3 Mose 16

3 Mose 16

Sikukuu ya Mapoza ya kila mwaka.

(Taz. 3 Mose 23:26-32; 4 Mose 29:7-11; Ebr. 9:6-14.)

1Wale wana wawili wa Haroni walipouawa kwa kumtokea Bwana kwa njia isiyopasa, walipokwisha kufa, Bwana akasema na Mose;[#3 Mose 10:1-2.]

2hapo Bwana alimwambia Mose: mwambie kaka yako Haroni, asiingie wakati wo wote Patakatifu ndani ya kile chumba cha mbele ya lile pazia na kukitokea Kiti cha Upozi kilichoko juu ya hilo Sanduku, asipate kufa. Kwani mimi hutokea winguni juu ya hicho Kiti cha Upozi.

3Ila Haroni apaingie Patakatifu akipeleka dume la ng'ombe aliye ndama bado kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo na dume la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima.[#3 Mose 4:3; 1:10.]

4Kuvaa na avae shati takatifu ya ukonge na suruali za ukonge mwilini mwake, nazo azifunge kwa mknda wa nguo y ukonge, tena na ajifunge kilemba cha ukonge, maana haya ndiyo mavazi yake matakatifu; kwanza sharti auogeshe mwili wake majini, kisha na ayavae hayo mavazi.[#2 Mose 28:39,42-43.]

5Kisha na achukue kwa mkutano wa wana wa Isiraeli madume mawili ya mbuzi kuwa ng'ombe za tambiko za weuo na dume moja la kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima.

6Kwanza Haroni na amtoe huyo dume la ng'ombe aliye ng'ombe yake ya tambiko ya weuo, ajipatie upozi mwenyewe nao wa mlango wake.[#Ebr. 7:27.]

7Kisha na awachukue wale madume mawili ya mbuzi, awasimamishe mbele ya Bwana hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano.

8Kisha Haroni na awapigie kura hawa madume mawili, kura moja ya Bwana, ya pili ya Azazeli.[#3 Mose 16:20-22; Mat. 12:43.]

9Kisha Haroni na amtoe dume yule aliyeangukiwa na kura ya Bwana; huyu amtengeneze kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo.

10Naye dume aliyeangukiwa na kura ya Azazeli na amsimamishe mbele ya Bwana, akiwa mzima, atumiwe kuwapatia upozi, wakimtuma kujiendea kwa Azazeli nyikani.

11Na viwe hivyo: Haroni akimtoa huyo dume la ng'ombe aliye ng'ombe yake ya tambiko ya weuo, ajipatie upozi mwenyewe nao wa mlango wake, na amchinje huyo dume la ng'ombe aliye ng'ombe yake ya tambiko ya weuo.

12Kisha na achukue chetezo kinachojaa makaa ya moto yatokayo mezani pa kutambikia mbele ya Bwana na magao mawili ya mavukizo yanukayo vizuri yaliyopondwa kuwa unga, aingie nayo katika chumba cha mbele ya lile pazia.

13Humo na ayatie hayo mavukizo juu ya moto mbele ya Bwana, moshi ya hayo mavukizo ukifunike Kiti cha Upozi kilichoko juu ya Sanduku la Ushahidi, asipate kufa.

14Kisha na achukue damu kidogo ya huyu dume la ng'ombe, ainyunyize kwa kidole chake juu ya Kiti cha Upozi upande wake wa maawioni kwa jua, napo mahali palipo mbele ya Kiti cha Upozi apanyunyizie mara saba hiyo damu kwa kidole chake.

15Kisha na amchinje yule dume la mbuzi aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo ya watu, damu yake nayo na aipeleke ndani ya chumba cha mbele ya lile pazia, kisha na aitumie hiyo damu kuyafanya yaleyale, aliyoyafanya kwa damu ya yule dume la ng'ombe, akiinyunyizia Kiti cha Upozi na mahali palipo mbele ya Kiti cha Upozi.[#Rom. 3:25.]

16Ndivyo, atakavyopapatia Patakatifu upozi, machafu ya wana wa Isiraeli na mapotovu yao yapatoke, maana makosa yao yote yamo. Kisha nalo Hema la Mkutano na alifanyizie vivyo hivyo, kwa kuwa linakaa nao katikati ya machafu yao.[#3 Mose 17:11.]

