The chat will start when you send the first message.
1Wana wa Yosefu kura ikawapatia nchi toka Yordani karibu ya Yeriko, nao mpaka wa maawioni kwa jua ulikuwa yale maji ya Yeriko, ulichukua nayo nyika inayopanda kutoka Yeriko mpaka mlimani kwa Beteli.
2Mpaka ulipotoka Beteli ulifika Luzi, tena uliendelea, ufike mpakani kwa Waarki hata Ataroti.
3Toka huko ulitelemka upande wa baharini kuufikia mpaka wa Wayafuleti hata mpaka wa Beti-Horoni wa chini mpaka Gezeri; mwisho ulitokea baharini.
4Wana wa Yosefu, Manase na Efuraimu, wakazipata nchi hizi, ziwe mafungu yao.
5Nchi, wana wa Efuraimu walizozipata za kuzigawanyia koo zao, mipaka yao ni hii: mpaka wa fungu lao wa maawioni kwa jua ulianzia Ataroti-Adari, ulifika Beti-Horoni wa juu.
6Toka huko mpaka ulikwenda kufika baharini. Upande wa kaskazini mpaka ulianzia Mikimetati, ulizunguka kwenda upande wa maawioni kwa jua, ufike Tanati-Silo, kisha ulipitia Yonoha upande wake wa maawioni kwa jua.
7Toka Yanoha ulitelemka kufika Ataroti na Nara, kisha uligusa Yeriko na kutokea Yordani.
8Tena kutoka Tapua mpaka ulikwenda upande wa baharini, ufike kwenye mto wa Kana, kisha ulitokea baharini. Nchi hizi zilikuwa fungu la shina la wana wa Efuraimu la kuzigawanyia koo zao.
9Tena wana wa Efuraimu walikuwa na miji waliyowekewa katikati ya fungu la wana wa Manase, nayo miji hiyo ilikuwa pamoja na mitaa yao.[#Yos. 17:9.]
10Lakini hawakuwafukuza Wakanaani waliokaa Gezeri; kwa hiyo Wakanaani wakakaa katikati ya Waefuraimu mpaka siku hii ya leo, lakini hawakuwa na budi kuwafanyizia kazi za kitumwa[#1 Fal. 9:16.]