The chat will start when you send the first message.
1Watu wa Efuraimu wakamwuliza: Kwa nini umetufanyizia hivi, usituite, ulipokwenda kupigana na Wamidiani? Wakamgombeza kwa nguvu.[#Amu. 12:1.]
2Naye akawaambia: Sasa mimi nimefanya nini, nijifananishe nanyi? Maokotezo ya Efuraimu siyo mema kuliko mavuno ya Abiezeri?[#Amu. 6:11,15.]
3Mikononi mwenu Mungu amewatia wakuu wa Wamidiani, Orebu na Zebu; nami nimeweza kufanya nini, nijifananishe nanyi? Ndipo, roho zao zilipomtulilia kwa kusema maneno haya.
4Gideoni alipoufikia Yordani, akauvuka yeye na wale watu 300 waliokuwa naye, lakini walikuwa wamechoka kwa kuwakimbiza adui.
5Kwa hiyo akawaambia watu wa Sukoti: Wapeni watu hawa wanaonifuata mikate! Kwani wamechoka, nami ninawakimbiza wafalme wa Midiani, Zeba na Salmuna.
6Lakini wakuu wa Sukoti wakamwambia: Je? Makonde ya Zeba na ya Salmuna yamo sasa mkononi mwako, tuwape mikate watu wa vikosi vyako?
7Gideoni akawaambia: Basi; hapo, Bwana atakapomtia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, ndipo, nitakapoziponda nyama za miili yenu kwa miiba ya nyikani na kwa mikunju.
8Alipotoka huko akapanda Penueli, nao wa huko akawaambia yaleyale, lakini watu wa Penueli wakamjibu, kama watu wa Sukoti walivyomjibu.
9Ndipo, alipowaambia nao watu wa Penueli kwamba: Nitakaporudi salama, nitaubomoa mnara huu.
10Lakini Zeba na Salmuna walikuwa huko Karkori pamoja na majeshi yao, kama watu 15000, ndio wote waliosalia wa hayo majeshi yao waliokaa upande wa maawioni kwa jua; nao waliouawa walikuwa 120000 waliojua wote kutumia panga.
11Gideoni akashika njia yao wanaosafiri na kukaa mahemani iliyopita Noba na Yogibeha upande wa Maawioni kwa jua, akayapiga yale majeshi, kwani majeshi hayo yalikuwa yakitulia tu.
12Ndipo, Zeba na Salmuna walipokimbia, lakini akawafuata mbiombio, akawakamata hawa wafalme wawili wa Midiani, Zeba na Salmuna, nayo majeshi yote akayatapanya kwa kuyastusha.
13Gideoni, mwana wa Yoasi, alipotoka vitani, arudi, akashika njia ya juu ipitayo Heresi.
14Huko akakamata kijana wa Sukoti wa kumwuliza, naye akamwandikia majina ya wakuu wa Sukoti na ya wazee na huko 77.
15Alipofika kwao wale watu wa Sukoti akawaambia: Watazameni akina Zeba na Salmuna, ambao mlinisimanga kwa ajili yao kwamba: Je? Makonde ya Zeba na ya Salmuna yamo sasa mkononi mwako, tuwape mikate watu wako waliochoka?
16Kisha akawachukua wazee wa mji na miiba ya nyikani na mikunju, akaitumia ya kuwafundisha watu wa Sukoti.
17Kisha akaubomoa mnara wa Penueli, nao watu wa mji huu akawaua.
18Kisha akamwuliza Zeba na Salmuna: Wale watu, mliowaua huko Tabori walikuwa wenye sura gani? Wakasema: Walikuwa kama wewe, kila mmoja wao; ukimtazama, alikuwa kama mwana wa mfalme.
19Ndipo, aliposema: Ndio ndugu zangu, wana wa mama yangu. Hivyo, Bwana alivyo Mwenye uzima, kama mngaliwaacha, wakae, nisingewaua ninyi!
20Kisha akamwambia Yeteri, mwanawe wa kwanza: Inuka, uwaue! Lakini huyu kijana hakuuchomoa upanga wake kwa kuwa na woga, kwani angaliko kijana.
21Ndipo, Zeba na Salmuna waliposema: Inuka wewe, utupige! Kwani mtu alivyo, ndivyo, nazo nguvu zake zilivyo. Ndipo, Gideoni alipoinuka, akamwua Zeba, naye Salmuna, akayachukua manyamwezi yaliyokuwa shingoni pa ngamia wao.
22Kisha watu wa Kiisiraeli wakamwambia Gideoni: Sharti ututawale wewe na mwanao na mjukuu wako, kwa kuwa umetuokoa mikononi mwa Wamidiani.
23Lakini Gideoni akawaambia: Mimi sitawatawala ninyi, wala mwanangu hatawatawala ninyi, sharti Bwana awatawale ninyi.
24Kisha Gideoni akawaambia: Liko moja, ninalolitaka kwenu: Nipeni kila mtu mapete ya masikioni, aliyoyateka, kwani walivaa mapete ya masikioni ya dhahabu kwa kuwa Waisimaeli.
25Wakasema: Tutakupa kabisa. Wakatanda nguo zao, wakatupia humo kila mtu mapete yake ya masikioni, aliyoyateka.
26Uzito wa haya mapete ya dhahabu ya masikioni, aliyoyataka, ukawa mzigo mkubwa wa mtu (sekeli 1700 za dhahabu, ndio ratli 62) pasipo manyamwezi na mapambo mengine ya masikioni na mavazi ya kifalme, wafalme wa Wamidiani waliyoyavaa, tena pasipo mikufu ya shingoni pa ngamia wao.
27Kisha Gideoni akazitumia hizo dhahabu za kutengeneza kisibau cha mtambikaji, akakiweka mjini kwake Ofura. Kwa kukitambikia huko Waisiraeli wote wakamfanyia Mungu ugoni; ndivyo, kilivyokuwa tanzi la kumnasa Gideoni na mlango wake.[#2 Mose 28:6-14; Amu. 17:5.]
28Wamidiani kwa hivyo, walivyonyenyekezwa mbele ya wana wa Isiraeli, hawakuviinua tena vichwa vyao, kwa hiyo nchi ikapata kutulia katika siku za Gideoni miaka 40.[#Amu. 3:11; 5:31.]
29Kisha Yerubaali, mwana wa Yoasi, akaenda zake kukaa nyumbani kwake.
30Yeye Gideoni akapata wana 70, aliowazaa, kwani alikuwa na wanawake wengi.
31Hata suria aliyekaa Sikemu akamzalia mwana, naye akamwita jina lake Abimeleki (Baba ni Mfalme).
32Gideoni, mwana wa Yoasi, akafa, mwenye uzee mwema, akazikwa kaburini mwa baba yake Yoasi kule Ofura kwa Abiezeri.[#Amu. 6:11.]
33Gideoni alipokwisha kufa, wana wa Isiraeli wakamfanyia Mungu ugoni tena na kuyafuata Mabaali, wakamtumia Baali la agano kuwa mungu wao.[#Amu. 2:11; 9:4.]
34Kwani wao wana wa Isiraeli hawakumkumbuka Bwana Mungu wao aliyewaponya mikononi mwa adui zao wote waliowazunguka,
35wala mlango wa Yerubaali, ndiye Gideoni, hawakuutedea mambo ya upole, kwamba wayalipe hayo mema yote, aliyowafanyizia Waisiraeli.[#Amu. 9:5,19,24.]