Yesaya 32

Yesaya 32

Siku za nyuma zitakuwa zenye wongofu na utengemano.

1Na mwone, mfalme akitawala kwa wongofu,

wakuu nao wakiwaendea watu kwa unyofu!

2Kila mmoja wao atakuwa kimbilio penye kimbunga

na ficho penye mvua nyingi,

watakuwa kama vijito vya maji katika nchi kavu,

na kama kivuli cha mwamba mkuu

katika nchi inayotwetesha.

3Hapo macho yao waonao hayatazibana tena,

nayo masikio yao wasikiao yatasikiliza.

4Nayo mioyo yao walio wa juujuu itatambua na kujua maana,

nazo ndimi zao wagugumizao maneno

zitasema upesi maneno ya sawasawa.

5Mjinga hataitwa tena bwana mkubwa,

wala mdanganyifu hataambiwa tena kuwa mkuu.

6Kwani mjinga husema yenye ujinga,

nao moyo wake hufanya maovu:

hufanya yaliyo machafu machoni pake Bwana,

tena husema maneno ya kupoteza watu, wasimjie Bwana,

mwenye njaa humwacha, akae vivyo hivyo na njaa yake,

naye mwenye kiu humnyima cha kunywa.

7Naye mdanganyifu mizungu yake ni mibaya:

huwaza njia za kupotoa,

apate kuangamiza wanyonge kwa maneno ya uwongo,

ijapo mkiwa aseme yanyokayo shaurini.

8Lakini aliye bwana mkubwa huwaza yapatanayo na ubwana,

naye atayasimamia ya ubwana.

9Ninyi wanawake msiojisumbua, inukeni,

mwisikilize sauti yangu!

Nanyi wanawali mnaojikalia tu,

yasikilizeni maneno yangu!

10Siku za nyuma, mwaka utakapopita,

mtatetemeka nyinyi mnaojikalia tu,

kwani mavuno ya zabibu yatakuwa yametoweka,

nayo mavuno ya matunda hayatakuwa tena.

11Stukeni, ninyi msiojisumbua!

Tetemekeni, ninyi mnaojikalia tu!

Jivueni na kuondoa mavazi, mpate kujifunga viunoni tu.

12Jipigeni vifua kwa ajili ya mashamba

yaliyokuwa yakipendeza,

na kwa ajili ya mizabibu iliyokuwa ikizaa sana!

13hata kwa ajili ya nchi yao walio ukoo wangu,

kwani miti yenye miiba kama mikunju itakuwamo;

hata kwa ajili ya nyumba zote za furaha

na kwa ajili ya huo mji uliojaa vigelegele.

14Kwani majumba yatakuwa mahame,

makelele ya mjini yatakuwa yameachwa,

boma lake na minara yake itakuwa imegeuka

kuwa mapango kale na kale ya kufurahisha vihongwe

na malisho ya makundi ya kondoo na mbuzi.

15Itakuwa hivyo, mpaka tutakapomwagiwa Roho itokayo juu.

Ndipo, nyika itakapokuwa shamba la mizabibu,

nalo shamba la mizabibu litawaziwa kuwa mwitu;

16ndipo, mashauri ya nyikani yatakapokatwa kwa unyofu,

nao wongofu utakaa mashambani kwa mizabibu.

17Nayo kazi ya wongofu itakuwa kuleta utengemano,

nao utumishi wa wongofu utakuwa kuwapatia watu utulivu,

wakae salama kale na kale.

18Ndipo, wao walio ukoo wangu watakapokaa mahali penye utengemano

na katika makao ya kukaa salama

na katika vituo visivyowasumbua.

19Lakini kwanza mvua ya mawe inye ya kuvunja mwitu,

tena ya kuunyenyekeza mji unyenyekee kabisa.

20Ninyi mtakuwa wenye shangwe,

kwa kuwa mtapanda kandokando ya maji po pote,

mtawaacha ng'ombe na punda, wajiendee, wanapotaka.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania