Yeremia 33

Yeremia 33

Kuokolewa katika uhamisho wa Babeli.

1Neno la Bwana likamjia Yeremia mara ya pili, alipokuwa amefungwa bado uani penye kifungo, la kwamba:[#Yer. 32:2.]

2Hivi ndivyo, anavyosema Bwana aliye mwenye kuvifanya, anavyovitengeneza, avitimize, Bwana ni Jina lake.

3Niite! ndipo, nitakapokujibu, nikuambie mambo makuu yaliyo magumu, usiyoyajua.

4Kwani hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema kwa ajili ya nyumba za mji huu na kwa ajili ya nyumba za wafalme wa Yuda zilizobomolewa, zitumike kujenga maboma ya kuzuilia panga;[#Yes. 22:10.]

5akasema hata kwa ajili yao waliokuja kupigana na Wakasidi, lakini wakawapatia tu watu wengi wa kuwaua, ndio wao, niliowapiga kwa makali yangu yaliyowaka moto, ndio wao, niliowaficha uso wangu, watu wa mji huu wasiuone kwa ajili ya mabaya yao.

6Mtaniona, nikiwapatia uzima na uponya; nitawaponya, kisha nitawafunulia mfuriko wa utengemano ulio wa kweli.

7Nitayafungua mafungo ya Wayuda na mafungo ya Waisiraeli, nitawajenga, wawe, kama walivyokuwa mwanzo.[#Yer. 29:14; 30:3.]

8Nitawaeua, maovu yote, waliyonikosea, yawatoke, nikiwaondolea hayo maovu yao yote, waliyonikosea na kunitengua.[#Yer. 31:34.]

9Ndipo, jina lake huo mji litakapokuwa la kunifurahisha kwa kunisifu na kunitukuza kwenye mataifa yote ya huku nchini, kwani watayasikia mema yote, mimi niliyowafanyizia, nao watastuka na kutetemeka kwa ajili ya hayo mema yote na kwa ajili ya huo utengemano wote, nitakaowapatia mimi.

10Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Ninyi mnapaita mahali hapa Penye mavunjiko, kwa kuwa hapana mtu wala nyama, lakini hapa napo penye miji ya Yuda na penye barabara za Yerusalemu zilizo peke yao, kwa kuwa hapana mtu wala apitaye wala akaaye wala hapana nyama,

11ndipo, patakaposikilika tena sauti za vicheko na sauti za furaha, hata sauti za wachumba wa kiume na wa kike, tena sauti zao wasemao: Mshukuruni Bwana Mwenye vikosi, ya kuwa Bwana ni mwema! Ya kuwa upole wake ni wa kale na kale! Watavileta vipaji vyao vya kumshukuru katika Nyumba ya Bwana, kwani nitayafungua mafungo ya nchi hii, iwe, kama ilivyokuwa mwanzo.[#Yer. 7:34; Ez. 3:11; Sh. 106:1.]

12Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mahali hapa palipo Penye mavunjiko, kwa kuwa hapana mtu wala nyama, napo penye miji yake yote patakuwa tena na malisho ya wachungaji, wanapowapumzisha kondoo wao.

13Katika miji iliyoko milimani, namo katika miji iliyoko mbugani, namo katika miji iliyoko upande wa kusini, hata katika nchi ya Benyamini na pande zote za Yerusalemu, namo katika miji ya Yuda makundi ya kondoo yatapita tena yakichungwa na mikono yao wanaowahesabu; ndivyo, Bwana anavyosema.[#Yer. 32:44.]

14Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija, nitakapolitimiza lile neno jema, nililowaambia walio wa mlango wa Isiraeli nao walio wa mlango wa Yuda!

15Siku zile za wakati ule zitakapotimia, ndipo, nitakapomchipuzia Dawidi chipuko lenye wongofu, naye atafanya katika nchi hii yaliyo sawa yaongokayo.[#Yer. 23:5; Yes. 4:2.]

16Siku zile ndipo, nchi ya Yuda itakapookolewa, nao mji wa Yerusalemu utakaa salama, nalo jina, utakaloitwa ni hili: Bwana ni wongofu wetu.[#Yer. 23:6; 5 Mose 33:28.]

17Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwao wa Dawidi hatakoseka mtu atakayekaa katika kiti cha kifalme cha mlango wa Isiraeli.[#2 Sam. 7:12; 1 Fal. 9:5.]

18Hata kwao watambikaji na Walawi hatakoseka mtu wa kutumikia usoni pangu, kama ni kuteketeza ng'ombe za tambiko au kuvukiza vipaji vya tambiko au kuyatengeneza matoleo ya tambiko ya kila siku.

Agano la Mungu la kale na kale.

19Neno la Bwana likamjia Yeremia kwamba:

20Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Hamwezi kulivunja agano langu la mchana wala agano langu la usiku, pasiwe mchana wala usiku panapopasa.[#Yer. 31:35-36.]

21Vilevile agano langu, nililoliagana na mtumishi wangu Dawidi, halitawezekana kuvunjwa asiwe na mwanawe atakayetawala na kukaa katika kiti chake cha kifalme, wala wasipatikane Walawi walio watambikaji wa kunitumikia.

22Kama vikosi vya mbinguni visivyohesabika, tena kama mchanga wa baharini usivyopimika, ndivyo, nitakavyowafurikisha walio wa kizazi cha mtumishi wangu Dawidi kuwa wengi, hata Walawi wanaonitumikia.[#1 Mose 15:5; 22:17.]

23Neno la Bwana likamjia Yeremia kwamba:

24Hukusikia, watu hawa wa huku wanavyosema kwamba: Koo mbili, Bwana alizozichagua, amezitupa? Kwa hiyo huwabeza walio ukoo wangu, wasiwe taifa tena machoni pao.

25Lakini hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Agano langu la mchana na la usiku liko, nayo maongozi ya mbinguni na ya nchini yako, hayaondoki.[#Yer. 33:20.]

26Vilevile sitawatupa walio wa kizazi cha Yakobo na cha Dawidi, wala sitaacha kuchukua katika kizazi chake watakaowatawala walio wa kizazi cha Aburahamu na cha Isaka na cha Yakobo, kwani nitayafungua mafungo yao nitakapowahurumia.[#Yer. 32:44.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania