3 Mose 20

3 Mose 20

Mapatilizo ya makosa makubwa.

(Taz. 3 Mose 18.)

1Bwana akamwambia Mose kwamba:

2Waambie wana wa Isiraeli: Mtu ye yote, kama ni mwana wa Isiraeli au kama ni mgeni akaaye ugenini kwao Waisiraeli atakayetoa hata mmoja tu miongoni mwao walio wa uzao wake na kumpa Moloki sharti auawe, watu wa nchi hiyo sharti wamtupie mawe.

3Nami nitamkazia macho mtu aliye hivyo, nimng'oe katikati yao walio ukoo wake, kwani miongoni mwao walio wa uzao wake ametoa mtu wa kumpa Moloki, kusudi apapatie Patakatifu pangu uchafu, alibezeshe nalo Jina langu takatifu.

4Ijapo watu wa nchi hiyo wayapofushe macho yao, wakiyaona, mtu yule aliyoyafanya alipotoa mtu miongoni mwao walio wa uzao wake na kumpa Moloki, wasipate kumwua,

5mimi na nimkazie macho yangu mtu aliye hivyo nao walio wa kizazi chake, nimng'oe yeye pamoja nao wote waliomfuata na kuufanya ugoni wake wa kumfuata Moloki kufanya ugoni naye, basi, na niwang'oe, watoweke katikati yao walio ukoo wao.

6Hata mtu akiwageukia waganga wa kutiisha mizimu na waaguaji, kufanya ugoni nao, na nimkazie macho yangu aliye hivyo, na nimg'oe katikati yao walio ukoo wake.[#3 Mose 19:31.]

7Kwa hiyo jitakaseni, mpate kuwa watakatifu! Kwani mimi Bwana ni Mungu wenu.[#3 Mose 19:2.]

8Yaangalieni maongozi yangu, myafanye! Mimi ni Bwana anayewatakasa ninyi.[#3 Mose 19:37.]

9Mtu ye yote atakayemwapiza baba yake au mama yake sharti auawe kabisa; akimwapiza baba yake au mama yake atakuwa amekora manza za kumwagwa damu yake.[#2 Mose 21:17.]

10Mtu akizini na mke wa mwingine, basi, yeye aliyezini na mke wa mwenzake sharti auawe, mwenyewe pamoja na mwanamke, aliyezini naye.[#2 Mose 20:14; Yoh. 8:5.]

11Mtu atakayelala na mkewe baba yake atakuwa ameufunua uchi wake baba yake; kwa hiyo wote wawili sharti wauawe, maana wamekora manza za kumwagwa damu zao.

12Mtu akilala na mke wa mwanawe, sharti wauawe wote wawili, maana wamefanya uchafu ulio mbaya zaidi, nao wamekora manza za kumwagwa damu zao.

13Mtu akilala na mwanamume mwingine, kama wanavyolala na mwnamke, wamefanya tapisho, wote wawili sharti wauawe, maaana wamekora manza za kumwagwa damu zao.

14Mtu akimchukua mwanamke pamoja na mama yake, ni ugoni, sharti wamteketeze kwa moto pamoja nao wale wanawake, ugoni ulio hivyo usiwe kwenu.

15Mtu akilala na nyama sharti auawe, hata huyo nyama sharti mmwue.

16Mwanamke akimkaribia nyama ye yote kulala naye, sharti mmwue huyo mwanamke pamoja na huyo nyama, wafe kabisa, maana wamekora manza za kumwagwa damu zao.

17Mtu akimchukua umbu lake aliye binti baba yake au binti mama yake, auone uchi wake, naye auone uchi wake yeye mwenyewe, ni tendo litwezalo, nao sharti wang'olewe machoni pao walio wana wa ukoo wao, maana ameufunua uchi wa umbu lake; hizi manza, alizozikora, zitamkalia.

18Mtu akilala na mwanamke aliye miezini, akiufunua uchi wake na kukitokeza waziwazi kijito chake, naye mwanamke akikifunua kijito cha damu yake, wote wawili sharti wang'olewe katikati yao walio ukoo wao.

19Uchi wa mama yako mkubwa na mdogo nao uchi wa shangazi yako usiufunue, kwani ni kuutokeza waziwazi uchi wao walio ndugu wa kuzaliwa nao; hizo manza, walizozikora, zitawakalia.

20Mtu akilala na mkewe baba yake mkubwa au mdogo, ameufunua uchi wa baba yake mkubwa au mdogo, nao huu ukosaji wao utawakalia, wafe pasipo kuzaa watoto.

21Mtu akimchukua mkewe mkubwa au mdogo wake, ni uchafu, maana ameufunua uchi wa ndugu yake wa kuzaliwa naye, nao watakufa pasipo kuzaa watoto.

22Yaangalieni maongozi yangu yote na maamuzi yangu yote, myafanye, ile nchi isiwatapike, nitakapowapeleka, mkae huko.

23Msiyafuate maongozi ya wamizimu, nitakaowafukuza mbele yenu. Kwa kuwa waliyafanya hayo makosa yote, nalichukizwa nao.

24Kwa hiyo niliwaambia ninyi: Ninyi mtaichukua nchi yao, iwe yenu, mimi nitawapa kuichukua hiyo nchi ichuruzikayo maziwa na asali. Mimi ni Bwana Mungu wenu niliyewatenga na kuwatoa katika makabila mengine.

25Nanyi mwapambanue nyama wenye kutkata nao wenye uchafu, nao ndege wenye uchafu nao wenye kutakata, msijifanye wenyewe kuwa tapisho kwa ajili ya nyama na ndege, wala kwa ajili ya wadudu wote watambaao katika nchi, niliowatenga kuwa kwenu wenye uchafu.[#3 Mose 11:25.]

26Ndipo, mtakapokuwa watakatifu wangu, kwani mimi Bwana ni mtakatifu, nikawatenga ninyi na kuwatoa katika makabila yote, mwe wangu.

27Mtu mume au mke akiwa mwenye roho ya kutiisha mizimu au mwenye roho ya kuagua sharti wauawe kwa kupigwa mawe, maana wamekora manza za kuuawa.[#2 Mose 22:18.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania