Iyobu 23

Iyobu 23

1Je? Hata leo maombolezo yangu ni kumkataa Mungu?

2Kwani mkono wangu umelemea kwa kupiga kite.

3Ninatamani kuijua njia ya kumwona, nifike hapo, anapokaa.

4Ningemwelezea shauri langu, alijue, nikakijaza kinywa changu maneno ya kushindana naye.

5Ningejua maneno, atakayonijibu, na kuyatambua, atakayoniambia.

6Je? Kwa nguvu zake nyingi angenigombeza? Sivyo, mwenyewe angeniangalia na kunisikia.

7Hapo ningeshindwa naye kwa kunyoka, nikapona kale na kale mikononi mwake anihukumuye.

8Lakini nikienda upande wa maawioni kwa jua, hayuko; wala upande wa machweoni kwa jua simwoni,

9wala kushotoni, kama yuko katika kazi zake, simpati, tutazamane; wala kuumeni simwoni, sijui, alikogeukia.

10Lakini anaijua njia, niliyoishika: kama angenijaribu, ningetokea nikitakata kama dhahabu.[#Sh. 17:3; 139:23-24.]

11Kwani miguu yangu imeshika njia ya kuzifuata nyayo zake yeye, nikaiangalia hiyo njia yake, nisiiache.

12Sikurudi nyuma na kuliacha agizo la midomo yake, maneno ya kinywa chake nikayaangalia kuliko maongozi yangu.

13Lakini yeye alivyo, ndivyo alivyo, yuko nani awezaye kumgeuza? nayo roho yake inayoyataka kweli, huyafanya.

14Hivyo atayatimiliza nayo, aliyoyaagiza, yanipate mimi; yako mengi yaliyomo moyoni mwake kama hayo.

15Kwa hiyo nitastuka, nitakapomwona, nashikwa na woga naye nikijaribu kumtambua.

16Mungu ameutisha moyo wangu, yeye Mwenyezi akanistusha.

17Kwani kwa kuogopa giza sizimii, wala kwa kuliona giza lenye weusi, jinsi lilivyonifunika.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania