Yesaya 46

Yesaya 46

Vinyago ni vya bure, wokovu uko kwake Mungu tu.

1Beli ameanguka, Nebo naye yuko chini,

vinyago vyao viko migongoni kwa punda na ng'ombe;

vilivyotembezwa nanyi vimefungwa,

ikawa mizigo ya kuchokesha nyama wanaoichukua.

2Wako chini pamoja, kama walivyoanguka pamoja,

hawakuweza kuviokoa vinyago, visichukuliwe,

wao wenyewe wamekwenda kufungwa kwa kuwa mateka.

3Nisikilizeni, ninyi mlio wa mlango wa Yakobo!

Ninyi wote mlio masao ya mlango wa Isiraeli!

Ninyi ndio, niliojitwika tangu hapo,

mlipokuwa tumboni mwa mama zenu,

ninyi ndio, niliojichukuza tangu hapo, mlipozaliwa.

4Hata mtakapokuwa wazee, mimi ndimi niliyekuwa;

hata mtakapotoka mvi, mimi nitawachukua.

Mimi nitayafanya nikijitwika mimi,

mimi nitawachukua na kuwaokoa.

5Yuko nani, ambaye mtanifananisha naye, tuwe sawa?

Yuko nani, ambaye mtanilinganisha naye, tufanane?

6Watu humwaga dhahabu toka mifukoni,

hupima fedha kwa mizani,

humlipa fundi, naye hufanya mungu,

wauangukie na kuutambikia.

7Kisha huuchukua mabegani, huutembeza,

kisha huuweka mahali pake;

hapo unasimama pasipo kuondoka mahali pake.

Wanapoulilia, hauwaitikii;

hakuna, umwokoaye katika shida yake.

8Haya yakumbukeni, mjishupaze!

Yawekeni mioyoni, ninyi wapotovu!

9Yakumbukeni yale ya mwanzo yaliyokuwapo tangu kale!

Kwani mimi ndimi Mungu, hakuna mwingine tena,

kweli, hakuna Mungu aliye kama mimi.

10Tangu mwanzo nayatangaza yatakayokuwa mwisho,

toka kale nayasema yasiyofanyika bado.

Kila nisemapo, shauri langu litatimia,

yote yanipendezayo mimi huyafanya.

11Ninaita kipanga maawioni kwa jua,

katika nchi ya mbali ndiko, ninakotoa mtu

atakayelifanya shauri langu.

Kama nilivyosema, ndivyo, nitakavyoyatimiza;

kama nilivyoyalinganya, ndivyo, nitakavyoyafanya.

12Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu,

ninyi mliojitenga na kuyaacha mbali yaliyoongoka!

13Yale yaongokayo nimeyafikisha karibu,

hayako mbali tena, wokovu wangu haukawilii.

Sioni ndimo, nitakamotokeza wokovu,

kwao Waisiraeli ndiko, nitakakotokeza utukufu wangu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania