The chat will start when you send the first message.
1Ya kuwa unayaweza yote, ninayajua;
2uliyoyataka, hayazuiliki.
3Yuko nani awezaye kuyatowesha mashauri yako? Maana ni mtu asiyejua kitu. Kweli nimesema, nisiyoyatambua, mastaajabu kama hayo yananishinda, siyajui.[#Iy. 38:2; Fano. 28:13; 1 Yoh. 1:9.]
4Sikiliza, niseme nami! Nitakuuliza, unijulishe![#Iy. 38:3.]
5Kusikia naliyasikia mambo yako kwa masikio yangu, lakini sasa macho yangu yamekuona.
6Kwa hiyo nayatangua mwenyewe, niliyoyasema, humu mavumbini na majivuni ninajuta.
7Ikawa, Bwana alipokwisha kumwambia Iyobu maneno haya, Bwana akamwambia Elifazi wa Temani: Makali yangu yamekuwakia wewe na wenzako hawa wawili, kwani maneno, mliyoyasema kuwa yangu, hayakunyoka kama yale ya mtumishi wangu Iyobu.
8Sasa jichukulieni ng'ombe waume saba na kondoo waume saba, mwende kwa mtumishi wangu Iyobu, mwatoe kuwa ng'ombe za tambiko zenu ninyi, naye mtumishi wangu Iyobu na awaombee; kwani kwa kumpendelea yeye nitaacha kuwafanyizia ninyi yaupasayo ujinga wenu, kwani maneno, mliyoyasema kuwa yangu, hayakunyoka kama yale ya mtumishi wangu Iyobu.[#Ez. 14:14.]
9Ndipo, Elifazi wa Temani na Bildadi wa Sua na Sofari wa Nama walipokwenda, wakafanya, kama Bwana alivyowaambia, naye Bwana akampendelea Iyobu.
10Kisha Bwana akayafungua mafungo ya Iyobu, alipowaombea wenzake; nayo yote, Iyobu aliyokuwa nayo, Bwana akayarudisha na kuyaongeza, akayapata yale ya kale mara mbili.[#Iy. 8:7.]
11Wakaja kwake ndugu zake wote wa kiume na wa kike nao waliojuana naye kale, wakala naye chakula nyumbani mwake, wakampongeza na kumtuliza moyo kwa ajili ya hayo mabaya yote, Bwana aliyokuwa alimletea, wakampa kila mtu kipande cha fedha na pete ya dhahabu.
12Hivyo Bwana akambariki Iyobu, mwisho wake utukuke kuliko mwanzo, akapata kondoo na mbuzi 14000 na ngamia 6000 na majozi 1000 ya ng'ombe na majike ya punda 1000.
13Akapata tena wana saba wa kiume na watatu wa kike.
14Hao akawaita majina yao, wa kwanza Yemima (Hua), wa pili Kesia (Marashi), wa tatu Kereni-Hapuki (Pembe ya Wanja).
15Hawakuonekana wanawake katika nchi yote nzima waliokuwa wazuri kama hao mabinti Iyobu. Naye baba yao akawapa mafungu, yawe yao, kama waumbu zao.[#4 Mose 27:8-11.]
16Hayo yote yalipokwisha, Iyobu akawapo miaka 140, akaona wana na wajukuu, vizazi vinne.
17Kisha Iyobu akafa alipokuwa mzee mwenye miaka mingi ya kumtosha.[#1 Mose 25:8.]