The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:
2Mwambie Haroni nao wanawe, wajiangalie sana kwa ajili ya vipaji vitakatifu vya wana wa Isiraeli wasilibezeshe Jina langu takatifu, maana wanavitoa kuwa vitakatifu vyangu mimi Bwana.
3Waambie: Hivi vinavipasa vizazi vyenu vitakavyokuwa: mtu ye yote aliye wa uzao wenu wo wote akavifikia karibu vipaji vitakatifu, wana wa Isiraeli wanavyomtolea Bwana kuwa vitakatifu vyake, basi, akivikaribia na kuwa mwenye uchafu, sharti ang'olewe, atoweke usoni pangu; mimi ni Bwana.
4Mtu ye yote aliye wa uzao wake Haroni akiwa mwenye ukoma au kisonono asile vipaji vitakatifu, mpaka atakapokuwa mwenye kutakata. Atakayegusa mtu aliyejipatia uchafu kwa mfu au aliyetokwa na mbegu alipolala usingizi,[#3 Mose 15:2,16.]
5au mtu atakayegusa dudu ye yote wa kumpatia uchafu au atakayegusa mtu wa kumpatia uchafu kwa kuwa mwenye uchafu wo wote,
6basi, atakayegusa cho chote kilicho hivyo ni mwenye uchafu mpaka jioni, kisha asile vitakatifu, asipokuw ameuogesha mwili wake majini.[#3 Mose 11:24-25.]
7Jua likiisha kuchwa, atakuwa mwenye kutakata; ndipo, atakapoweza kula vitakatifu, kwani ndio chakula chake.
8Nyama aliyekufa kibudu au aliyeraruliwa na nyama mwingine asile, asijipatie uchafu kwake. Mimi ni Bwana.[#2 Mose 22:31.]
9Na wayaangalie maagizo yangu yawapasayo kuyaangalia, wasijitwike kosa la kuyakosea, wakauawa nalo kwa kuchafua vitakatifu. Mimi ni Bwana anayewatakasa.
10Lakini mgeni ye yote asile kilicho kitakatifu, wala mtu akaaye mwa mtambikaji wala amfanyiaye kazi ya mshahara asile kilicho kitakatifu.
11Lakini mtambikaji akinunua mtumishi kwa fedha zake, yeye ataweza kula; nao watumwa watakaozaliwa nyumbani mwake wataweza kula hicho chakula chake.
12Tena binti mtambikaji akiolewa na mtu mgeni hana ruhusa kula vipaji vitakatifu vya kunyanyuliwa.
13Lakini binti mtambikaji atakapokuwa mjane au atakapofukuzwa na mumewe hakuzaa watoto, kisha akirudi kukaa nymbani mwa baba yake, kama akiwa alivyokaa katika ujana wake, ataweza kukila chakula cha baba yake; lakini mgeni ye yote asikile.
14Mtu akila kitakatifu pasipo kukijua, sharti amrudishie mtambikaji hicho kitakatifu na kukiongezea fungu lake la tano.[#3 Mose 5:16.]
15Watambikaji wasivichafue vipaji vitakatifu vya wana wa Isiraeli, wanavyomnyanyulia Bwana,
16huku ni kwamba, wasiwakoseshe Waisraeli kukora manza za kula wenyewe vipaji vyao vitakatifu. Kwani mimi ni Bwana anayevitakasa.[#3 Mose 22:9.]
17Bwana akamwmbia Mose kwamba:
18Sema na Haroni na wanawe na wana wote wa Isiraeli na kuwaambia: Mtu ye yote, kama ni wa mlango wa Isiraeli, au kama ni mgeni akaaye kwao Waisiraeli, akitaka kutoa toleo lake, kama ni la kulipa yo yote, aliyoyaapa, au kama ni kwa kupendezwa tu, basi, mtu akitaka kumtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima
19ya kujipendezesha kwake, sharti iwe dume asiye na kilema, kama ni la ng'ombe au la kondoo au la mbuzi.
20Kila nyama mwenye kilema msimtoe, kwani hatawapendezesha kwake.[#5 Mose 15:21; 17:1; Mal. 1:8.]
21Hata mtu akitaka kumtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya shukrani, kama ni ya kuyalipa aliyoyaapa, au kama ni ya kupenda kwa moyo tu, kama anatoa ng'ombe au kama anatoa mbuzi au kondoo, sharti awe pasipo kilema, apate kupendeza, asiwe nyama mwenye kilema cho chote,
22kama mwenye upofu au mwenye kuvunjika kiungo au mwenye kidonda au mwenye majipu au mwenye kifua kikuu au mwenye upele; nyama aliye hivyo msimtolee Bwana, wala msimteketezee Bwana vipande vyake mezani pa kutambikia.
23Ng'ombe au kondoo mwenye viungo virefu zaidi au mwenye viungo vifupi zaidi utaweza kumtoa ukipenda mwenyewe kwa moyo, lakini haitafaa kumtoa kuwa wa kuyalipa uliyoyaapa.
24Nyama mwenye mapumbu yaliyopondwa au yaliyosetwa au yaliyovunjwavunjwa au nyama aliyekatwa mapumbu kabisa msimtolee Bwana. Mtakapofika katika nchi yenu msivifanye.
25Ijapo mpewe nyama walio hivyo na mtu mgeni, msimtolee Mungu wenu mmoja tu aliye hivyo kuwa chakula chake, kwani nyama hao sio wazima, ni wenye vilema; kwa hiyo hawatawapendezesha.
26Bwana akamwambia Mose kwamba:[#2 Mose 22:30.]
27Ng'ombe au kondoo au mbuzi akiisha kuzaliwa sharti akae siku saba kwa mama yake. Tangu siku ya nane na baadaye atafaa wa kumtolea Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa.
28Lakini ng'ombe au kondoo msimchinje siku moja pamoja na mtoto wake.[#5 Mose 22:6-7.]
29Mkimtolea Bwana ng'ombe ya tambiko ya kumtukuza, sharti mmchinje kwa njia itakayowapendezesha.
30Sharti aliwe siku iyo hiyo, msisaze hata kidogo mpaka kesho. Mimi ni Bwana.[#3 Mose 7:15.]
31Yaangalieni maagizo yangu, myafanye! Mimi ni Bwana.[#3 Mose 22:9,16.]
32Msilichafue Jina langu takatifu, nipate kutakaswa katikati yao wana wa Isiraeli. Mimi ni Bwana anayewatakasa ninyi.
33Niliwatoa ninyi katika nchi ya Misri, niwe Mungu wenu, mimi Bwana.