3 Mose 1

3 Mose 1

Ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima.

1Bwana akamwita Mose, akasema naye toka Hemani mwa Mkutano kwamba:

2Waambie wana wa Isiraeli na kuwaagiza hivyo: Mtu wa kwenu akitaka kumpelekea Bwana matoleo ya nyama wa kufuga sharti hayo matoleo yenu myatoe katika ng'ombe au katika mbuzi na kondoo.

3Kama toleo lake ni ng'ombe, anayemtoa kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, sharti atoe dume asiye na kilema, ampeleke pa kuliingilia Hema la Mkutano, Bwana apate kupendezwa naye.[#3 Mose 17:4.]

4Kisha aubandike mkono wake kichwani pake hiyo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, impatie upendezo wa kupozwa kwake.[#2 Mose 29:10.]

5Kisha amchinje huyo mwana wa ng'ombe mbele ya Bwana, nao wana wa Haroni walio watambikaji na waipeleke damu, nayo hiyo damu wainyunyize pande zote juu ya meza ya kutambikia iliyopo hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano.

6Kisha aichune hiyo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima na kuichangua.

7Kisha wana wa Haroni walio watambikaji watie moto hapo pa kutambikia na kupanga kuni juu ya moto.

8Kisha wana wa Haroni walio watambikaji na wavipange vile vipande vya nyama, hata kichwa na mafuta juu ya kuni zilizopangwa juu ya moto uliowashwa mezani pa kutambikia.

9Lakini matumbo na miguu yake na aioshe kwa maji, kisha mtambikaji atayachoma moto yote yaliyowekwa juu ya meza ya kutambikia. Ndivyo, ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima inavyotolewa, iwe moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana.[#1 Mose 8:21.]

10Kama toleo lake, analolitoa kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ni nyama mdogo kama kondoo au mbuzi sharti apeleke dume asiye na kilema.

11Amchinje mbele ya Bwana kando ya meza ya kutambikia upande wake wa kaskazini, nayo damu yake wana wa Haroni walio watambikaji na wainyunyize pande zote juu ya meza ya kutambikia.

12Kisha amchangue, naye mtambikaji avipange vipande vyake pamoja na kichwa chake na mafuta yake juu ya moto uliowashwa mezani pa kutambikia.

13Lakini matumbo na miguu na aioshe kwa maji, kisha mtambikaji atayatoa yote kwa kuyachoma moto yote yaliyowekwa juu ya meza ya kutambikia. Ndivyo, naye nyama mdogo anavyokuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana.

14Kama toleo lake, analomtolea Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ni ndege, basi, sharti apeleke hua au kinda la njiwa manga.

15Naye mtambikaji atampeleka mezani pa kutambikia, atamvunja kichwa chake, apate kumchoma moto mezani pa kutambikia, lakini damu yake sharti idondoke ukutani pake meza ya kutambikia.

16Kisha akiondoe kibofu chake cha koo pamoja na machafu yaliyomo, akitupe majivuni kando ya meza ya kutambikia upande wa maawioni kwa jua.

17Kisha ampasue kidogo mabawani, lakini asiyatenge! Kisha mtambikaji amchome moto mezani pa kutambikia juu ya kuni zilizowekwa juu ya moto. Ndivyo, naye ndege anavyokuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, ndio moto wenye mnuko wa kumpendeza Bwana.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania