The chat will start when you send the first message.
1Yatakayowapata wana wa Amoni. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Je? Hakuna wana kwao Waisiraeli? Hakuna awezaye kulichukua fungu lake? Mbona Malkamu ameichukua nchi ya Gadi nao watu wa ukoo wake wanakaa katika miji yao?[#Ez. 25:2-7; Amo. 1:13-15; Sef. 2:8-11; 1 Fal. 11:5.]
2Ndivyo, asemavyo Bwana: Wataona, siku zikija, nitakapovumisha makelele ya vita huko Rabati ulio mji wa wana wa Amoni, nao utakuwa machungu ya mabomoko, nayo miji ya wana wao itateketezwa kwa moto; ndipo, Waisiraeli watakapoyachukua mafungu yao kwao walioyachukua. Ndivyo, Bwana anavyosema:
3Pigeni vilio, ninyi wa Hesiboni, ya kuwa Ai umebomolewa! Pigeni makelele, ninyi wanawali wa Raba! Jifungeni magunia! Ombolezeni na kwenda huko na huko penye nyua! Kwani Malkamu atakwenda kutekwa na kuhamishwa pamoja na watambikaji wake na wakuu wake.[#Yer. 49:1.]
4Mnayasifiaje mabonde zaidi, mlio na bonde lichuruzikalo maji, ninyi wanawali wakatavu? Mnaviegemea vilimbiko vyenu kwamba: Yuko nani atakayenijia?
5Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu Mwenye vikosi: Mtaniona, nikiwaletea mastusho toka pande zote pia, nanyi mtafukuzwa, kila mtu akimbie pasipo kutazama nyuma, tena hatakuwako atakayewakusanya hao watoro.
6Hayo yatakapokwisha, nitayafungua mafungo ya wana wa Amoni.[#Yer. 48:47.]
7Yatakayowapata Waedomu. Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Je? Huko Temani hakuna tena werevu wa kweli? Wajuzi wamepotelewa na akili, werevu wao wa kweli ukatoweka?[#Yes. 21:11; 34:5-15; Ez. 25:12-14; Amo. 1:11-12; Oba. 1-21.]
8Kimbieni, mtoroke! Chimbeni mashimo ya kukaa ndani yao, ninyi mkaao Dedani! Kwani nitawaletea angamio la Esau siku ya kuwapatiliza.
9Kama wachuma zabibu wanakujia, hawasazi za kuokoteza; kama wezi wanakujia na usiku, hupokonya, mpaka wakitoshewa.
10Kwani mimi nimemvumbua Esau, nikayafunua maficho yake, asiweze kujificha tena. Kizazi chake kumeharibiwa pamoja na ndugu zake, nao waliokaa nao hawako kabisa.
11Waacheni watoto wenu waliofiwa na wazazi! Mimi nitawatunza; nao wajane wenu na waniegemee!
12Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Tazama, wasiopaswa kukinywa kinywaji changu hawakuwa na budi kukinywa, nawe wewe usilipishwe? Nawe utalipishwa, kwani utakinywa![#Yer. 25:15,21.]
13Ndivyo, asemavyo Bwana: Nimejiapia mwenyewe kwamba: Bosira sharti ustukiwe kwa kutiwa soni, ukae peke yake kwa kuapizwa, nayo miji yake yote itakuwa mabomoko kale na kale.[#Yer. 44:12.]
14Nimesikia mbiu kwake Bwana, mjumbe ametumwa kwenda kwa mataifa kwamba: Jikusanyeni, mwujie! Ondokeni kwenda vitani!
15Kwani mtaniona, nikiwafanya kuwa wadogo katika mataifa, mbezwe na watu!
16Kuogopesha kwenu ni majivuno tu ya mioyo yenu yaliyowadanganya, kwa kuwa mnakaa nyufani kwenye miamba, mkagandamana na milima mirefu. Lakini ijapo mvijenge vituo vyenu juu kabisa kama tai, huko nako nitawashusha; ndivyo, asemavyo Bwana.
17Nchi ya Edomu itakuwa mapori matupu, kila atakayepapita atastuka na kuyazomea mapigo yake yote.[#Yer. 50:13.]
18Bwana anasema: Kama Sodomu na Gomora ilivyoangamizwa pamoja na vijiji vyao, hivyo napo hapo hapatakaa mtu, wala hapatalala mgeni wa kimtu.[#Yes. 1:9.]
19Kama simba anavyopanda akitoka machakani kwenye Yordani, ajie maboma yenye nguvu, ndivyo, nitakavyowakimbiza kwao kwa mara moja, naye aliyechaguliwa nitamweka kuwa mkuu wao, kwani yuko nani afananaye na mimi? Au yuko nani atakayeniwekea siku? Yuko mchungaji gani atakayesimama usoni pangu?[#Yer. 50:44.]
20Kwa hiyo lisikieni shauri la Bwana, alilowakatia Waedomu, nayo mawazo yake, aliyowawazia wakaao Temani: kweli watakaowakokotakokota ndio wadogo wa makundi, kweli nchi yao yenyewe itawastukia.
21Kwa mtutumo wa kuanguka kwao nchi itatetemeka, nazo sauti za vilio vyao zitasikilika hata kwenye Bahari Nyekundu.
22Tazameni, anaurukia Bosira kama kozi na kuukunjulia mabawa yake. Kwa hiyo mioyo ya wapiga vita wa Edomu itakuwa siku ile kama moyo wa mwanamke anayetaka kuzaa.
23Yatakayoupata Damasko. Hamati na Arpadi wamepatwa na soni, kwani wamesikia mbiu mbaya, wakayeyuka na kuhangaika kama bahari isiyoweza kutulia.[#Yes. 17:1; Amo. 1:3-5.]
24Wadamasko wamelegea, wakageuka, wakimbie, mtetemeko ukawashika, masongano na machungu yakawapata kama mwanamke anayetaka kuzaa.
25Kumbe umeachwa wote mji huo uliokuwa mji, walimoshangilia kwa kufurahi!
26Kwa hiyo wavulana wake wataanguka barabarani mwake, nao wapiga vita wote watanyamazishwa siku ile; ndivyo, asemavyo Bwana Mwenye vikosi.
27Kisha nitawakisha moto bomani mwa Damasko, uyale majumba ya Beni-hadadi.
28Yatakayoipata nchi ya Kedari nazo nchi za kifalme za Hasori, Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, alizozipiga. Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Inukeni, mpande kwenda Kedari, mwaangamize wana wa nchi iliyoko maawioni kwa jua![#Yes. 21:16-17; Yos. 11:10.]
29Na wayachukue mahema yao na makundi yao, wajitwalie mazulia yao na vyombo vyao vyote na ngamia wao, nao watawalilia kwamba: Matisho po pote!
30Kimbieni na kupiga mbio sana! Chimbeni mashimo ya kukaa ndani yao, ninyi mkaao Hasori! ndivyo, asemavyo Bwana; kwani Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, amewakatia shauri na kuwawazia mawazo.[#Yer. 49:8.]
31Ndivyo, asemavyo Bwana: Inukeni, mpande kwenda kwa taifa lililojituliza na kukaa pasipo mahangaiko! Hawama milango wala makomeo, hujikalia peke yao tu.
32Ngamia wao watakuwa mateka yenu, nao kondoo na mbuzi wao wengi mno watakuwa mapato yenu. Wao wenyewe wanyoao denge nitawatawanya kwenda pande zote, upepo utokako, nikiwaletea maangamizo, yawatokee po pote; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 9:26; 25:23.]
33Ndipo, Hasori utakapokuwa kao la mbwa wa mwitu kwa kukaa peke yao tu kale na kale. Hapatakaa mtu, wala hapatalala mgeni wa kimtu.[#Yer. 9:11.]
34Hili ndilo neno la Bwana lililomjia mfumbuaji Yeremia kuwaambia Waelamu, Sedekia, mfalme wa Yuda, alipoanzia kuwa mfalme.[#Yer. 25:25.]
35Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Mtaniona, nikizivunja pindi zao Waelamu, nguvu zao nyingi zilimo.
36Nitawaletea Waelamu pepo nne zitokazo pande nne za mbinguni, niwatawanye kwenye hizo pepo, pasiwe taifa lisilojiwa na watoro wa nchi ya Elamu.
37Nitawastusha Waelamu, wawaogope adui zao nao wazitafutao roho zao; kisha nitawaletea mabaya, makali yangu yenye moto yatakapowawakia, mpaka niwamalize.
38Ndipo, nitakapokiweka kiti changu cha kifalme huko Elamu, nimwangamize mfalme na wakuu, watoweke huko; ndivyo, asemavyo Bwana.
39Lakini siku zitakapotimia, nitayafungua mafungo ya Waelamu; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 49:6.]