17Mle Hemani mwa Mkutano msiwe na mtu ye yote, akiingia kupoza mle Patakatifu, mpaka atakapotoka akiisha kujipatia upozi mwenyewe nao wa mlango wake nao mkutano wote wa Waisiraeli.

18Akitoka na afike penye meza ya kutambikia iliyoko mbele ya Bwana, aipatie upozi nayo akichukua damu kidogo ya yule dume la ng'ombe na ya dume la mbuzi, azipake pembe za meza ya kutambikia pande zote.[#2 Mose 30:10.]

19Kisha ainyunyizie damu kwa kidole chake mara saba, aieue na kuitakasa, machafu ya wana wa Isiraeli yaitoke.

20Akimaliza kupapatia upozi Patakatifu na Hema la Mkutano nayo meza ya kutambikia na amlete yule dume la mbuzi aliye mzima bado.

21Kisha Haroni na aibandike mikono yake yote miwili kichwani pake huyu dume la mbuzi aliye mzima bado, aungame juu yake manza zote za wana wa Isiraeli na mapotovu yao yote na makosa yao yote, ayatwike kichwani pake huyu dume la mbuzi, kisha na ampe mtu aliyewekwa kuwa tayari, ampeleke nyikani, ajiendee.

22Naye huyu dume la mbuzi na azichukue manza zao zote alizotwikwa, azipeleke katika nchi isiyokaa watu; huko nyikani ndiko amwachilie, ajiendee.

23Kisha Haroni sharti aingie Hemani mwa Mkutano kuzivua nguo zake za ukonge, alizozivaa alipoingia Patakatifu, aziweke hapo.

24Nao mwili wake sharti auogeshe majini mahali patakatifu, kisha na azivae nguo zake mwenyewe, kisha atoke, atengeneze ng'ombe yake ya tambiko ya kuteketezwa nzima nayo ya watu, ajipatie upozi mwenyewe, hata watu.

25Nayo mafuta ya ng'ombe ya tambiko ya weuo na ayateketeze kuwa moshi mezani pa kutambikia.

26Naye yule mtu aliyempeleka dume la mbuzi la Azazeli na kumwachilia sharti azifue nguo zake na kuuogesha mwili wake majini, baadaye ataweza kuingia makambini.

27Naye dume la ng'ombe aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo naye dume la mbuzi aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo, ambao damu zao zilipelekwa Patakatifi za kupozea mumo humo, na awapeleke nje ya makambi, wateketeze huko kwa moto ngozi zao na nyama zao na mavi yao.[#3 Mose 4:12; 6:30; Ez. 43:21; Ebr. 13:11.]

28Naye atakayeziteketeza sharti azifue nguo zake na kuuogesha mwili wake majini, baadaye ataweza kuingia makambini.

29Haya na yawe kwenu maongozi ya kale na kale: katika mwezi wa saba siku ya kumi ya mwezi huu sharti mjitese wenyewe, msifanye kazi yo yote, wala wenyeji wala wageni walioko kwenu!

30Kwani siku hiyo ndipo, watakapowapatia upozi na kuwaeua, makosa yenu yote yawatoke, mpate kuwa wenye kutakata mbele ya Bwana.[#Ebr. 10:3.]

31Siku hiyo ya mapumziko sharti iwe kwenu ya mapumziko kabisa; ndipo, mtakapojitesa kwa kufunga. Haya ndiyo maongozi ya kale na kale.

32Mwenye kupoza sharti awe mtambikaji, waliyempaka mafuta na kulijaza gao lake, apate kutambika mahali pa baba yake, naye sharti azivae hizo nguo za ukonge, maana ndizo nguo zipasazo Patakatifu.

33Kisha na apapatie upozi Patakatifu penyewe nalo Hema la Mkutano, nayo meza ya kutambikia na aipatie upozi, nao watambikaji wote pamoja na watu wote wa huu mkutano na awapatie upozi.

34Haya sharti yawe kwenu maongozi ya kale na kale ya kuwapatia upozi wana wa Isiraeli kila mwaka mara moja, makosa yao yote yawatoke. Naye akayafanya, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania