The chat will start when you send the first message.
1Na niimbe mambo ya mpendwa wangu!
Ni wimbo wa mpenzi wangu wa kuiimbia mizabibu yake.
Mpendwa wangu alikuwa na shamba la mizabibu
penye kilima kilichoiotesha sana.
2Akalima na kuchimba, hata mawe akayaokota,
akapanda mizabibu mizuri akajenga dungu katikati,
akachimbua nalo kamulio kwake;
kisha alingoja, izae zabibu, lakini ikazaa mbaya zisizolika.
3Sasa ninyi mkaao Yerusalemu nanyi waume wa Yuda,
tuamulieni mimi na mizabibu yangu!
4Yako mambo gani ya kuifanyizia mizabibu, nisiyoifanyizia?
Mbona nilikaa na kuzingojea zabibu,
ikanizalia tu zisizolika?
5Sasa na niwajulishe, mimi nitakayoifanyizia mizabibu yangu:
nitaliondoa boma lao, iwe malisho,
nitakibomoa kitalu chao, ife kwa kukanyagwa.
6Nitaiacha, iwe pori lenyewe,
isipogolewe wala isilimiwe, pakue mikunju na mibigili;
kisha nitayaagiza mawingu, yasiinyeshee mvua.
7Kwani mizabibu ya Bwana Mwenye vikosi
ni mlango wa Isiraeli na watu wa Yuda,
ndio shamba lake lipendwalo naye.
Akangojea manyofu, lakini alipotazama, ni mapotovu;
akangojea wongofu, lakini alipotazama, ni vilio tu.
8Yatawapata wanaokusanya nyumba na nyumba
ndio wanajiongezea mashamba na mashamba,
pasiwepo tena mahali pasipo penu,
mkae peke yenu katika nchi.
9Masikioni mwangu limo neno la Bwana Mwenye vikosi:
Kweli nyumba nyingi zitakuwa mahame,
ijapo ziwe kubwa na nzuri,
asipatikane mtu wa kukaa humo.
10Kwani mashamba kumi ya mizabibu yatatoa kibuyu kimoja tu,
kikapu kizima cha mbegu kitaleta pishi moja tu.
11Yatawapata waamkao mapema wakijitafutia vileo
nao wakaao mpaka usiku kwenye pombe na kuvimbisha vichwa.
12Hapo wanyweapo yako mazeze na mapango,
hata matoazi na mazomari,
lakini kazi za Bwana hawazitazami,
wala matendo ya mikono yake hawayaoni.
13Kwa hiyo wao walio ukoo wangu watatekwa wakiwa hawajui maana,
watukufu wao watakuwa wenye njaa,
nao walio watuwatu tu watazimia kwa kiu.
14Kwa hiyo kuzimu kutakuwa kumejipanua
na kukifumbua kinywa chake pasipo mpaka,
watukufu wa Sioni pamoja na watu wake wapate kushuka
nao waliochezacheza mle na kupiga vigelegele vya furaha.
15Hapo watu watainamishwa, nao waume watanyenyekezwa,
hayo macho yenye majivuno yatanyenyekezwa.
16Lakini Bwana Mwenye vikosi
atatukuka kwa kunyosha maamuzi,
yeye aliye Mungu mtakatifu atajulika
kwa wongofu kuwa Mtakatifu kweli.
17Wana wa kondoo watalisha hapo, kama ni malisho yao,
nako kwenye mahame ya wale wakwasi watakula wageni.
18Yatawapata wajivutiao mabaya
kwa vigwe vya udanganyifu,
tena makosa kwa kamba za magari.
19Ndio wanaosema: Na apige mbio,
afanye upesi matendo yake, tuyaone!
Shauri lake Mtakatifu wa Isiraeli
na litimie na kutokea, tulitambue!
20Yatawapata wanaosema: Kibaya ni chema
nacho chema wanakiita kibaya.
Giza huigeuza kuwa mwanga,
nao mwanga huugeuza kuwa giza.
Machungu huyageuza kuwa matamu,
nayo matamu huyageuza kuwa machungu.
21Yatawapata wanaojiwazia wenyewe
kuwa werevu wa kweli na watambuzi.
22Yatawapata walio wenye nguvu za kunywa pombe,
walio na ufundi wa kuchanganya vileo.
23Kwa kupenyezewa mali huwashindisha wapotovu shaurini,
lakini wongofu wao waongokao huutengua, wasishinde!
24Kwa hiyo watakuwa hivyo: kama ndimi za moto zinavyokula mabua,
au kama majani makavu yanavyojipinda motoni,
ndivyo, mizizi yao itakavyobunguka,
nayo maua yao yatapeperushwa kama mavumbi,
kwani waliyakataa Maonyo yake Bwana Mwenye vikosi,
wakalibeza Neno lake Mtakatifu wa Isiraeli!
25Kwa hiyo Bwana akawachafukia walio ukoo wake,
mkono wake ukawainamia, ukawapiga;
milima ikatetemeka, mizoga yao ikawa kama mataka njiani.
Kwa hayo yote makali yake hayajatulia bado,
mkono wake ungaliko umekunjuka bado.
26Atatweka bendera ya kuwaitia wamizimu wakaao mbali
nao wakaao kwenye mapeo ya nchi atawapigia mbiu,
na mwaone, wakija na kupiga mbio sana.
27Mwao hao hamna mchovu ajikwaaye mara kwa mara,
wala hamna apendaye kusinzia wala kulala usingizi,
wala hamna mwenye mshipi kiunoni ufungukao,
wala hamna mwenye viatu vikatikavyo mikanda.
28Mishale yao itakuwa imenolewa, nyuta zao zitakuwa zimepindwa,
kwato za farasi wao zitaonekana kuwa ngumu kama mawe,
magurudumu ya magari yao yatapiga mbio kama upepo mkali.
29Mazomeo yao ni kama ngurumo ya simba, hulia kama wana wa simba.
Watakuja na kuvuma na kukamata mateka, wayapeleke kwao;
napo hapo hatakuwapo atakayewaponya.
30Makelele, watakayowapigia siku ile,
yatakuwa kama maumuko ya mawimbi ya bahari;
kama mtaichungulia nchi,
itakuwa yenye giza la kuogopesha,
mwanga utakuwa umegeuka giza
kwa weusi wa mawingu yaliyoko juu yake.