Iyobu 9

Iyobu 9

Jibu la pili la Iyobu: Hakuna awezaye kubishana na Mungu.

1Iyobu akajibu akisema: Najua, hii ni kweli; ndivyo, vilivyo kweli:[#Iy. 25:4.]

2Sisi watu hakuna aliye mwongofu mbele yake Mungu.

3Kama anataka kuulizana na mtu, akimwuliza maneno elfu, moja tu hawezi kumjibu.[#Sh. 19:13.]

4Moyo wake ni wenye werevu wa kweli, naye ni mwenye nguvu nyingi, yuko nani aliyejishupaza kushindana naye, akapona?

5Aondoa milima na kuiweka pengine, isivijue, makali yake yakiwaka, anaifudikiza.

6Anaitetemesha nchi, itoweke mahali pake, nayo mashikizo yake yatikisike sana.

7Akiliagiza jua, halichi, nazo nyota anazifunga na kuzitia muhuri.

8Yeye peke yake ndiye anayezitanda mbingu, anatembea na kuyakanyaga mawimbi ya bahari.[#Yes. 40:22.]

9Yeye ndiye aliyezitengeneza nyota, kama za Gari nazo za Choma, nikuchome, hata za Kilimia, nazo zile za mifanofano iliyoko upande wa kusini.[#Iy. 38:31; Yes. 13:10; Amo. 5:8.]

10Hufanya mambo makuu yasiyochunguzika, navyo vioja vyake havihesabiki.[#Iy. 5:9.]

11Tazama! Akinikaribia na kujiendea tena, simwoni, wala simtambui, akipita.

12Tazama! Yuko nani awezaye kumrudisha nyuma, akipokonya? Yuko nani awezaye kumwuliza: Unafanya nini?

13Kwa kuwa Mungu haachi kukasirika, nao wanaosaidiana na nondo wa baharini hawana budi kumwangukia.[#Iy. 26:12.]

14Sembuse mimi nitawezaje kumjibu lo lote? Mbele yake nitawezaje kuchagua maneno yafaayo?

15Ingawa niwe sikukosa, nisingemjibu, ila kwa kuwa ni mwamuzi wangu, ningemlalamikia tu.

16Kama ningemwita, akaniitikia, nisingemtegemea kwamba: Ataisikia sauti yangu.

17Kwa kunijia na nguvu za chamchela yeye ameniponda, akanitia vidonda vingi zaidi pasipo kosa langu lo lote.

18Tena haniachi kabisa, nipate kutoa pumzi tu, kwani machungu ndiyo, anayonishibisha.

19Kama ninatazamia nguvu, nimekwisha kumwona, anavyoshupaa; kama ninatazamia kupiga shauri, yuko nani atakayenishuhudia?[#Iy. 9:33.]

20Ingawa niwe mwenye wongofu, kinywa changu kingeniponza; kingenitokeza kuwa mpotovu, ingawa niwe sikukosa.

21Mimi ni mtu asiyekosa. Kuzimia kwa roho yangu nakuwazia kuwa si kitu, huku kuwapo kwangu kunanichukiza.

22Yote ni mamoja; kwa hiyo nasema: Wasiokosa nao wasiomcha yeye huwaangamiza wote.[#Iy. 8:20; Mbiu. 9:2-3.]

23Akiwapatia watu mapigo ya kuwaua kwa mara moja, huwasimanga nao wasiokora manza, wakiyeyuka.

24Nchi hii imetiwa mikononi mwao wasiomcha Mungu, naye huzifunika nyuso zao waamuzi wake; kama siye yeye mwenyewe mwingine yuko wapi?

25Nazo siku zangu hupita upesi sana kuliko mpiga mbio, ijapo, hazikuona mema hujikimbilia.

26Zimepita upesi kama mitumbwi ya matete, zinafanana na tai, akiangukia chakula.

27Ikiwa, niseme: Na nivisahau hivi vinavyoniliza, na niache kununa usoni, nichangamke,

28maumivu yangu yote hunistusha, kwani najua: hutanitokeza kabisa kuwa mtu asiyekosa.

29Basi, kwa kuwa mimi nitatokezwa kuwa mtu asiyemcha Mungu, nijichokeshe bure tena, nipate nini?

30Ingawa ningejitawaza kwa maji ya theluji, au ningeinawa mikono yangu kwa sabuni,

31hapo napo ungenichovya shimoni mwenye machafu, nguo zangu mwenyewe zinitapishe.

32Kwani Mungu si mtu kama mimi, nimjibu, tukaja kukutana shaurini kuamuliwa.

33Kwetu sisi, yeye na mimi, hakuna awezaye kutuamua, akitushika sote wawili kwa mkono wake.

34Na aiondoe fimbo yake, isinipige, vitisho vyake visinistushe!

35Ndipo, nitakaposema pasipo kumwogopa, kwani hivyo sivyo, mimi nionavyo moyoni mwangu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania