3 Mose 9

3 Mose 9

Ng'ombe ya tambiko ya kwanza ya Haroni na ya wanawe inateketezwa.

1Siku ya nane Mose akamwita Haroni nao wanawe na wazee wa Isiraeli,[#3 Mose 8:33.]

2akamwambia Haroni: Jichukulie ndama dume, awe ng'ombe ya tambiko ya weuo, tena dume la kondoo, awe ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, wote wawili wawe pasipo kilema, uwatoe mbele ya Bwana.

3Nao wana wa Isiraeli waambie kwamba: Chukueni dume la mbuzi, awe ng'ombe za tambiko ya weuo, tena ndama na mwana kondoo wa mwaka mmoja wasio na kilema, wawe ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima.

4Tena chukueni dume la ng'ombe na la kondoo, wawe ng'ombe z tambiko za shukrani wa kuwachinja mbele ya Bwana na vilaji vya tambiko vilivyochanganywa na mafuta. Kwani leo Bwana atawatokea ninyi.

5Wakayachukua yote, Mose aliyowaagiza, wakayapeleka hapo mbele ya Hema la Mkutano; nao mkutano wote ulipokuja, wakasimama mbele ya Bwana.

6Mose akasema: Hili ndilo neno, Bwana aliloliagiza, mlifanye, utukufu wa Bwana uwatokee.

7Kisha Mose akamwambia Haroni: Ikaribie meza ya kutambikia, utengeneze ng'ombe yako ya tambiko ya weuo nayo ya kuteketezwa nzima, ujipatie upozi mwenyewe! Tena kwa ajili ya watu nao litengeneze nalo toleo lao hawa watu, uwapatie upozi nao, kama Bwana alivyoyaagiza![#3 Mose 16:6,11,15; Ebr. 5:3; 7:27.]

8Ndipo, Haroni alipoikaribia meza ya kutambikia, akamchinja ndama wake wa kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo.

9Nao wanawe Haroni wakampelekea hiyo damu, naye akakichovya kidole chake katika damu, akazipaka pembe za meza ya kutambikia, nayo damu nyingine akaimwagia misingi ya meza ya kutambikia.

10Nayo mafuta na mafigo na kile kipande cha ini cha hiyo ng'ombe ya tambiko ya weuo akayachoma moto mezani pa kutambikia, kama Bwana alivyomwagiza Mose.[#3 Mose 4:8-12.]

11Nazo nyama na ngozi akaziteketeza kwa moto nje ya makambi.

12Tena alipomchinja ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, wanawe Haroni wakampelekea hiyo damu, naye akainyunyiza pande zote juu ya meza ya kutambikia.[#3 Mose 1:10-13.]

13Hiyo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima ilipokwisha kuchanguliwa, wakampelekea vipande vyake pamoja na kichwa, naye akavichoma moto mezani pa kutambikia.

14Alipokwisha kuuosha utumbo na miguu akaichoma moto juu ya hiyo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima mezani pa kutambikia.

15Kisha akayatoa matoleo ya watu. Akamchukua dume la mbuzi aliye ng'ombe ya tambiko ya weuo ya watu, akamchinja na kumtoa kama yule wa kwanza, awe ng'ombe ya tambiko ya weuo.

16Akaitoa nayo ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, akaifanya kama desturi.

17Alipovitoa vilaji vya tambiko akalijaza gao lake humo, akavichoma moto mezani pa kutambikia penye ng'ombe ya tambiko ya asubuhi ya kuteketezwa nzima.

18Kisha akamchinja dume la ng'ombe na dume la kondoo walio ng'ombe za tambiko za shukrani za watu, nao wanawe Haroni wakampelekea hizo damu, akazinyunyiza pande zote juu ya meza ya kutambikia.

19Nayo mafuta ya dume la ng'ombe, nayo ya dume la kondoo: mkia nayo yaufunikayo utumbo na mafigo na kile kipande cha ini,

20haya mafuta wakayaweka juu ya vidari, naye Haroni akayachoma moto haya mafuta mezani pa kutambikia.

21Lakini kidari na paja la kuume Haroni akavipitisha motoni huku na huko kuwa vipaji vya tambiko vya kupitishwa motoni mbele ya Bwana, kama Mose alivyoagiza.[#3 Mose 7:30-34.]

22Kisha Haroni akawainulia watu mikono yake, akawabariki. Alipokwisha akashuka na kutoka hapo, alipozitoa ng'ombe za tambiko za weuo na za kuteketezwa nzima na za shukrani.[#4 Mose 6:22-27.]

23Kisha Mose na Haroni wakaingia Hemani mwa Mkutano; napo walipotoka wakawabariki hao watu, ndipo, utukufu wa Bwana ulipowatokea watu wote.[#2 Mose 40:34.]

24Moto ukatoka mbele ya Bwana, ukaila juu ya meza ya kutambikia ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima pamoja na yale mafuta. Watu wote walipoviona wakapiga shangwe na kuanguka kifudifudi.[#2 Mambo 7:1.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania