Waamuzi 16

Waamuzi 16

Maanguko na mateso ya Samusoni.

1Samusoni alipokwenda Gaza akaona huko mwanamke mgoni, akaingia kwake.

2Wagaza walipoambiwa, ya kuwa Samusoni ameingia humo, wakaizunguka hiyo nyumba na kumvizia usiku wote penye lango la mji, wakanyamaza kimya usiku kucha kwa kwamba: Tungoje mapambazuko ya asubuhi, tupate kumwua.

3Lakini Samusoni akalala mpaka usiku wa manane tu; hapo usiku wa manane ndipo, alipoondoka, akaishika milango ya lango la mji pamoja na miimo yake miwili, akaing'oa pamoja na komeo, akajitwika mabegani, akaipandisha mlimani kunakoelekea Heburoni.

4Ikawa baadaye, Samusoni akapenda mwanamke aliyekaa penye kijito cha Soreki, jina lake Delila.

5Ndipo, wakuu wa Wafilisti walipopanda kufika kwake, wakamwambia: Umnyenge, upate kuona, nguvu zake kubwa zilimo, tena utazame njia ya kumwona sisi, tupate kumfunga na kumshinda. Kisha tutakupa kila moja fedha elfu moja na mia moja.[#Amu. 14:15.]

6Ndipo, Delila alipomwambia Samusoni: Nijulishe, nguvu zako kubwa zilimo, tena ndivyo ufungwe navyo, watu wakushinde!

7Samusoni akamwambia: Kama wangenifunga kamba saba za mishipa zisizokauka bado, ningekuwa mnyonge kuwa kama kila mtu mwingine.

8Kisha wakuu wa Wafilisti wakampelekea kamba saba za mishipa zisizokauka bado, naye akamfunga nazo,

9watu waliokuwa wanamvizia wakikaa kwake chumbani. Kisha akamwambia: Wafilisti wanakujia, Samusoni; ndipo, alipozirarua hizo kamba, kama uzi wa madifu ukionja moto; lakini nguvu zake hazikujulikana.[#Amu. 15:14.]

10Kisha Delila akamwambia Samusoni: Tazama, umenidanganya, ukaniambia maneno ya uwongo, sasa nijulishe, ndivyo ufungwe navyo!

11Akamwambia: Kama wangenifunga kwa kamba mpya zisizotumika bado kazini, ningekuwa mnyonge kuwa kama kila mtu mwingine.

12Ndipo, Delila alipochukua kamba mpya, akamfunga nazo, akamwambia: Wafilisti wanakujia, Samusoni; lakini watu waliokuwa wanamvizia walikaa chumbani. Naye akazirarua hizo kamba mikononi pake kama uzi.

13Ndipo, Delila alipomwambia Samusoni; Mpaka sasa umenidanganya, ukaniambia maneno ya uwongo, sasa nijulishe, ndivyo ufungwe navyo! Akamwambia: Kama ungefuma shungi saba za kichwani pangu pamoja na nyuzi za mtande za kufuma nguo, basi.

14Alipokwisha kuzipigilia kwa uwambo akamwambia: Wafilisti wanakujia, Samusoni; ndipo, alipoamka katika usingizi, akaung'oa ule uwambo wa kufumia pamoja na nyuzi za mtande.

15Ndipo, alipomwambia: Unasemaje: Ninakupenda, moyo wako ukiwa hauko kwangu? Mara hizi tatu umenidanganya usiponijulisha, nguvu zako kubwa zilimo.

16Ikawa, alipozidi kumsumbua siku zote na hayo maneno yake kwa kumhimiza, mwisho roho yake ikalegea, atake kufa tu;[#Amu. 14:17.]

17ndipo, alipomjulisha yote yaliyokuwamo moyoni mwake, akamwambia: Hakijafika kinyoleo kichwani pangu, kwani mimi nilitengwa kuwa wake Mungu tangu hapo, nilipozaliwa na mama yangu. Kama ningenyolewa, nguvu zangu zingenitoka, niwe mnyonge kuwa kama kila mtu mwingine.[#Amu. 13:5.]

18Delila alipoona, ya kuwa amemjulisha yote yaliyokuwamo moyoni mwake, akatuma kuwaita watu wa Wafilisti kwamba: Pandeni mara hii tu! Kwani amenijulisha yote yaliyokuwamo moyoni mwake. Nao wakuu wa Wafilisti walipopanda kufika kwake walishika zile fedha mikononi mwao.

19Kisha akambembeleza, alale usingizi penye magoti yake; alipokwisha akaita mtu, naye akazinyoa zile chungu saba za kichwani pake; ndivyo, alivyoanza kumshinda, maana nguvu zake zilikuwa zimemtoka.

20Kisha akasema: Wafilisti wanakujia, Samusoni. Alipoamka katika usingizi, alisema moyoni: Nitatoka kama mara nyingine zote kwa kujinyosha tu, kwani hakujua, ya kuwa Bwana ameondoka kwake.[#1 Sam. 16:14.]

21Ndipo, Wafilisti walipomkamata, wakamchoma macho, wakamshusha kumpeleka Gaza, wakamfunga kwa minyororo miwili ya shaba, kisha akawa kifungoni akisaga unga.

22Lakini kwa hivyo, alivyonyolewa, nywele za kichwani pake zikaanza kuota tena.

Kujilipiza kisasi na kufa kwake Samusoni.

23Wakuu wa Wafilisti walipokusanyika kufanya sikukuu ya tambiko kubwa ya mungu wao Dagoni wakamfurahia kwamba: Mungu wetu ametupa adui yetu Samusoni mikononi mwetu![#1 Sam. 5:2.]

24Watu walipomwona wakamsifu mungu wao, kwani walisema: Mungu wetu ametupa adui yetu mikononi mwetu, ndiye aliyeiangamiza nchi yetu kwa kuua watu wengi wa kwetu.

25Mioyo yao ilipochangamka, wakasema: Mwiteni Samusoni, atuchezee! Wakamwita Samusoni na kumtoa kifungoni, awachezee. Walipomsimamisha katikati ya nguzo,

26Samusoni akamwambia kijana aliyemshika mkono: Niachie, nizipapase hizi nguzo zinazoishikiza nyumba hii, niziegemee!

27Nayo hiyo nyumba ilikuwa imejaa watu waume na wake, nao wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo, namo darini walikuwamo kama 3000 waume na wake, waliomtazama Samusoni, jinsi alivyocheza.

28Ndipo, Samusoni alipomlilia Bwana kwamba: Bwana Mungu, nikumbuke, unitie nguvu hii mara moja tu, Mungu wangu, niwalipishe hawa Wafilisti kwa mara moja macho yangu mawili!

29Kisha Samusoni akazikamata hizo nguzo mbili za katikati zilizoishikiza hiyo nyumba, akaziegemea moja kwa mkono wa kuume, moja kwa mkono wa kushoto.

30Kisha Samusoni akasema: Nami mwenyewe na nife pamoja na hawa Wafilisti. Naye alipoinama kwa nguvu, nyumba ikawaangukia wakuu na watu wote pia waliokuwamo. Hivyo wenye kufa, aliowaua kwa kufa akwake, wakawa wengi zaidi kuliko wao, aliowaua alipokuwa yuko mzima bado.

31Kisha ndugu zake nao wote wa mlango wa baba yake wakatelemka, wakamchukua, wakampeleka kwao, wakamzika katikati ya Sora na Estaoli kaburini mwa baba yake Manoa. Naye alikuwa mwamuzi wa Waisiraeli miaka 20.[#Amu. 13:25; 15:20.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania