The chat will start when you send the first message.
1*Watulizeni mioyo! Watulizeni mioyo walio ukoo wangu!
Ndivyo, Mungu wenu anavyosema.
2Wayerusalemu wapeni mioyo na kuwatangazia,
ya kuwa utumishi wao wa vita umemalizika,
ya kuwa manza zao, walizozikora, zimekwisha kulipwa,
kwani mkono wa Bwana umewalipisha mara mbili
makosa yao yote.
3Iko sauti ya mtu apigaye mbiu nyikani:
Itengenezeni njia ya Bwana!
Yanyosheni nyikani mapito ya Mungu wetu!
4Vibonde vyote vifukiwe,
navyo vilima vyote na vichuguu vyote vichimbuliwe!
Napo palipopotoka panyoshwe,
napo penye mashimo pawe njia ya sawasawa!
5Utukufu wake Bwana upate kufunuliwa,
wote wenye miili wauone pamoja!
Kwani kinywa chake Bwana kimevisema.
6Iko sauti ya mtu asemaye: Tangaza!
Mwingine akasema: Na nitangaze nini?
Kila mwenye mwili ni kama majani,
nao uzuri wake wote ni kama ua la shambaani.
7Majani hunyauka, nayo maua hupukutika,
upepo wa Bwana ukiyapuzia; kweli watu ndio majani.
8Majani hunyauka, nayo maua hupukutika,
lakini Neno lake Mungu wetu litasimama kale na kale.*
9Jipandie mlima mrefu, Sioni, upige mbiu njema!
Paza sauti na nguvu, Yerusalemu, upige mbiu njema!
Paza sauti, usiogope! Iambie miji ya Yuda:
Mtazameni Mungu wenu!
10Tazameni! Bwana Mungu anakuja mwenye nguvu!
Mkono wake unamtengenezea ufalme.
Tazama! Mshahara wake wa kulipa anao.
nayo mapato yake yako mbele yake.
11Kama mchungaji anavyolichunga kundi lake,
atawakusanya wana kondoo kwa mkono wake, awabebe kifuani,
nao wanyonyeshao atawapeleka polepole.
12Yuko nani apimaye bahari kwa kofi lake?
Yuko nani azilinganyaye mbingu kwa upana wa shibiri?
Yuko nani aenezaye mavumbi ya nchi katika kibaba?
Yuko nani apimaye milima kwa mizani
au vilima kwa kipimo gani kingine?
13Yuko nani aielekezaye roho yake Bwana?
Yuko nani aliyekula njama naye ya kumjulisha jambo?
14Yuko nani aliyepiga shauri naye la kumtambulisha kitu?
Yuko nani aliyemfundisha mapito yaendayo sawasawa?
Yuko nani aliyemfundisha kupambanua njia
na kumjulisha utambuzi?
15Tazameni: mataifa mazima huwaziwa kuwa
kama tone la maji katika ndoo, au kama kivumbi katika mizani!
Tazameni: visiwa ni kama kichanga alichokiokota!
16Misitu ya Libanoni haitoshi kuwa kuni,
nao nyama wake hawatoshi kuwa ng'ombe za tambiko.
17Mataifa yote yako mbele yake, kama si kitu,
huwaziwa kuwa kama hayako kabisa na kuwa hayana maana.
18Mungu mtamfananisha na nani?
Mtatengeneza mfano gani wa kuwa, kama yeye alivyo?
19Labda kinyago? Tena ni fundi aliyekiumba,
kisha mfua dhahabu anakifunika chote kwa dhahabu,
akakitia vinyororo vya fedha.
20Akosaye mali za kununua kipaji kama hicho
huchagua mti usiooza,
kisha hutafuta fundi aijuaye kazi hiyo,
amsimamishie kinyago kisichoyumbayumba.
21Nanyi hamvijui? Hamvisikii? Hamkuambiwa tangu mwanzo?
Hamkuitambua misingi ya nchi?
22Anakaa juu ya mviringo wa nchi,
waikaliao wakawa kama funutu machoni pake;
anazitanda mbingu kama nguo nyembamba,
anaziwamba kuwa kama mahema ya kukaa.
Wakuu anawatangua, wawe kama si kitu;
23Waamuzi wa nchi nao anawatendea, kama hawana maana.
24Wanapokuwa hawajapandwa, wala mbegu zao hazijamwagwa.
wanapokuwa mashina yao hayajatia mizizi:
mara anawapuzia, wakanyauka,
kisha upepo mkali ukawachukua kama makapi.
25Kwa hiyo mtanifananisha na nani, niwe, kama yeye alivyo?
Ndivyo, Mtakatifu anavyosema.
26*Yaelekezeni macho yenu juu, mtazame!
Ni nani aliyeviumba hivi?
Ni yeye anayevitokeza vikosi vyao hivyo, alivyovihesabu,
navyo vyote pia anaviita majina.
Kwa kuwa uwezo wake unazidi, nazo nguvu zake zinakaza,
hakuna hata kimoja kinachokoseka.
27Mbona unasema, Yakobo, unanena, Isiraeli:
Njia yangu imefichika, Bwana asiione,
nayo maamuzi, ninayoyangojea, yamempita Mungu wangu?
28Hujayajua bado, hujayasikia bado?
Mungu wa kale na kale ni Bwana aliyeyaumba mapeo ya nchi;
hachoki, wala halegei, utambuzi wake hauchunguziki.
29Achokaye humpa nguvu, asiyeweza humwongezea uwezo;
30ijapo vijana wachoke na kulegea, ijapo wavulana nao wajikwae,
31lakini wamngojeao Bwana hupata nguvu mpya,
waruke, kama watatumia mabawa ya kozi,
hupiga mbio pasipo kulegea,
hukaza mwendo pasipo kuchoka.*