Yosua 14

Yosua 14

Nchi ya Kanaani inagawanywa.

1Hizi ndizo nchi, wana wa Isiraeli walizozipata katika nchi ya Kanaani kuwa mafungu yao; nao waliowagawanyia haya mafungu ni mtambikaji Elazari na Yosua, mwana wa Nuni, pamoja na wakuu wa baba za mashina ya wana wa Isiraeli.[#4 Mose 34:17.]

2Waliyapata mafungu yao kwa kuyapigia kura, kama Bwana alivyoviagiza kinywani mwa Mose kwa ajili ya hayo mashina tisa na nusu ya Manase.[#4 Mose 26:55.]

3Kwani yale mashina mawili na nusu ya lile shina moja Mose aliwapa mafugu yao ng'ambo ya huko ya Yordani, lakini Walawi hakuwapa fungu katikati yao.[#Yos. 13:14-33.]

4Kwani wana wa Yosefu walikuwa mashina mawili: Manase na Efuraimu, lakini Walawi hawakuwapa fungu katika nchi yao, walipata miji tu ya kukaa pamoja na malisho yao ya kulisha nyama wao wa kufuga na mahali pa kuwekea mapato yao.[#Yos. 21.]

5Kama Bwana alivyomwagiza Mose, ndivyo, wana wa Isiraeli walivyovifanya walipojigawanyia nchi hiyo.

Fungu la Kalebu.

6Hapo, wana wa Yuda walipofika kwake Yosua kule Gilgali, Mkenizi Kalebu, mwana wa Yefune, akamwambia: Wewe unalijua lile neno, Mungu alilolisema kule Kadesi-Barnea kwa ajili yangu na kwa ajili yako.[#4 Mose 14:24; 5 Mose 1:36.]

7Mimi nilikuwa mwenye miaka 40, Mose, mtumishi wa Bwana, aliponituma kule Kadesi-Barnea kwenda kuipeleleza nchi hii, nami nikamletea habari za mambo ya huku, kama nilivyoyaona moyoni mwangu.[#4 Mose 13:6,30.]

8Lakini ndugu zangu waliopanda pamoja nami wakaiyeyusha mioyo ya watu hawa, lakini mimi nilijishupaza kabisa kumfuata Bwana Mungu wangu.[#4 Mose 13:31.]

9Siku hiyo Mose akaapa kwamba: Nchi hiyo, miguu yako iliyoikanyaga, itakuwa fungu lako, iwe yako na ya wanao kale na kale, kwa kuwa umejishupaza kabisa kumfuata Bwana Mungu wangu.

10Sasa tazama, Bwana amenikalisha uzimani, kama alivyosema, tangu hapo, alipomwambia Mose lile neno, miaka hii 45, Waisiraeli waliyoitembea nyikani, sasa leo hivi unaniona kuwa mwenye miaka 85.

11Na leo ningaliko mwenye nguvu kama siku hiyo, Mose aliponituma; nguvu zangu kama zilivyokuwa hapo, ndivyo, hizo nguvu zangu zilivyo na leo za kupiga vita, nipate kwenda na kurudi.[#5 Mose 34:7.]

12Sasa nipe milima hiyo, Bwana aliyoitaja siku hiyo. Kwani mwenyewe ulisikia siku hiyo, ya kuwa wako Waanaki, ya kuwa iko nayo miji mikubwa yenye maboma. Labda Bwana atakuwa pamoja na mimi, nipate kuwafukuza, kama Bwana alivyosema.[#Yos. 11:21.]

13Ndipo, Yosua alipombariki Kalebu, mwana wa Yefune, akampa Heburoni, uwe fungu lake.[#Yos. 15:13-19; 21:11-12.]

14Kwa hiyo Heburoni ukawa wake Mkenizi Kalebu, mwana wa Yefune, uwe fungu lake mpaka siku hii ya leo, kwa kuwa alijishupaza kabisa kumfuata Bwana Mungu wa Isiraeli.

15Kale jina lake Heburoni lilikuwa mji wa Arba aliyekuwa mkubwa kuwapita Waanaki wote. Siku zile nchi hii ikapata kutengemana, kwa kuwa vita vilikoma.[#Yos. 11:23.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania