The chat will start when you send the first message.
1*Ule mwaka, mfalme Uzia alipokufa, nilimwona Bwana, akikalia kiti kirefu cha kifalme kilichowekwa juu, nazo nguo zake zikalijaza Jumba takatifu.[#Yoh. 12:41.]
2Maserafi walikuwa wanasimama juu yake; kila mmoja wao alikuwa mwenye mabawa sita: mawili aliyatumia kuufunika uso wake, mawili kuifunika miguu yake, mawili ya kurukia.
3Wakapaliziana sauti kwamba:
Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu
ni Bwana Mwenye vikosi!
Nchi zote zimejaa utukufu wake!
4Ikatetemeka hata misingi ya vizingiti kwa ukuu wa sauti yake aliyeyatangaza; nayo nyumba ikajaa moshi.[#Ez. 10:4; Ufu. 15:8.]
5Nikasema: Ninakufa, ninaangamia! Kwani ndimi mtu mwenye midomo isiyotakata, tena mimi ninakaa kwa watu wenye midomo isiyotakata, kwani macho yangu yamemwona Mfalme, ndiye Bwana Mwenye vikosi![#2 Mose 33:20.]
6Hapo mmoja wao wale Maserafi akaruka, akanijia; namo mkononi mwake alishika kaa la moto, alilolichukua kwa koleo penye meza ya kutambikia.
7Akagusa nalo kinywa changu, akasema: Tazama! Hili lilipoigusa midomo yako, manza zako, ulizozikora, zimekutoka, nayo makosa yako yamefunikwa.[#Zak. 3:4.]
8Nikasikia sauti ya Bwana, akisema: Nitamtuma nani? Yuko nani atakayetuendea? Nikajibu: Mimi hapa! Nitume!*
9Akasema: Nenda, uwaambie watu wa ukoo huu kwamba:
Kusikia mtasikia, lakini hamtajua maana;
kutazama mtatazama, lakini hamtaona.
10Kwani mioyo yao walio ukoo huu uishupaze,
nayo masikio yao uyazibe,
nayo macho yao uyafumbe,
wasije wakaona kwa macho yao,
au wakasikia kwa masikio yao,
au wakajua maana kwa mioyo yao,
wakanigeukia, nikawaponya!
11Nikasema: Mpaka lini, Bwana? Akasema: Mpaka hapo, miji itakapokuwa mahame, kwa kuwa hamna mwenye kukaa humo, kwa kuwa nyumba hazina watu; mpaka hapo, nchi nayo itakapoangamia kwa kuwa mapori tu;
12mpaka hapo, Bwana atakapowapeleka watu mbali, mahame yawe mengi katika nchi hii.
13Tena kama sao litakuwa fungu la kumi tu, litaangamizwa mara nyingine. Litakuwa kama mkwaju au mtamba: ukikatwa, kunasalia shina lake; hilo shina lake litakuwa mbegu takatifu.[#Yes. 4:3.]