The chat will start when you send the first message.
1Ningoje kidogo, nikueleze mambo!
2Kwani yako mengine ya Mungu, nitakayoyasema.
3Haya, ninayoyajua, niliyatoa mbali, nimtokeze yeye aliyenifanya kuwa mwenye wongofu.
4Kweli maneno yangu siyo ya uwongo, anayesema na wewe ni mwenye ujuzi utimilikao.
5Tazama! Mungu ni mwenye uwezo, lakini hamtupi mtu, ni mwenye uwezo kwa nguvu zilizo za moyo.
6Hamkalishi uzimani asiyemcha, lakini watesekao huwakatia mashauri yaliyo sawa.[#Sh. 72:4,12.]
7Kwake mwongofu hayaondoi macho yake, anawakalisha pamoja na wafalme katika viti vya kifalme, wakae hapo kale na kale, wapate kutukuka.
8Lakini walipofungwa kwa mapingu, au walipokamatwa kwa kamba za mateso,
9ndipo, anapowaelezea matendo yao, wayaone, jinsi yalivyo, huwaonyesha mapotovu yao, waliyoyafanya kwa kujikuza.
10Hapo huwafunulia masikio, wasikie, akiwaonya, na kuwaambia, warudi na kuyaacha maovu yao, akiwatisha.[#Iy. 33:16.]
11Ikiwa, wanamsikia, waje kumtumikia, ndipo, watakapozimaliza siku zao na kuona mema, nayo miaka yao na kuifurahia;
12wengine sharti wapite penye mishale iuayo, ndio wasiomsikia; kwa kukosa ujuzi watazimia.
13Ndipo, wenye mioyo mipotovu watakapokasirika, lakini hawatajipa mioyo ya kupiga kelele, ya kuwa aliwafunga.
14Hivyo roho zao zitakufa katika ujana wao, nayo mioyo yao huzimia kwao wagoni.
15Lakini watesekao huwaponya katika mateso yao, akawafunua masikio kwa kuwasonga.[#Iy. 36:10.]
16Wewe nawe anakutaka, akuopoe katika masongano, akuweke papana pasipokusonga, nawe uandaliwe yenye mafuta mengi mezani pako.
17Lakini ukizidi kuzitamani hukumu zao wasiomcha Mungu. basi, hukumu zao na mashauri yao yatakupata kweli.
18Angalia, ukali usikuponze, ukitukana, wala wingi wa makombozi usikupoteze!
19Je? Makelele yako yatakupatia mahali pasiposongeka, ijapo, ujikaze kulia kwa nguvu zote?
20Usikutwetee kuchwa, kuwe usiku! Kwani ndio unaomaliza makabila mazima, yatoweke mahali pao.
21Jiangalie mwenyewe, usiyageukie maovu! Kwani ndiyo, unayoyapenda kuliko mateso.
22Tazama! Mungu hufanya makuu kwa nguvu zake, yuko nani awezaye kufundisha kama yeye?[#Sh. 25:9.]
23Yuko nani amwagizaye kuzishika njia zake yeye? Au yuko nani awezaye kumwambia: unafanya mapotovu?
24Usisahau kuyatukuza matendo yake, watu wanayoyaimbia!
25Watu wote huyatazamia na kuyachunguzia, yangaliko mbali.
26Tazama! Mungu ni mkuu, tusimjue hivyo, alivyo, hesabu ya miaka yake haichunguziki.
27Huvuta matone ya maji, yaje juu kuwa kungugu, kisha hugeuka kuwa mvua idondokayo chini;[#Iy. 5:10.]
28ndivyo, mawingu yanavyoichuruzisha, inyeshee watu wengi.
29Je? Yuko anayeyatambua matandazo ya mawingu? Au makao yake, ngurumo zitokamo?[#Sh. 104:3.]
30Tazama! Huutandaza umeme wake, umzunguke, navyo vilindi vya bahari huvifunika.[#Sh. 18:15-16.]
31Hivyo ndivyo, anavyoyapatiliza makabila ya watu, tena ndivyo, anavyowapa watu vyakula, viwe vingi mno.
32Mikono yote miwili huifunika kwa umeme, akauagizia wao, utakaowapiga.
33Ngurumo zake ndizo zinazoujulisha, akichafuka kwa kumkasirikia amwinukiaye.