The chat will start when you send the first message.
1*Sasa sikia mtumishi wangu Yakobo!
Nawe Isiraeli, niliyemchagua!
2Hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliyekuumba,
aliyekutengeneza tumboni mwa mama, anayekusaidia:
Usiogope, mtumishi wangu Yakobo,
nawe Isiraeli uongokaye, niliyemchagua!
3Kwani nitamwaga maji panapo kiu, nitokeze mito pakavu,
nitaimwaga Roho yangu kwao walio uzao wako,
nayo mbaraka yangu kwao walio miche yako.
4Watakuwa kama majani kwenye maji
au kama mifuu kwenye mito yenye maji.
5Huyu atasema: Mimi ni wake Bwana,
naye mwenziwe atajiita kwa jina la Yakobo,
naye mwingine ataandika mikononi mwake: Wa Bwana,
mwingine atajivunia jina la Isiraeli,
6Hivi ndivyo, anavyosema Bwana, mfalme wa Isiraeli,
aliye mkombozi wake, yeye Bwana Mwenye vikosi:
Mimi ni wa mwanzo na wa mwisho,
pasipo mimi hakuna Mungu.*
7Yuko nani anayefanana na mimi?
Na apaze sauti, ayatangaze!
Tena anieleze, kama ni kwa sababu gani,
nikiweka ukoo wa watu kuwa wa kale na kale.
Hata yajayo nayo yatakayokuja na wayatangazie watu!
8Msistuke, wala msitetemeke!
Kumbe sikukuambia hayo toka kale na kuyatangaza?
Ninyi m mashahidi wangu: Yuko Mungu pasipo mimi?
Hakuna mwamba mwingine, nisioujua.
9Watengenezao vinyago wote si kitu, navyo viumbe vyao vya kupendeza havifai, wanaovishuhudia wenyewe hawaoni, wala hawatambui kazi, ambazo vilizifanya, kusudi wapatwe na soni.
10Ni nani aliyetengeneza mungu na kuyeyusha kinyago kisichofaa kitu?[#Yes. 45:16; Yer. 10:3-16; Sh. 115:4-8.]
11Tazameni! Wote walio upande wao hupatwa na soni, nao mafundi na watu tu. Na wakusanyike wote pamoja na kusimama hapa, wote pamoja watastuka na kupatwa na soni.[#Yes. 42:17.]
12Mhunzi huvishika vyombo vyake, hutumia moto wa makaa akivitengeneza vinyago kwa vyundo; hivyo anavimaliza kwa mkono wake wenye nguvu; lakini asipokula, nguvu hupotea, napo asipokunywa hulegea.[#Yes. 40:18-20.]
13Fundi wa kuchonga miti huipima kwa kamba na kuiandika kwa kalamu; kisha hutumia visu na kupimapima tena penye kuviringana. Hivyo anatengeneza kinyago, kifanane na mtu mwenye utukufu wa kimtu, kikae nyumbani.
14Huagiza watu, wamkatie miangati, huchukua hata mipingo na mivule, hujichagulia miti ya mwituni iliyo migumu, hupanda nayo mise, mvua iikuze.
15Watu huitumia ya kuchoma moto, huchukua vibanzi vyao vya kuotea, vingine huvitumia jikoni vya kuchomea mikate, tena kipande hukitengeneza kuwa mungu wa kuuangukia; alipokwisha kufanya kinyago, hukitambikia.
16Hivyo hutumia kipande cha mti cha kuchoma moto, apate kuota, kipande cha kupikia nyama, ale nazo zilizochomwa, ashibe, apate hata jasho, aseme: A, nimepata jasho, nimeona moto!
17Kipande kinachosalia hukitengeneza kinyago kuwa mungu, hukitambikia na kukiangukia na kukilalamikia kwamba: Niponye! Kwani mungu wangu ndiwe wewe!
18Lakini hawa hawavijui wala hawavitambui, kwani macho yao yamegandamana, yasione, mioyo yao isielewe maana.
19Hakuna ayawazaye moyoni, wala hakuna ayajuaye na kuyatambua kwamba: Kipande chake nimekichoma moto, kipande nimetumia makaa yake, yachome mkate, kipande nimechoma cha kuchomea nyama, nikala. Tena sao lake nilitengeneze kuwa chukizo, nitambikie kilicho kipande cha mti?
20Ni hivyo: Achungaye majivu moyo wake umedanganyika, ukampoteza, asiiponye roho yake, wala asiseme: Siyo yenye uwongo yaliyomo mkononi mwangu?
21Haya yakumbukeni, Yakobo na Isiraeli!
Kwani wewe ndiwe mtumishi wangu;
nimekutengeneza wewe kuwa mtumishi wangu,
wewe Isiraeli hutasahauliwa kwangu.
22Nimeyatowesha mapotovu yako kama wingu,
nayo makosa yako kama kungugu.
Rudi kwangu! Kwani nimekukomboa.
23Shangilieni, mbingu, ya kuwa Bwana ameyatimiza!
Pigeni kelele, vilindi vya kuzimuni!
Pigeni shangwe na kupaza sauti,
milima na misitu na miti yote iliyomo!
Kwani Bwana amemwokoa Yakobo,
nako kwake Isiraeli anautokeza utukufu wake.
24Hivi ndivyo, anavyosema Bwana, mkombozi wako,
aliyekutengeneza tumboni mwa mama:
Mimi Bwana niliyafanya yote.
Mimi nilipoziwamba mbingu peke yangu,
nikazitanda hata nchi,
yuko nani aliyekuwa kwangu?
25Ndege, wapuzi wanazoziona, nazibezesha,
nao waaguaji nawalevya,
nao walio werevu wa kweli nawarudisha nyuma,
ujuzi wao naugeuza kuwa ujinga.
26Neno la mtumishi wake hulisimamisha,
nayo mashauri ya wajumbe wake huyatimiza.
Ni yeye auambiaye Yerusalemu: Na ukaliwe!
Nayo miji ya Yuda anaiambia: Jengweni!
Nami nitayasimamisha mabomoko yao!
27Kilindi cha maji anakiambia: Kauka!
mimi nitaipwelesha mito yako.
28Yeye ndiye anayemwambia Kiro:
Huyu ndiye mchungaji wangu
atakayeyatimiza mapenzi yangu yote.
Hivyo Yerusalemu utajengwa,
nalo Jumba takatifu litawekewa misingi.