Iyobu 37

Iyobu 37

Mwisho wa maneno ya Elihu: Utukufu wa Mungu.

1Kweli moyo wangu nao huyastukia hayo, ukakupuka mahali pake, ulipokuwa.

2Ngurumo za sauti yake zisikilizeni vema, nayo mavumi yanayotoka kinywani mwake![#Sh. 29:3.]

3Huzifungua, zienee po pote chini ya mbingu, nao umeme wake huufikisha nako mapeoni kwa nchi.

4Sauti yake hunguruma, ukiisha kuwapo; ndipo, unapoivumisha hiyo sauti yake yenye utukufu; kusudi sauti yake ipate kusikilika, hauzuii umeme.

5Mungu akiivumisha sauti yake, inastaajabisha; hufanya makuu, tusiyoweza kuyajua.

6Kwani huiambia kungugu: Anguka chini! nayo manyunyu huyafanya kuwa mvua, kisha hizo mvua huzitia nguvu zake, zinyeshe sana.[#Iy. 38:28; Sh. 147:16.]

7Hizo huizuia mikono ya watu wote kufanya kazi, wote pia wayajue matendo yake.

8Hapo nao nyama huenda kujificha, watulie mapangoni mwao, ndimo, wanamotaka kukaa.[#Sh. 104:22.]

9Chamchela hutoka chumbani mwake huko kusini, nako kaskazini hutoka upepo wenye baridi ufukuzao mawingu.

10Kwa pumzi ya Mungu hutokea barafu, nayo maji yaliyopanuka hugandamana.

11Hata mawingu huyalemeza kwa kuyatia maji mengi, yaanguke chini, tena hutandaza nayo mawingu yenye umeme wake.

12Naye huyaongoza, yageuke huko na huko kuzifanya kazi zao, atakazoyaagiza, zitendeke huku chini po pote panapokaa watu;

13kama anataka kuipiga nchi yake au kuihurumia, kila mara huyapeleka papo hapo, anapoyatakia kazi.

14Haya yasikilize, wewe Iyobu, upate kuyatambua vema mastaajabu ya Mungu!

15Jinsi Mungu anavyoyaagiza, unavijua? au jinsi anavyoumulikisha umeme ulioko mawinguni kwake?[#Iy. 38.]

16Je? Unayajua mawingu, jinsi yanavyoning'inia? Mastaajabu yake, aliyotimiza kuyajua yote, unayatambua nawe?

17Nguo zako hazikuwashi joto, wewe mtu, nchi ikitulia kwa jasho litokalo kusini?

18Je? Unaweza kuzitandaza mbingu kama yeye, ziwe kama kioo cha shaba kwa kushupaa hivyo?

19Haya! Na utujulishe tutakayomwambia! Sisi hatuwezi kuyatunga kwa kuwa gizani.

20Je? Atapashwa habari ya kwamba: Nataka kusema? Yuko mtu aliyesema, aangamizwe?

21Mwanga wa jua, likiwaka mbinguni, watu hawawezi kuutazama, upepo ukiisha kupita na kuyaondoa mawingu, pang'ae tena.

22Kaskazini hutokea mionzi ya jua imetukayo kama dhahabu, kweli utukufu wake Mungu huogopesha.

23Sisi hatukumwona Mwenyezi kwa kuwa mkuu mwenye nguvu, hapotoi shauri wala mambo yo yote yaongokayo.[#Iy. 28:12-28.]

24Kwa hiyo inapasa, watu wamwogope, hawatazami watu wo wote wajiwaziao kuwa werevu wa kweli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania