The chat will start when you send the first message.
1Mwenye kuapizwa ni wewe mkorofi usiyekorofishwa bado,
mwenye kuapizwa ni wewe mpokonyi usiyepokonywa bado.
Utakapomaliza kukorofisha utakorofishwa,
utakapomaliza kupokonya utapokonywa!
2Bwana, tuwie mpole! Wewe tumekungojea;
uwe mkono wao kila kunapokucha!
Uwe nao wokovu wetu, tunaposongeka!
3Waliposikia sauti ya uvumi, makabila ya watu yalikimbia,
wewe ukiinuka, wamizimu hutawanyika.
4Ndipo, mateka yenu yatakapookotwa,
kama watu wanavyookota nzige;
kama funutu wanavyojikimbilia,
ndivyo, watakavyojikimbilia.
5Bwana ametukuka, kwani anakaa juu,
hujaza Sioni maamuzi yaongokayo.
6Ndipo, siku zako zitakapokuwa zimeelekea pamoja,
yenye werevu wa kweli na utambuzi yatakuwa malimbiko ya kujisaidia,
kumwogopa Bwana ndiko kutakakokuwa mali zake Sioni.
7Wasikilizeni wanguvu wao wanaopiga makelele huko nje,
wajumbe wa kuomba utengemano wanalia kwa uchungu.
8Barabara ziko peke yao, hakuna apitaye njiani.
Amevunja agano kwa kuibeza miji
na kwa kuwawazia watu kuwa si kitu.
Nchi inazimia kwa kusikitika:
9Libanoni kumekauka kwa kuona soni,
Saroni kumegeuka kuwa kama nyika,
Basani na Karmeli kumepakatika majani.
10Ndivyo, anavyosema Bwana: Sasa nitainuka,
sasa nitajitukuza, sasa nitaoneka.
11Kwa kuwa mimba zenu ni za majani makavu,
mtazaa mabua makavu tu;
kufoka kwenu ni moto utakaowala wenyewe.
12Ndipo, makabila ya watu yatakapochomwa kama chokaa,
watakuwa kama miiba iliyokatwa ya kuteketezwa na moto.
13Sikieni, ninyi mkaao mbali, mliyoyafanya!
nanyi mkaao karibu, zijueni nguvu zangu!
14Wakosaji walioko Sioni wamestuka,
tetemeko likawashika wapotovu,
wakasema: Kwetu sisi yuko nani
awezaye kukaa penye moto ulao?
Kwetu sisi yuko nani awezaye kukaa penye majiko
yasiyozima kale na kale?
15Ni yeye aendeleaye kwa wongofu naye asemaye yanyokayo,
naye akataaye mapato ya ukorofi
naye akung'utaye mikono yake, isishike mapenyezo,
naye ayazibaye masikio yake,
asisikie mashauri ya damu zilizomwagwa,
naye ayafumbaye macho yake, asiyaone mabaya.
16Ndiye atakayekaa juu:
maboma yaliyoko magengeni yatakuwa ngome yake,
mkate atapewa tu, nayo maji yake hayatakauka.
17Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake,
yataiona nayo nchi, jinsi itakavyopanuka.
18Moyo wako utakapoyawaza yale mastusho utasema:
Yuko wapi mwenye kuhesabu fedha?
Yuko wapi mwenye kuzipima?
Yuko wapi mwenye kuihesabu minara?
19Lile kabila lenye ukorofi hulioni tena,
ndimi zao zikagugumiza tu maneno yasiyokuwa na maana.
20Utazameni Sioni ule mji wetu wa kukusanyikiamo!
Macho yako yataona,
ya kuwa Yerusalemu ni kao lisilosumbua,
ni hema lisilosafiri,
mambo zake hazing'olewi kale na kale,
kamba zake zote hazikatiki kamwe.
21Kwani huko Bwana mwenye utukufu atakuwa kwetu,
atukingie penye mito mikubwa yenye mikono mipana,
mitumbwi ya kuvukia haitapatikana,
wala vyombo havitapita hapo.
22Kwani Bwana ni mwamuzi wetu,
Bwana ndiye atakayetuongoza,
Bwana ni mfalme wetu, yeye ndiye atakayetuokoa.
23Kamba zako zilikuwa zimelegea,
hazikuukaza ulingo wa mlingoti wao,
wala hazikutanda tanga;
ndipo, mateka mengi mazuri yatakapogawanywa,
nao waendao pecha wataweza kujitwalia mateka.
24Hapataonekana mwenyeji
atakayesema: Nimeugua,
kwani watu watakaokaa mle
watakuwa wameondolewa manza, walizozikora.