The chat will start when you send the first message.
1Nisikilizeni, ninyi mnaofuata yaongokayo,
ninyi mnaomtafuta Bwana!
Utazameni mwamba, ambao mlichongwa mumo humo!
Litazameni shimo la kisima, ambalo mlichimbuliwa mumo humo!
2Mtazameni baba yenu Aburahamu na mzazi wenu Sara!
Nilimwita yeye mmoja tu,
nikambariki, nikampa kuwa wengi.
3Kwani Bwana ameutuliza Sioni,
ameyatuliza mabomoko yake yote,
kwa kuwa atayageuza mapori yake kuwa mashamba,
nazo nyika zake kuwa kama bustani ya Bwana.
Ndipo, kutakapooneka mle kufurahi na kuchangamka,
kushukuru na kuimba kwa sauti kuu.
4Niangalieni, ninyi mlio ukoo wangu,
ninyi mlio watu wangu nisikilizeni!
Kwani maonyo yatatoka kwangu,
nayo yanyokayo machoni pangu
nitayaweka kuwa mwanga wa makabila ya watu.
5Bado kidogo nitakuja kushinda na kuutokeza wokovu wangu;
ndipo, mikono yangu itakapoyapatiliza makabila ya watu.
Mimi ndimi, visiwa vitakayemngojea
na kuuchungulia mkono wangu.
6Yaelekezeni macho yenu mbinguni!
Kisha zitazameni nchi zilizoko chini!
Kwani mbingu zitatoweka kama moshi,
nazo nchi zitachakaa kama nguo,
nao wazikaliao mara watakufa vivyo hivyo.
Lakini wokovu wangu utakuwa wa kale na kale,
nao wongofu wangu hautaangamika.
7Nisikilizeni, ninyi mjuao yaongokayo,
mlio watu wayashikao Maonyo yangu mioyoni mwenu,
msiogope kutwezwa na watu,
wala msiyastukie matusi yao!
8Yako yatakayowala, kama nondo wanavyokula nguo,
au kama mende wanavyokula pamba,
lakini wongofu wangu utakuwa wa kale na kale,
nao wokovu wangu utakalia vizazi na vizazi.
9Amka! Amka, uone nguvu, wewe mkono wa Bwana!
Amka kama siku za kale kwenye vizazi vya zamani!
Si wewe uliomkatakata Rahabu (Mkuu wa maneno wa Misri)
na kumchoma yule joka kubwa?
10Si wewe ulioikausha bahari
yenye vilindi vya maji mengi
na kutoa njia mlemle vilindini mwa bahari,
wapitemo waliokombolewa?
11Waliookolewa na Bwana watarudi,
waje Sioni na kupiga shangwe;
vichwani pao itakuwa furaha ya kale na kale,
machangamko na furaha zitawafikia,
lakini machungu yatakimbia, wasipige kite tena.
12Mimi ndimi ninayewatuliza mioyo yenu.
Wewe ndiwe nani ukiogopa watu wafao
na wana wa watu watowekao kama majani?
13Umemsahau Bwana aliyekufanya,
aliyezitanda mbingu, aliyezishikiza nchi,
ukatetemeka siku zote pasipo kukoma
kwa ajili ya makali yake anayekusonga,
kwa kuwa alitaka kukuangamiza;
na sasa makali yake aliyekusonga yako wapi?
14Aliyepindika kwa kufungwa atafunguliwa upesi,
hatakufa, atupwe shimoni, wala hatakosa chakula chake.
15Kwani mimi na Bwana Mungu wako,
achafuaye bahari, mawimbi yake yaumuke;
Bwana Mwenye vikosi ni Jina langu.
16Nami nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako,
nikakuficha kivulini mwa mkono wangu,
nipate kuzitokeza mbingu mpya na kuishikiza nchi tena,
na kuuambia Sioni: Ukoo wangu ndiwe wewe.
17Amka! Amka! Inuka, Yerusalemu!
Umekunywa mkononi mwa Bwana kikombe chenye makali yake,
hicho kikombe kilichojaa kileo cha kupepesusha
umekinywa na kukimaliza.
18Katika watoto wote, aliowazaa, hakuwako, aliyemwongoza,
wala katika watoto wote, aliowakuza,
hakuwako, aliyemshika mkono.
19Mambo yaliyokupata ni haya mawili,
-lakini yuko nani atakayekupongeza?-
kuvunjwa na kubomolewa,
tena kuuawa kwa njaa na kwa panga,
lakini nitawezaje kukutuliza moyo?
20Wanao wa kiume walikuwa wamezimia,
wakalala pembeni kwenye njia zote za mji,
wakawa kama paa waliokamatwa na wavu,
kwa kuwa walileweshwa na makali yake Bwana,
na makemeo yake Mungu wako.
21Kwa hiyo yasikilize haya,
wewe uliyenyongeka kwa kulewa, lakini sio kwa mvinyo!
22Ndivyo, anavyosema Bwana aliye Bwana na Mungu wako,
awapiganiaye walio ukoo wake:
Tazama! Nimekichukua mkononi mwako
kile kikombe chenye kileo cha kupepesusha,
hicho kikombe kilichojaa makali yangu hutakinywa tena.
23Sasa nitakitia mikononi mwao waliokutesa,
waliokuambia: Lala chini, tupite juu yako!
nawe hukuwa na budi kitumia migongo yako kuwa nchi,
kuwa njia ya kupitia hapohapo.