Yeremia 51

Yeremia 51

Mji wa Babeli utatekwa na Wamedi; ndipo, Wayuda watakapofunguliwa.

1Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mtaniona, nikiinua upepo uangamizao, uujie Babeli nao wakaamo walio wenye mioyo ya kuniinukia.

2Nitatuma wenye nyungo kwenda Babeli, waupepete, kisha watazichukua mali za nchi, kwani siku ile mbaya watazunguka mjini po pote.[#Yer. 15:7.]

3Hapo hatakuwako mwenye upindi atakayewapiga mshale, wala hatakuwako mwenye shati ya chuma atakayeweza kuwainukia. Lakini msiwaonee uchungu vijana wake! Ila wao wote wa vikosi vyao watieni mwiko wa kuwapo!

4Hivyo wataanguka tu katika nchi ya Wakasidi waliopata vidonda, nao waliochomwa watalala huko barabarani.

5Kwani Isiraeli na Yuda hawakuachwa na Mungu wao aliye Bwana Mwenye vikosi, wawe wajane, ila nchi yao wale ilijaa maovu, waliyomkosea Mtakatifu wa Isiraeli.[#Yer. 50:11,29; Yes. 54:4.]

6Kimbieni na kutoka mwake Babeli, kila mtu aiponye roho yake, msinyamazishwe kwa ajili ya manza, walizozikora wao! Kwani hii ndiyo siku ya lipizi ya Bwana, awalipishe matendo yao.[#Yer. 50:8; Yes. 48:20; Ufu. 18:4.]

7Babeli ulikuwa kinyweo cha dhahabu mkononi mwa Bwana kilichozilevya nchi zote; mvinyo yake mataifa yaliinywa, kwa hiyo mataifa yakaingiwa na wazimu.[#Yer. 25:25; Ufu. 17:4; 18:3.]

8Mara Babeli umeanguka, ukavunjika! Ulilieni! Leteni mafuta ya kwaju kuyatia penye madonda yake! Labda utapona.[#Ufu. 18:2.]

9Tulitaka kuuponya Babeli, lakini haukuponyeka; basi, uacheni, twende kila mtu katika nchi ya kwao! Kwani hukumu yake inafika hata mbinguni, inakwenda juu mpaka kwenye mawingu.

10Bwana ameyatokeza, ya kuwa mambo yetu yameongoka; njoni, tusimulie Sioni, Bwana Mungu wetu aliyoyafanya.

11Inoeni mishale! Zishikeni ngao! Bwana ameziinua roho za wafalme wa Wamedi, kwani mawazo yake yameuelekea Babeli, auangamize, kwani hili ndilo lipizi lake Bwana, alilipizie Jumba lake takatifu.[#Yer. 50:28; Yes. 13:17.]

12Twekeni bendera zielekeazo kuta za Babeli! Malindo yatieni nguvu mkiongeza walinzi na kuweka nao wenye kuvizia! Kwani Bwana aliyoyawaza huyafanya, ayatimize nayo yale, aliyoyasema, ya kuwa atawafanyizia wakaao Babeli.

13Unakaa penye maji mengi, unavyo vilimbiko, lakini mwisho wako umefika, ndipo hapo palipopimiwa choyo chako.[#Ufu. 17:1.]

14Bwana Mwenye vikosi amejiapia mwenyewe kwamba: Ijapo nimekujaza watu kama nzige, itakuwa, wakuzomee kwa kukushinda.

(15-19: Yer. 10:12-16)

15Yeye ndiye aliyeifanya nchi kwa uwezo wake, akausimika ulimwengu kwa werevu wake wa kweli, akazitanda mbingu kwa utambuzi wake.

16Huvumisha maji mbinguni kwa ngurumo na kupandisha mawingu yatokayo mapeoni kwa nchi, kisha hupiga umeme kwenye mvua na kutoa upepo huko, alikouweka.

17Ndipo, kila mtu anapopumbaa tu, asijue yatokako, hata kila mfua dhahabu hupatwa na soni kwa ajili ya kinyago chake, kwani alichokitengeneza ni uwongo tu, hata pumzi haimo.

18Havina maana, ni kazi ya kuchekwa tu; siku vitakapopatilizwa huangamia.

19Lakini aliye fungu lake Yakobo hafanani navyo, kwani yeye ndiye aliyeyatengeneza yote, naye Isiraeli ni ukoo uliopata fungu kwake; Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake.

20Kweli ulikuwa nyundo yangu, nikakutumia kuwa chombo cha vita; hivyo nikaponda mataifa, nikaangamiza nchi za kifalme kwa kukutumia.[#Yer. 50:23; Yes. 10:5.]

21Nikaponda farasi pamoja nao waliowapanda kwa kukutumia, nikaponda magari nao walioyapanda kwa kukutumia.

22Nikaponda waume na wake kwa kukutumia, nikaponda wazee na wana kwa kukutumia, nikaponda wavulana na wasichana kwa kukutumia.

23Nikaponda wachungaji na makundi yao kwa kukutumia, nikaponda wakulima pamoja na ng'ombe wao wa kulima kwa kukutumia, nikaponda watawala nchi na wakuu kwa kukutumia.

24Lakini machoni penu nitaulipisha Babeli pamoja nao wote wakaao katika nchi ya Wakasidi mabaya yao yote, waliyoyafanya huko Sioni; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yer. 50:29.]

25Ndivyo, asemavyo Bwana: Utaniona, nikikujia wewe, mlima uangamizao! Umeziangamiza nchi zote, lakini nimekukunjulia mkono wangu, nikuporomoshe, utoke miambani; nitakugeuza kuwa mlima uliochomwa moto.

26Hawatachukua kwako mawe ya pembeni wala ya msingi, kwani utakuwa jangwa la kale na kale; ndivyo, asemavyo Bwana.

27Twekeni bendera katika nchi hii! Pigeni mabaragumu kwa mataifa! Yaeueni mataifa, yaujie! Ziiteni nchi za kifalme za Ararati na za Mini na za Askenazi, ziujie! Wekeni mkuu wa vita, aupige! Pandisheni farasi walio wengi kama nzige wenye manyoya![#1 Mose 10:3; Yes. 13:3.]

28Yaeueni mataifa, yaujie, wafalme wa Wamedi nao watawala nchi wa kwao nao wakuu wao wote na nchi zote za ufalme wao!

29Ndipo, nchi itakapotetemeka kwa kustuka, kwani mawazo yake Bwana yameuinukia Babeli kuigeuza nchi ya Babeli kuwa peke yake tu, isikae mtu.

30Wapiga vita wa Babeli wameacha kwenda vitani, hukaa ngomeni, nguvu zao zimezimia, wakageuka kuwa wanawake; makao yao ya mjini wameyateketeza, makomeo yao yakavunjwa.

31Mkimbizi anamfuata mkimbizi mwenziwe, vilevile mjumbe anamfuata mjumbe mwenziwe kumpasha mfalme wa Babeli habari, ya kuwa mji wake umetekwa, wakiutokea pande zote;

32ya kuwa vivuko vyote vimechukuliwa, ya kuwa manyasi ya bwawani yamechomwa moto, kwa hiyo wapiga vita wakaishia ukali.

33Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema: Binti Babeli anafanana na mahali pa kupigia ngano pakitengenezwa na kupondwa, siku za mavuno zitaujia bado kidogo.

34Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, amenila, amenitowesha, ameniweka kuwa chombo kitupu, amenimeza kama joka na kulijaza tumbo lake, akanifukuza katika paradiso yetu.

35Makorofi, waliyonitendea, nayo miili ya watu, waliowaua kwetu, na iujie Babeli! ndivyo, watakavyosema wakaao Sioni; damu, walizozimwaga kwetu, na ziwajie wakaao katika nchi ya Wakasidi! ndivyo, watakavyosema Wayerusalemu.

36Kweli hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kwa hiyo mtaniona, nikiwagombea magomvi yenu, nikiwalipizia malipizi yenu; nitaukausha mto wao mkubwa, navyo visima vyao nitavinyima maji, vipwe.

37Hivyo Babeli utageuka kuwa machungu ya mabomoko na makao ya mbwa wa mwitu, kwa kustukiwa utazomelewa, kwa kuwa hautakaa mtu.[#Yer. 50:13.]

38Watanguruma wote pamoja kama simba, wataguna kama simba wachanga.

39Lakini vichwa vyao vitakapokuwa vinene, ndipo, nitakapowapa vinywaji vyao vya kuwalevya, wapige vigelegele, kisha walale usingizi wa kale na kale, wasiamke tena; ndivyo, asemavyo Bwana.

40Nitawaangusha kama wana kondoo, wakichinjwa kama madume ya kondoo na ya mbuzi.

41Kumbe Sesaki umetekwa! Kumbe umechukuliwa uliosifiwa na nchi zote! Kumbe Babeli umegeuka kuwa stusho kwa mataifa![#Yer. 25:26.]

42Bahari imepanda kuja Babeli, ukafunikizwa na mawimbi yake yaumukayo.

43Miji yake ikawa ya kustukiwa kwa kuwa nchi kavu na jangwa, ni nchi isiyokaa mtu ye yote, wala hapapiti mwana wa mtu.

44Nitampatiliza naye Beli mle Babeli nikitoa kinywani mwake, aliyoyameza, mataifa yasimjie tena mengi na mengi; nazo kuta za boma la Babeli zitaanguka.[#Yer. 50:2.]

45Tokeni mwake, ninyi mlio ukoo wangu! Kila mtu na aiponye roho yake, asifikiwe na makali yake Bwana yenye moto![#Yer. 51:6.]

46Mioyo yenu isizimie kwa woga, mtakapozisikia zile habari zitakazosikilika katika nchi hii, mwaka mmoja ikija habari, mwaka mwingine ikija habari tena, nao ukorofi ukizidi katika nchi hii, kwa kuwa watawala nchi watainukiana.

47Kwa hiyo mtaona, siku ikija, nitakapovipatiliza vinyago vya Babeli, nchi yake yote ipatwe na soni, kwa kuwa watu wake wote waliouawa wataanguka mlemle mwake.

48Ndipo, mbingu na nchi navyo vyote vilivyomo vitakapouzomea Babeli, kwani toka kaskazini waangamizaji wataujia; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Ufu. 18:20.]

49Babeli nao utaanguka kwa ajili ya Waisiraeli walioanguka wakiuawa, kama walivyoanguka watu wa nchi zote wakiuawa kwa ajili ya Babeli.

50Ninyi mliozikimbia panga, nendeni tu msisimame! Nako katika nchi za mbali mkumbukeni Bwana! Nao Yerusalemu na uingie mioyoni mwenu![#Sh. 137:5.]

51Tuliona soni, tulipotukanwa, nyuso zetu zote zikaiva kabisa, wageni walipopaingia Patakatifu pa Nyumba ya Bwana.

52Ndivyo, asemavyo Bwana: Kwa hiyo mtaona, siku zikija, nitakapovipatiliza vinyago vyake Babeli; ndipo, wenye kuumizwa watakapopiga kite katika nchi yake yote.

53Babeli ingawa upande hata mbinguni kujijengea huko juu ngome yenye nguvu, huko nako waangamizaji wataujia; ndivyo, asemavyo Bwana.

54Sauti za makelele zinasikilika upande wa Babeli na shindo la vunjiko kubwa upande wa nchi ya Wakasidi.

55Kwani Bwana anauangamiza Babeli na kuzikomesha sauti za makelele yake makuu; mawimbi yanayoujia yanavuma kama maji mengi, sauti za kuumuka kwao zinazidi.

56Kwani mwangamizaji ameujia Babeli, wapiga vita wake watekwe, pindi zao zivunjwe, kwani Bwana ni Mungu mwenye lipizi, hulipisha, naye hasazi akilipisha.[#5 Mose 32:35.]

57Ndipo, nitakapowalevya wakuu wake na werevu wake wa kweli na watawala nchi wake na wajumbe wake na wapiga vita wake, walale usingizi wa kale na kale, wasiamke tena; ndivyo, asemavyo Mfalme, Bwana Mwenye vikosi ni Jina lake.[#Yer. 51:39.]

58Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Kuta za boma la Babeli, zingawa ni nene, zitabomolewa mpaka chini, nayo malango yake, yangawa ni marefu, yatateketezwa kwa moto. Koo za watu husumbukia mambo ya bure, nayo makabila hujichokesha kwa ajili ya moto.[#Hab. 2:13.]

59Hili ndilo neno, mfumbuaji Yeremia alilomwagizia Seraya, mwana wa Neria, mwana wa Masea, alipokwenda Babeli pamoja na mfalme Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa ufalme wake; naye Seraya alikuwa mkuu wa makambi.[#Yer. 36:4.]

60Yeremia alikuwa ameyaandika hayo mabaya yote yatakayoujia Babeli katika kitabu kimoja, ni hayo maneno yote, Babeli uliyoandikiwa humo.

61Yeremia akamwambia Seraya: Utakapofika Babeli, jitafutie pafaapo, kisha yasome hayo maneno yote!

62Ndipo, utakaposema: Wewe Bwana, umepaambia mahali hapa, ya kuwa utapaangamiza, pasiwe mtu wala nyama atakayekaa hapa, kwani patakuwa peke yake tu kale na kale.

63Utakapokwisha kukisoma kitabu hicho, ukifungie jiwe, kisha ukitupe katikati katika mto wa Furati[#Ufu. 18:21.]

64ukisema: Hivi ndivyo, Babeli utakavyozama, usioneke tena kwa ajili ya mabaya, mimi nitakayouletea, hata wazimie.

Mpaka hapa ni maneno ya Yeremia.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania