The chat will start when you send the first message.
1Roho yangu mtaisikitisha mpaka lini
2kwa kujisemea maneno tu ya kuniumiza?
3Sasa ni mara kumi, mkinitukana; lakini kwa kunihangaisha hivyo hamwoni soni?
4Itakapotokea kuwa kweli, ya kama nimekosa, mimi ndiye, litakayemkalia hilo kosa langu.
5Kama mnajikuza kweli na kunibeua, kama mimi ni mtu apaswaye na kutwezwa, haya! Niumbueni!
6Jueni, ya kuwa ndiye Mungu aliyenipotoa kwa kunitegea pande zote tanzi lake.
7Tazameni! Nikiulilia ukorofi sijibiwi, wala hakuna aniamuliaye, nikilalamika.[#Iy. 30:20.]
8Njia yangu ameifunga kwa kitalu, nisipitie hapo, napo penye mikondo yangu amepapatia giza.[#Omb. 3:7,9.]
9Yaliyokuwa utukufu wangu amenivua, nacho kilemba amekiondoa kichwani pangu.
10Kwa sababu amenibomolea pande zote, sina budi kujiendea, nacho kingojeo changu ameking'oa, kama ni mti tu.
11Akanitolea makali yake, yaniwakie moto, akaniwazia kuwa kama mmoja wao wapingani wake.[#Iy. 13:24; 33:10.]
12Vikosi vyake vikaja, vikutanie pamoja, vikajitengenezea njia ya kufika kwangu, vikayapiga makambi yao, yanizunguke hemani mwangu.[#Iy. 30:12.]
13Ndugu zangu akawaweka mbali, wasije kwangu, nao wenzangu wa kujuana nao wakanigeukia kuwa kama wageni.[#Sh. 31:12; 69:9.]
14Walio wa ukoo wangu nao wakapotea, nao rafiki zangu wema wakanisahau.[#Sh. 38:12.]
15Waliokaa pamoja na watumishi wa kike nyumbani mwangu wao ndio wanaoniwazia kuwa mgeni, machoni pao nikageuka kuwa mtu asiye wa kwao.
16Nikimwita mtumishi wangu, haitikii, sharti nimwambie maneno mengi ya kumbembeleza.
17Pumzi zangu zinamchukia mke wangu, mnuko wangu mbaya unawachukia, niliowazaa mwenyewe.[#Iy. 2:9.]
18Nao walio vijana bado hunibezabeza, nikiinuka, husema maneno ya kunifyoza.[#Iy. 30:1.]
19Wote waliokuwa wenzangu wa njama wanachukizwa na mimi, nao waliogeuka kuwa wapingani wangu ndio, niliowapenda.[#Iy. 19:13.]
20Ngozi na nyama za mwili wangu zinagandamana na mifupa, kilichopona kwangu ni ufizi tu.[#Sh. 102:6.]
21Nihurumieni, nihurumieni, ninyi wenzangu! Kwani mkono wa Mungu umenipiga.[#Ruti 1:13.]
22Mbona mnanikimbiza kama Mungu, msishibe kuzinyafuanyafua nyama za mwili wangu?[#Sh. 27:2.]
23Laiti maneno yangu yangeandikwa kwa kupigwa chapa kitabuni!
24Laiti yangechorwa namo mwambani kwa kalamu ya chuma, kisha kutiwe risasi, yawepo kale na kale!
25Mimi ninayoyajua ndiyo haya: Mkombozi wangu yupo, ni mwenye uzima, naye huko mwisho ndiye atakayeinuka uvumbini.[#Yes. 41:14; Hos. 13:14; 2 Tim. 1:12.]
26Mwili wangu wenye ngozi utakapokwisha kuharibika, huu mwili wangu wenye nyama utakapokuwa haupo, hapo ndipo, nitakapopata kumwona Mungu;[#Sh. 17:15; 73:24.]
27mimi mwenyewe nitamwona kuwa wangu, macho yangu ndiyo yatakayomwona, siyo ya mgeni tu; mafigo yangu yanazimia ndani yangu kwa kuyatunukia hayo.[#1 Yoh. 3:2.]
28Mkisema: Haya! Na tumkimbize! kwani mizizi ya mambo haya imeonekana kwangu:
29uogopeni upanga rohoni mwenu! Kwani kutoa makali yenye moto hutupatia hukumu za upanga; zitakapotokea, ndipo, mtakapojua: mapatilizo yako!
Sofari wa Nama akajibu akisema: