwa umejaa maamuzi yanyokayo, wongofu ukapata kao kwako,
lakini sasa ni kao la wauaji.
22Fedha yako imegeuka kuwa mavi ya chuma tu,
mvinyo yako imechanganywa na maji.
23Wakuu wako hufanya fujo, wenzao ni wezi,
wao wote hupenda matunzo, hufuata fedha za kupenyezewa,
wafiwao na wazazi hawawaamulii,
wala mashauri ya wajane hayafiki kwao.
24Kwa sababu hiyo ndivyo, asemavyo Bwana,
yeye Bwana Mwenye vikosi amtawalaye Isiraeli:
Patafika, nitakapojituliza kwao wapingani wangu,
nikiwalipiza adui zangu!
25Ndipo, mkono wangu utakapokurudia tena,
hapo nitayayeyusha mavi yako ya chuma kwa dawa kali,
niyaondoe yasiyokupasa yote yaliyomo.
26Kisha nitakupa tena waamuzi kama huko kale,
nao wakata mashauri watakuwa kama wao wa mwanzoni.
Kwa hiyo utaitwa Ngome ya Wongofu au Mji wenye Welekevu.
27Sioni utakombolewa kwa maamuzi ya kweli,
nao watu wake walioigeuza mioyo
watakombolewa kwa wongofu.
28Lakini wapotovu na wakosaji watavunjwa wote pamoja,
nao waliomwacha Bwana watatoweka.
29Kwani watatwezwa kwa ajili ya mitamba, mliyoitunukia,
nazo nyuso zenu zitaiva kwa kuona soni
kwa ajili ya mashamba, mliyoyachagua.
30Kwani mtakuwa kama mtamba uliokauka pamoja na majani yake,
au mtafanana na shamba lisilo na maji.
31Mwenye nguvu atageuka kuwa kama madifu makavu,
nazo kazi zake zitakuwa kama cheche la moto;
kisha yatateketea yote pamoja,
asipatikane awezaye kuuzima moto huo.