The chat will start when you send the first message.
1Siku zile hakuwako mfalme kwao Waisiraeli. Kulikuwa na mtu wa Kilawi aliyekaa ugenini milimani kwa Efuraimu huko ndani, akajichukulia mwanamke wa Beti-Lehemu wa Yuda, awe suria.[#Amu. 17:6.]
2Lakini huyu suria akamfanyizia matata, akaondoka kwake kwenda nyumbani mwa baba yake huko Beti-Lehemu wa Yuda, akawa huko miezi minne.
3Ndipo, mumewe alipoondoka, akamfuata, aseme naye maneno ya kuugeuza moyo wake, apate kumrudisha; alikuwa anaye mtumishi wake na punda wawili. Yule kijana wa kike akamwingiza nyumbani mwa baba yake, naye baba yake alipomwona akafurahi kwa kukutana naye.
4Mkwewe, babake yule kijana wa kike, akamshika, akae naye siku tatu; wakala, wakanywa, wakalala huko.
5Siku ya nne wakaamka na mapema; alipotaka kuondoka, aende zake, babake yule kijana wa kike akamwambia mkwewe: Ushikize moyo wako kwa chakula kidogo, kisha mtakwenda zenu.
6Basi, wakakaa, wakala wao wawili pamoja, wakanywa, kisha babake yule kijana wa kike akamwambia huyu mtu: Afadhali ulale, moyo wako upate kuchangamka.
7Yule mtu alipoamka, aende zake, mkwewe akamhimiza kwa kumwomba, basi, akarudi, akalala huko.
8Siku ya tano akaamka na mapema, aende zake; lakini babake yule kijana wa kike akasema: Ushikize moyo wako, mkawilie, mpaka jua lipinduke. Wakala wao wawili.
9Yule mtu alipoondoka, aende zake, yeye na suria yake na mtumishi wake, mkwewe, babake yule kijana wa kike, akamwambia: Tazama, mchana umekwisha fikia kuwa jioni, afadhali ulale! Tazama, jua limekwisha kuchwa; lala hapa, moyo wako upate kuchangamka! Kesho mtajidamka kwenda zenu, ufike hemani kwako.
10Lakini yule mtu hakutaka kulala tena, akaondoka, akaenda zake, akafika ng'ambo ya Yebusi, ndio Yerusalemu; naye alikuwa na punda wake wawili waliotandikwa, hata suria yake alikuwa naye.[#Amu. 1:21; 1 Mambo 11:4.]
11Walipokuwa karibu ya Yebusi, mchana ulikuwa umekuchwa kabisa; ndipo, mtumishi alipomwambia bwana wake: Twende, tufike humu mjini mwa Wayebusi, tulale humo!
12Bwana wake akamwambia: Tusifikie mjini mwa wageni wasio wana wa Isiraeli, ila tuendelee, tufike Gibea.
13Kisha akamwambia mtumishi wake: Twende kufika katika mji mmoja wa hapa mbele, tulale Gibea au Rama.
14Wakashika njia kwendelea kwenda, nalo jua likawachwea, walipokuwa karibu ya Gibea wa Benyamini.
15Wakafika huko na kuingia mle Gibea, wapate mahali pa kulala. Walipokwisha kuingia na kukaa katika uwanja wa mji, hakuna mtu aliyewakaribisha nyumbani, wapate kulala.
16Mara wakaona mzee aliyechelewa, naye akatoka kazini kwake shambani; naye mtu huyu alikuwa wa milimani kwa Efuraimu, humo Gibea alikaa ugenini, maana wenyeji wa hapa walikuwa wana wa Benyamini.
17Alipoyainua macho yake akamwona yule mpitaji katika uwanja wa mji; ndipo, yule mzee alipomwuliza: Unakwenda wapi? Tena umetoka wapi?
18Akamwambia: Sisi tu wapitaji; tumetoka Beti-Lehemu wa Yuda, tunakwenda huko ndani milimani kwa Efuraimu, ndiko, nilikotoka; nalikwenda Beti-Lehemu wa Yuda, na sasa ninakwenda nyumbani mwa Bwana, lakini hakuna mtu aliyenikaribisha nyumbani.
19Tunayo mabua ya ngano na chakula kingine cha punda zetu, hata mikate na mvinyo mtumishi wako anayo ya kunitunza mimi na mjakazi wako na kijana huyu, hakuna ukosefu wa kitu cho chote.
20Mzee akamwambia: Tengemana tu! Yote unayoyakosa nitakupatia, usilale tu nje uwanjani!
21Akamwingiza nyumbani mwake, hata punda akawapa ya kula. Kisha wakaiosha miguu yao, wakala, wakanywa.
22Wao walipokuwa wanaichangamsha mioyo yao, mara watu wa mjini wasiofaa kitu wakaizunguka hiyo nyumba na kugonga mlangoni, wakamwambia mwenye nyumba, yule mzee kwamba: Mtoe huyo mtu aliyeingia nyumbani mwako, tumjue![#1 Mose 19:4-5.]
23Ndipo, mwenye nyumba alipotokea kwao, akawaambia: Ndugu zangu, hivi sivyo! Msifanye mabaya! Kwa kuwa mtu huyu ameingia nyumbani mwangu, msifanye upumbavu kama huu.[#1 Mose 19:7.]
24Tazameni, yuko mwanangu wa kike, ni mwanamwali, tena yuko suria yake; hawa nitawatoa kwenu, mwakorofishe na kuwatendea yote, mtakayoyaona kuwa mema, lakini mtu huyu msimfanyizie upumbavu kama huu!
25Lakini hao watu wakakataa kumsikia; ndipo, yule mtu alipomkamata suria yake, akamtoa nje kwao. Nao walipomjua wakamfanyizia mabaya usiku kucha mpaka asubuhi; kulipopambazuka, ndipo, walipomwachia.
26Usiku ulipokucha, yule mwanamke akaja, akaanguka mlangoni penye nyumba ya yule mtu, bwana wake alimokuwa, akalala hapo chini, mpaka mchana ukitokea.
27Bwana wake alipoinuka asubuhi, akaifungua milango ya nyumba; tena alipotoka, ashike njia ya kwenda zake, mara akamwona suria yake vivyo hivyo, alivyokuwa ameanguka mlangoni penye nyumba, mikono yake ikishika kizingiti.
28Alipomwambia: Inuka, twende zetu! hakuna aliyejibu. Ndipo, alipomchukua na kumweka juu ya punda; ndivyo, yule mtu alivyoondoka kwenda kwao.
29Alipofika nyumbani mwake, akatwaa kisu, kisha akamshika suria yake, akamkata mifupa kwa mifupa kuwa vipande kumi na viwili, akavituma kufika mipakani po pote kwao Waisiraeli.[#1 Sam. 11:7.]
30Kila mtu aliyeviona akasema: Jambo kama hili halijafanyika, wala halijaonekana tangu siku hiyo, wana wa Isiraeli walipotoka Misri kwenda kupanda huku, mpaka siku hii ya leo. Haya! Liwekeni mioyoni mwenu, mpige mashauri, kisha mseme!