3 Mose 15

3 Mose 15

Uchafu wa mwili.

1Bwana akamwambia Mose na Haroni kwamba:[#4 Mose 5:2.]

2Semeni na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Mtu mume ye yote akiwa mwenye kisonono mwilini mwake ni mwenye uchafu kwa ajili ya hicho kisonono chake.

3Nao uchafu, anaoupata kwa kisonono chake, ni wa namna hii: kama mwili wake unachuruzika usaha wa kisonono chake, au kama mwili wake unaukomeshakomesha, uchafu ni uo huo.

4Kilalo cho chote, mwenye kisonono atakachokilalia, ni chenye uchafu.

5Naye mtu atakayekigusa kilalo chake sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

6Naye atakayekalia kitu, mwenye kisonono alichokikalia, sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

7Naye atakayeugusa mwili wake mwenye kisonono sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

8Naye mwenye kisonono akitemea mate mwenye kutakata, huyo sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

9Nayo matandiko yo yote, mwenye kisonono atakayoyakalia akipanda, yatakuwa yenye uchafu.

10Naye kila atakayegusa cho chote kilichokuwa chini yake atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni, naye atakayevichukua vilivyo hivyo sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

11Naye kila mtu, mwenye kisonono atakayemgusa pasipo kunawa kwanza mikono yake kwa maji, sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

12Nacho chombo cha udongo, mwenye kisonono atakachokigusa, sharti kivunjwe, nacho kila chombo cha mti sharti kioshwe majini.[#3 Mose 11:33.]

13Lakini mwenye kisonono akipata kutakata, kwa kuwa kisonono chake kimekoma, sharti ahesabu siku saba kuanzia hapo, alipopata kutakata, kisha sharti azifue nguo zake pamoja na koga katika maji ya mtoni; ndipo, atakapokuwa mwenye kutakata.

14Siku ya nane na achukue hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga, amtokee Bwana hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano, ndipo ampe mtambikaji wale ndege.[#3 Mose 5:7.]

15Naye mtambikaji na awatengeneze, mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, wa pili kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi mbele ya Bwana kwa ajili ya kisonono chake.

16Lakini mtu akitokwa na mbegu akilala sharti auogeshe mwili wake wote mzima majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.[#3 Mose 22:4.]

17Nazo nguo zote na ngozi zote zilizonyewa na hizo mbegu sharti zifuliwe majini, nazo zitakuwa zenye uchafu mpaka jioni.

18Tena mtu aliye hivyo akilala na mwanamke, sharti wote wawili na waoge majini, kisha watakuwa wenye uchafu mpaka jioni.

19Mwanamke akiingia miezini, atokwe na damu mwilini mwake, sharti atengwe siku saba, naye kila atakayemgusa atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.[#3 Mose 18:19.]

20Nayo yote, atakayoyalalia siku hizo za kutengwa kwake, yatakuwa yenye uchafu; nayo yote, atakayoyakalia, yatakuwa yenye uchafu.

21Naye kila atakayekigusa kilalo chake sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

22Naye kila atakayegusa cho chote, alichokikalia, sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

23Naye atakayegusa cho chote kilichoko juu ya kilalo chake au juu ya kitu, alichokikalia, atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

24Tena mtu akilala naye, akiwa miezini, atakuwa mwenye uchafu siku saba, hata kilalo chake, atakachokilalia, kitakuwa chenye uchafu.

25Mwanamke akitoka damu zake siku nyingi zisizo zake za kuwa miezini, au kama anatoka damu kuzipita hizo siku za kuwa miezini, basi siku zote za kutoka damu ni mwenye uchafu; kama alivyo akiwa miezini, ndivyo, mwenye uchafu alivyo siku hizo nazo.

26Kilalo cho chote, atakachokilalia siku zote za kutoka damu zake, ni chenye uchafu, kama kilalo chake cha kuwa miezini kilivyo chenye uchafu; nacho kitu cho chote, atakachokikalia, ni chenye uchafu, kama kilivyo chenye uchafu siku zake za kuwa miezini.

27Naye kila atakayevigusa atakuwa mwenye uchafu, sharti azifue nguo zake pamoja na koga majini, kisha atakuwa mwenye uchafu mpaka jioni.

28Lakini akipata kutakata, kwa kuwa damu yake imekoma, sharti ahesabu siku saba, halafu atakuwa ametakata.

29Siku ya nane na achukue hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga, awapeleke kwa mtambikaji penye kuliingilia Hema la Mkutano.[#3 Mose 15:14.]

30Naye mtambikaji na atengeneze mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, wa pili kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima. Ndivyo, mtambikaji atakavyompatia upozi mbele ya Bwana kwa ajili ya uchafu wake, damu zake ziliomtia.

31Hivi ndivyo, mtakavyowatengesha wana wa Isiraeli na uchafu wao, wasife kwa ajili ya uchafu wao wakilichafua Kao langu lililoko katikati yao.

32Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya mwenye kisonono nayo yake anayejipatia uchafu kwa kutokwa na mbegu akilala;

33tena ya mwanamke akiingia miezini, nayo ya kila mwenye kisonono, kama ni mtu mume, au kama ni mtu mke, nayo ya mtu anayelala na mwanamke aliye mwenye uchafu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania