The chat will start when you send the first message.
1Bwana, yakumbuke yaliyotupata!
Tazama, uone, jinsi tunavyotiwa soni!
2Mafungu yetu ya nchi yamechukuliwa, yawe mali za wengine,
nyumba zetu zinakaa wageni.
3Tumegeuka kuwa wana waliofiwa na baba zao,
mama zetu ni kama wajane.
4Maji yetu tunayanywa tukiyanunua kwa fedha,
kuni zetu nazo tunazipata tu tukizilipa.
5Watukimbizao wako penye shingo zetu;
tunapochoka hatuoni pa kupumzika.
6Wamisri na Waasuri tukawanyoshea mikono,
tupate vyakula vya kushiba.
7Baba zetu waliokosa hawako tena,
nasi tunatwikwa manza, walizozikora wao.
8Watumwa ndio wanaotutawala,
lakini hakuna anayetupokonya mikononi mwao.
9Tunaziponza roho zetu tukijichumia vyakula,
kwa kuwa nako nyikani ziko panga.
10Ngozi zetu ni zenye moto kama wa tanuru
kwa kuteketezwa na njaa.
11Wanawake waliokuwamo Sioni waliwakorofisha,
nao wasichana waliokuwako katika nchi za Yuda.
12Wakuu wakanyongwa kwa mikono yao,
nazo nyuso za wazee hazikupewa macheo.
13Vijana hutwikwa majiwe ya kusagia,
watoto huvunjwa na mizigo ya kuni.
14Ndipo, wazee walipoyaacha maongezi ya malangoni,
nao vijana wakayakomesha mazeze yao.
15Yakakoma yaliyoifurahisha mioyo yetu,
michezo yetu ya ngoma ikageuka kuwa maombolezo.
16Vilemba vilivyovipamba vichwa vyetu vimekwisha kuanguka chini,
tukapatwa na mabaya, kwa kuwa tumekosa.
17Kwa hiyo mioyo yetu imezimia,
kwa hiyo macho yetu nayo yameguiwa na giza.
18Ni kwa ajili ya mlima wa Sioni ulioko peke yake,
kwa kuwa ni mbweha tu wanaotembea huko.
19Wewe Bwana, unakaa kale na kale,
kiti chako cha kifalme kiko kwa vizazi na vizazi!
20Mbona unatusahau kale na kale,
ukatuacha siku hizi zilizo nyingi?
21Bwana, turudishe kwako! Ndivyo, tutakavyopata kurudi;
siku zetu zigeuke kuwa mpya tena kama zile zilizopita!
22Kweli umetutupa kabisa,
umetukasirikia sanasana.