Iyobu 8

Iyobu 8

Bildadi anasema: Ajutaye huona mema; wasiomcha Mungu huangamia. Bildadi wa Sua akajibu akisema:

1Kama hayo utayasema hata lini?

2Maneno ya kinywa chako yatavuma hata lini yakiwa kama upepo wa kimbunga?

3Je? Yako maamuzi, Mungu anayoyapotoa? Au yako yanyokayo, Mwenyezi anayoyapotoa?[#Iy. 34:10.]

4Kwa kuwa wanao walimkosea, amewatwika maovu yao.[#Iy. 1:18-19.]

5Lakini wewe ukimtafuta Mungu mapema na kumlalamikia Mwenyezi,

6ukiwa umetakata, ukanyoka, kweli ataamka sasa hivi, aje kwako, alitengemanishe kao lako, wongofu wako ukae humo;[#Sh. 35:23.]

7ndipo, mali zako za kwanza zitakapokuwa chache, maana zako za mwisho zitazidi kuwa nyingi mno.[#Iy. 42:10.]

8Walio wa kizazi cha kale waulize wao, kajishikize kwa mambo ya baba zao, waliyoyachunguza!

9Kwani sisi tu wa jana tu, hatujui neno, kwani siku zetu ni kama kivuli kipitacho katika nchi.[#Sh. 102:12.]

10Hao sio watakaoweza kukufunza wakikuelezea mambo, wakitoa mioyoni mwao watakayokuambia?

11Je? Pasipokuwa penye unyevu huotesha matete? Pasipokuwa penye maji huchipuza mafunjo?

12Siku za kuyakata zitakapotimia, yako majani ya kwanza tu; majani mengine yakiwa mabichi bado, yale yamekwisha kukauka.

13Hivyo ndivyo, zilivyo njia zao wale waliomsahau Mungu, ndivyo, kinavyoangamia kingojeo cha mpotovu.[#Iy. 11:20; 18:14; Fano. 10:28.]

14Kwani egemeo lake litavunjika, nalo kimbilio lake ni tando la buibui.

15Akijiegemeza penye nyumba yake, haisimani, akiishika kwa nguvu, haikai.

16Naye akiwa mwenye utomvu mwingi, ijapo jua liwe kali, nayo machipukizi yake yakilieneza shamba lake,

17mizizi yake ikizinga nazo chungu za mawe, ikijiingiza kwa nguvu zao namo maweni penye nyumba:

18lakini wakimng'oa mahali pake, alipokuwa, ndipo, hapo pake patakapomkana kwamba: Sijakuona.

19Tazama! Hii ndiyo furaha, njia yake inayompatia, kisha wataota wengine hapo uvumbini, alipokuwa.

20Utaona, Mungu hamtupi mtu asiyekosa, lakini wafanyao mabaya hawashiki mikono.

21Kweli kinywa chako atakijaza vicheko, midomo yako nayo na ishangilie.[#Sh. 126:2.]

22Lakini watakaoiva nyuso kwa soni ndio wachukivu wako, nayo mahema yao wasiomcha Mungu yatakuwa hayako.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania