3 Mose 13

3 Mose 13

Jinsi ukoma wa mtu unavyojulikana.

1Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba:[#5 Mose 24:8.]

2Ngozi ya mwili wa mtu ikitoa kivimbe au kipele au balanga, hiyo ngozi ya mwili wake ikitaka kumpatia pigo la ukoma, na apelekwe kwa mtambikaji Haroni au kwa mmoja wao wanawe walio watambikaji.

3Mtambikaji akilitazama hilo doa la ngozi ya mwili, akiona, ya kuwa nywele penye hilo doa zimegeuka kuwa nyeupe, tena hilo doa likionekana kuwa linabonyea katika ngozi nyingine ya mwili, basi, ndio doa la ukoma; mtambikaji akiisha kumwona kuwa hivyo hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu.[#3 Mose 14:37.]

4Lakini hilo balanga jeupe penye ngozi ya mwili wake lisipoonekana, ya kuwa linabonyea katika ngozi, tena nywele zikiwa hazikugeuka kuwa nyeupe, mtambikaji atamfungia mwenye doa hilo siku saba.

5Siku ya saba mtambikaji atamtazama tena. Atakapoona kwa macho yake, ya kama hilo doa ni lilelile, ya kama hilo doa halikuongezeka katika ngozi, mtambikaji na amfungie mara ya pili siku saba.

6Mtambikaji akimtazama mara ya pili siku ya saba, akiona, ya kama hilo doa limo katika kufifia, ya kama hilo doa halikuongezeka katika ngozi, basi, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ametakata kwa kuwa ni mba tu, kisha mwenyewe na azifue nguo zake; ndipo, atakapokuwa ametakata.

7Lakini hiyo mba ikiongezeka katika ngozi, mtambikaji alipokwisha kumtazama na kusema, ya kuwa ametakata, sharti amtokee mtambikaji mara ya pili.

8Mtambikaji atakapomtazama tena na kuona, ya kama hiyo mba imeongezeka mwilini, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu, kwa kuwa ni ukoma.

9Mtu akiwa mwenye pigo la ukoma sharti apelekwe kwa mtambikaji.

10Mtambikaji akimtazama akiona kivimbe cheupe penye ngozi, akiona tena, ya kama hapo nywele zimegeuka kuwa nyeupe, akiona tena, ya kama nyama mbichi zimeota nyingi ndani ya kile kivimbe,

11basi, ndio ukoma wa kale hapo penye ngozi ya mwili wake, naye mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu pasipo kufungia, kwani ni mwenye uchafu kweli.

12Lakini ukoma ukitokea na kuenea katika ngozi po pote, ukoma ukiifunika hiyo ngozi iliyopatwa nao toka kichwani pake huyo mtu mpaka miguuni pake pote, macho ya mtambikaji yanapotazama,

13basi, mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama ukoma umeufunika mwili wake wote pia, hana budi kusema, ya kama mtu huyo aliyepatwa hivyo ni mwenye kutakata; kwa kugeuka wote mzima kuwa mweupe amekwisha kutakata.

14Lakini siku hiyo, nyama mbichi itakapoonekana kwake atakuwa mwenye uchafu.

15Naye mtambikaji akiiona hiyo nyama mbichi hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu; kwa kuwa hiyo nyama mbichi ni yenye uchafu, ndio ukoma.

16Lakini hiyo nyama mbichi ikigeuka tena kuwa nyeupe, na afike kwa mtambikaji.

17Mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama hapo palipopatwa na ukoma pamegeuka kuwa peupe, mtambikaji hana budi kusema, ya kama huyu aliyepatwa na ukoma ametakata, kwa kuwa amekwisha kutakata kweli.

18Mwili wa mtu ukiwa wenye jipu penye ngozi yake, nalo likipona,

19tena hapo, lile jipu lilipokuwa, pakitokea kivimbe cheupe au balanga jeupe lenye damudamu, sharti amtokee mtambikaji kutazamwa.

20Mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama hapo panaonekana kuwa panabonyea katika ngozi, tena ya kama nywele zimegeuka kuwa nyeupe, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu, ndio ugonjwa wa ukoma uliotokea hapo penye jipu.

21Lakini mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama nywele hazikugeuka kuwa nyeupe, tena hapakubonyea katika ngozi, ila panaanza kufifia, mtambikaji na amfungie siku saba.

22Basi, mahali pale pakiendelea katika ngozi, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu, kwani ndio ugonjwa ule mbaya.

23Lakini hilo balanga likiwa lilelile hapo mahali pake, lisiendelee, basi, ndio kovu la jipu tu, naye mtambikaji hana budi kusema, ya kama ametakata.[#3 Mose 13:28.]

24Mwili wa mtu ukiwa wenye kidonda cha moto penye ngozi yake, nazo nyama za humo kidondani zikiwa balanga jeupe lenye damudamu au jeupe lenyewe,

25mtambikaji hana budi kupatazama; akiona, ya kama nywele zimegeuka kuwa nyeupe penye hilo balanga, napo pakionekana kuwa panabonyea katika ngozi, ndio ukoma uliotokea katika kidonda cha moto, naye mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu, kwani ndio ugonjwa wa ukoma.

26Lakini mtambikaji akipatazama na kuona, ya kama hapo penye balanga hapana nywele nyeupe, wala hapakubonyea katika ngozi, napo panaanza kufifia, mtambikaji na amfungie siku saba.

27Mtambikaji atakapomwona siku ya saba, ya kuwa mahali hapo pameendelea katika ngozi, mtambikaji hana budi kusema, ya kuwa ni mwenye uchafu, kwani ndio ugonjwa wa ukoma.

28Lakini kama hilo balanga ni lilelile mahali pake, halikuendelea katika ngozi, ila limeanza kufifia basi, ndio kivimbe cha kidonda cha moto tu, naye mtambikaji hana budi kusema, ya kama ametakata, kwani ni kovu tu la kidonda cha moto.[#3 Mose 13:23.]

29Tena mtu mume au mke akitoka upele kichwani au kidevuni,

30mtambikaji akiutazama huo upele na kuona, ya kama unaonekana kuwa unabonyea katika ngozi, ya kama nazo nywele za hapo ni nyekundu kidogo, tena ni nyembamba, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu, kwani ndio upele mbaya, maana ukoma wa kichwani na wa kidevuni.

31Lakini mtambikaji akiutazama ugonjwa huo wa upele mbaya na kuona, ya kama hapaonekani kuwa panabonyea katika ngozi, tena ya kama hapana nywele zilizo nyekundu kidogo, mtambikaji na amfungie siku saba huyo mwenye ugonjwa wa upele mbaya.

32Mtambikaji atakapomtazama huyu mgonjwa siku ya saba na kuona, ya kama huo upele mbaya haukuendelea, wala hapana nywele zilizo nyekundu kidogo, wala upele huo mbaya hauonekani kuwa unabonyea katika ngozi,

33na ajinyoe nywele, lakini hapo penye upele mbaya asipanyoe; kisha mtambikaji na amfungie huyu mwenye upele mbaya mara ya pili siku saba.

34Mtambikaji atakapomtazama tena huyu mwenye upele mbaya siku ya saba na kuona, ya kama huo upele mbaya haukuendelea katika ngozi, wala hauonekani kuwa unabonyea katika ngozi, mtambikaji hana budi kusema, ya kama ametakata, naye na azifue nguo zake, kisha atakuwa ametakata kweli.

35Lakini upele mbaya ukiendelea katika ngozi, mtambikaji alipokwisha kusema, ya kama ametakata,

36naye akimtazama tena na kuona, ya kama upele mbaya umeendelea katika ngozi, mtambikaji asitafute nywele zilizo nyekundu kidogo, kwani mtu yule ni mwenye uchafu.

37Lakini akiona kwa macho yake, ya kuwa upele mbaya ni uleule, ya kuwa nywele nyeusi zimeota hapo, basi, upele mbaya umepona, naye mwenyewe ametakata, naye mtambikaji hana budi kusema ya kama ametakata.

38Mtu mume au mke akiwa mwenye mabalanga penye ngozi ya mwili wake, hayo mabalanga yakiwa meupe,

39naye mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama penye ngozi ya mwili wake yako mabalanga meupe yaliyoanza kufifia, ndio mba zilizotoka katika ngozi, naye mwenyewe ni mwenye kutakata.

40Kama nywele za mtu zimeng'oka kichwani pake, ni mwenye kipara cha kisogoni, ni mwenye kutakata.

41Kama nywele za upande wa usoni zimeng'oka kichwani pake, ni mwenye kipara cha paji la usoni, naye ni mwenye kutakata.

42Lakini penye kipara cha kisogoni au cha utosini pakitokea vipele vyeupe vyenye damudamu, ndio ukoma unaotoka penye kipara chake cha kisogoni au cha utosini.

43Mtambikaji akimtazama na kuona, ya kama ni kivimbe cha vipele vyeupe vyenye damudamu penye kipara chake cha kisogoni au cha utosini kinachoonekana kuwa kama ukoma penye ngozi ya mwili,

44basi, ni mtu mwenye ukoma, naye ni mwenye uchafu, naye mtambikaji hana budi kusema, ya kama ni mwenye uchafu kweli, nao huo ugonjwa wake mbaya uko kichwani pake.

45Mwenye ukoma aliyepatwa na ugonjwa huu mbaya nguo zake sharti ziraruliwe, nazo nywele za kichwani pake sharti ziachwe wazi, nazo ndevu za midomoni sharti azifunike na kuita: Mchafu! Mchafu!

46Siku zote, atakazokuwa na ugonjwa huu mbaya atakuwa mwenye uchafu wa kweli, sharti akae peke yake, nalo kao lake sharti liwe nje ya makambi.[#4 Mose 5:3.]

Ukoma wa mavazi.

47Tena uko ukoma wa mavazi: vazi kama ni la nywele za kondoo au la pamba, linaweza kupatwa na ugonjwa huu mbaya wa ukoma;

48nguo yake ikiwa imefumwa au ikiwa imesokotwa na kushonwa, kama ni ya pamba au ya nywele za kondoo, kama ni ngozi yenyewe au ngozi iliyotengenezwa kwa namna yo yote,

49zote pia hupatwa na ukoma: madoadoa ya kimajanijani au ya damudamu yakitoka katika nguo au katika ngozi au katika nyuzi za kufumwa au katika nyuzi za kusokotwa au katika chombo cho chote kilichotengenezwa kwa ngozi, ndio huo ugonjwa mbaya wa ukoma; kwa hiyo sharti utazamwe na mtambikaji.

50Mtambikaji akiutazama huo ugonjwa mbaya, sharti hicho kilichopatwa nacho akifungie siku saba.

51Atakapokitazama siku ya saba hicho kilichopatwa na huu ugonjwa mbaya na kuona, ya kama ugonjwa huu mbaya umeendelea katika nguo au katika nyuzi za kufumwa au katika nyuzi za kusokotwa au katika ngozi, ijapo hiyo ngozi iwe imetengenezewa kazi yo yote, basi, ugonjwa huu mbaya ndio ukoma unaokula, nacho kile kitu ni chenye uchafu.

52Sharti waziteketeze hizo nguo au hizo nyuzi za kufumwa au hizo nyuzi za kusokotwa, kama ni za nywele za kondoo au za pamba, navyo vyo vyote vilivyotengenezwa kwa ngozi vilivyo vyenye ugonjwa huo mbaya, kwani ndio ukoma unaokula; kwa hiyo sharti viteketezwe kwa moto.

53Lakini mtambikaji akivitazama na kuona, ya kama ugonjwa huo mbaya haukuendelea katika nguo au katika nyuzi za kufumwa au katika nyuzi za kusokotwa au katika chombo cho chote cha ngozi,

54mtambikaji na aagize, wavifue vilivyo vyenye ugonjwa huo mbaya, kisha avifungie mara ya pili siku saba.

55Mtambikaji atakapovitazama vilivyopatwa na ugonjwa huo mbaya, vikiisha kufuliwa, na kuona, ya kama hapo penye ugonjwa huo mbaya hapakugeuka kuwa namna nyingine, ijapo ugonjwa wenyewe uwe haukuendelea, basi, ni vichafu, sharti waviteketeze kwa moto, kwani mahali hapo panabonyea upande wa nyuma na wa mbele.

56Lakini mtambikaji akipatazama na kuona, ya kama hapo penye ugonjwa huo mbaya pameanza kufifia, vile vitu vilipofuliwa, basi, na apaondoe katika nguo au katika ngozi au katika nyuzi za kufumwa au katika nyuzi za kusokotwa.

57Lakini ugonjwa huo ukionekana tena katika hizo nguo au katika hizo nyuzi za kufumwa au katika hizo nyuzi za kusokotwa au katika hivyo vyombo vyo vyote vya ngozi, kama unatokea humo tena, na wavichome moto vilivyopatwa na ugonjwa huo mbaya.

58Lakini hizo nguo au hizo nyuzi za kufumwa au hizo nyuzi za kusokotwa au hivyo vyombo vyo vyote vya ngozi vilivyotokwa na ugonjwa huo mbaya vilipofuliwa na vifuliwe mara ya pili; ndipo, vitakapokuwa vimetakata.

59Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya ugonjwa mbaya wa ukoma, ukishika nguo, kama ni za nywele za kondoo au za pamba, au nyuzi za kufumwa au nyuzi za kusokotwa au vyombo vyo vyote vya ngozi, wapate kusema, ya kama ni vyenye kutakata au vyenye uchafu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania